May 05, 2024 03:20 UTC
  • Jumapili, 5 Mei, 2024

Leo ni Jumapili 26 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria mwafaka na 5 Mei 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.  ***

Karl Heinrich Marx

 

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni. Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya. Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya. ***

Napoleon Bonaparte

 

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Bobby Sands mwanamapambano maarufu wa Ireland baada ya kukaa katika jela ya Uingereza kwa wiki kadhaa na kugoma kula chakula kwa muda wa siku 66 katika kupigania uhuru wa Ireland ya Kaskazini. Serikali ya kikoloni ya Uingereza ilikabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kufuatia kifo cha Bobby Sands na wanaharakati wenzake wa Ireland ambao waligoma kula chakula wakiwa katika jela za nchi hiyo. ***

Bobby Sands

 

 Na tarehe 5 Mei imetangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirikisho la Kimataifa la Wakunga kuwa ni ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga. Siku hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza kuwa Siku ya Kimataifa ya Wakunga mwaka 1980 na kutangazwa rasmi mwaka 1992. Lengo la kuainishwa siku hii kuwaenzi wakunga na kazi ya ukunga, kuzidisha uelewa na kubadilishana maarifa na taarifa zinazohusiana na afya ya akina mama na watoto wachanga na vilevile kuonyesha umuhimu wa kazi za wakunga. ***