UNESCO: Al Khalil (Hebron) ni turathi ya kimataifa ya Palestina
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeuweka mji wa al Khalil na Haram ya Nabii Ibrahim (as) katika orodha ya turathi za kimataifa zinazokabiliwa na hatari ya kutoweka na limelaani vikali hatua za utawala ghasibu wa Israel katika eneo hilo.
Kabla ya hapo taasisi hiyo ya kimataifa ilikuwa tayari imepasisha azimio kwa maslahi ya watu wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa ni mji unaokaliwa kwa mabavu.
Mkutano wa 40 wa Kamati ya Turathi ya Unesco ulifanyika mwezi huu katika mji wa Kraków huko Poland ambapo jumuiya hiyo iliutambua mji wa al Khalil (Hebron) huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel kuwa ni turathi ya kimataifa. Mji wa kihistoria wa Yazd nchini Iran, sehemu ya kale ya mji wa Ahmamadabad huko India na sehemu moja ya mji wa Strasbourg nchini Ufaransa ni miongoni mwa maeneo yaliyowekwa kwenye orodha hiyo.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameshambulia vikali azimio hilo la UNESCO kuhusu mji wa al Khalil na kuutaja uamuzi huo kuwa ni upuuzi. Netanyahu amesema katika ujumbe wa video kwamba: Huu ni miongoni mwa maamuzi ya kipuuzi yaliyopasishwa na Umoja wa Mataifa.
Baada ya hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kuliweka eneo la kale la mji wa al Khalil katika orodha ya turathi za kimataifa zinazokabiliwa na hatari ya kutoweka, utawala wa Kizayuni wa Israel umetangaza kwamba, utajenga jumba la makumbusho la hisroria ya Mayahudi katika mji huo.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetangaza kuwa, Netanyahu amechukua uamuzi wa kupunguza dola milioni moja katika fedha za haki ya uanachama wa dola hilo katika Umoja wa Mataifa ikiwa ni kulalamikia uamuzi wa UNESCO na kwamba, fedha hizo zitatumika kujenga jumba la makumbusho la historia ya Mayahudi walioishi katika mji wa al Khalil.
Israel iliukalia kwa mabavu mji wa al Khalil na maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Baitul Muqaddas Mashariki na Ukanda wa Gaza katika vita vya mwaka 1967 na Waarabu na inayadhibiti maeneo hayo tangu wakati huo licha ya malalamiko na ukosoaji mkubwa wa jamii ya kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel pia imeitaja hatua ya UNESCO kuwa ni doa la fedheha na aibu katika kipaji cha uso wa jumuiya hiyo ya kimataifa!
Baada ya uamuzi huo wa UNESCO wa kuitambua sehemu ya kale ya mji wa al Khalil kuwa ni ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel, Marekani imetangaza kuwa, itatazama upya uhusiano wake na UNESCO. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikkiy Haley ameutaja uamuzi wa UNESCO kuwa ni kuivunjia heshima historia! Haley amedai kuwa, azimio hilo la UNESCO litakwamisha juhudi za serikali ya Donald Trump za kutaka kuhuisha mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina!
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Marekani ambayo ni miongoni mwa wanachama 58 wa Baraza la Utendaji la UNESCO haina haki ya kupiga kura katika vikao vya taasisi hiyo ya kimataifa.
Kamati ya Turathi za Kimataifa ya UNESCO imelinda uhuru na kujitawala kwake licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na balozi wa Israel katika mkutano huo kwa ajili ya kuzuia uamuzi wowote wa kamati hiyo kwa maslahi ya Wapalestina. Katika kura iliyopigwa katika mkutano huo, Kamati ya Turathi za Kimataifa ya UNESCO imeliweka eneo la kale la mji wa al Khalil (Hebron) na Haram ya Nabii Ibrahim katika orodha ya turathi zinazokabiliwa na hatari ya kuangamia kutokana na uvamizi wa dola ghasibu la Israel. Uamuzi huo umekabiliwa na majibu ya kifedhuli na yasiyo na adabu ya balozi wa Israel katika shirika hilo la kimataifa. Balozi huyo alisema mwishoni mwa hotuba yake kwamba, analazimika kwenda chooni, kwa sababu kitendo hicho ni muhimu zaidi kwake kuliko kushiriki kwenye mkutano kama huo wa UNESCO! Hadhirina na wawakilishi wa nchi mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo, kwa pamoja, walimzomea na kumpiga vijembe balozi huyo wa Israel wakati alipokuwa akiondoka kwenye mkutano huo. Hata hivyo wajumbe wa Kamati ya Turathi za Kimataifa wa UNESCO wamepasisha uamuzi huo licha ya malalamiko makali ya balozi wa Israel katika jumuiya hiyo, Carmel Shama. Azimio hilo limesisitiza kuwa: Mji wa al Khalil ambao ndio mkubwa zaidi wa eneo la Ukingo wa Magharibi na uko umbali wa kilomita 30 kusini mwa Baitul Muqaddas (Jerusalem), ni turathi ya kimataifa ya UNESCO. Hatua hii inahesabiwa kuwa ushindi mwingine wa kidiplomasia wa Wapalestina dhidi ya Israel inayolikalia kwa mabavu eneo hilo.
Mji wa al Khalil ambao una historia ya maelfu ya miaka, una jamii ya Wapalestina Waislamu laki mbili na katika miaka ya hivi karibuni umevamiwa na Wazayuni baada ya Israel kujenga vitongoji kadhaa vya walowezi wa Kiyahudi karibu ya maeneo ya kihistoria ya mji huo, suala ambalo linahatarisha na kutishia uhai wa maeneo hayo. Azimio la UNESCO limesisitiza juu ya utambulisho wa Kiislamu wa eneo la kale la mji wa al Khalil (Hebron).
Mwezi Mei mwaka jana wa 2016 pia Kamati ya Utendaji ya UNESCO ilipasisha azimio lililoulaani utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kukiuka sheria za kimataifa katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na Ukanda wa Gaza na kutoa wito wa kuheshimiwa utambulisho wa kihistoria wa mji huo. Azimio hilo pia liliutaka utawala ghasibu wa Israel kuheshimu utambulisho wa Kiislamu wa Msikiti wa al Aqsa na Haram ya Nabii Ibrahim. UNESCO ilisema katika azimio hilo kwamba, lengo la kuweka kipengee kinachosisitiza kuwa Baitul Muqaddas ni eneo tukufu kwa wafuasi wa dini tatu zinazompwekesha Mwenyezi Mungu yaani Waislamu, Wakristo na Wayahudi, ni kuzuia mikakati inayofanywa na Israel ya kutaka kuuyahudisha mji huo. Azimio hilo liliutambua mji huo wa Jerusalem kuwa ni eneo llililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu.
UNESCO pia iliukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kuchimba mashimo ya chini kwa chini katika eneo la mashariki mwa Baitul Muqaddas na eneo la kale la mji huo na kutangaza kuwa, mienendo ya utawala huo katika miji ya Gaza na Bait Laham (Bethlehem) pia inakiuka sheria za kimataifa.
Baada ya uamuzi wa UNESCO kuhusu mji wa al Khalil, Waziri Utalii na Turathi za Kale wa Palestina Rula Maa’yaa amesema kuwa, tukio hilo ni la kihistoria linalodhihirisha tena utambulisho wa Kipalestina wa mji wa al Khalil (Hebron) na Haram ya Nabii Ibrahim. Amesisitiza kuwa, azimio la taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa limefichua tena uongo wa madai ya utawala haramu wa Israel unaotaka eneo hilo liwekwe katika orodha ya turathi za Mayahudi.
Mji wa al Khalil (Hebron) ni miongoni mwa miji ya kale zaidi ya Palestina na una hitoria ya miaka elfu sita. Mji huo unahesabiwa kuwa mtakatifu kwa wafuasi wa dini zote za mbinguni. Mji huo unahesabiwa kuwa wa nne kwa utukufu baina ya Waislamu kwa ujumla baada ya miji ya Makka, Madina na Quds, na turathi muhimu zaidi ya mji huo ni Haram ya Nabii Ibrahim al Khalil (as). Mji huo una majengo mengi ya kale na ya kihistoria likiwemo jengo lenye makaburi ya Manabii Ibrahim, Is'haq na Yaaqub (as) na wake zao. Kwa sababu hiyo unatambuliwa pia kuwa ni eneo takatifu kwa wafuasi wa dini zote za mbinguni.
Baada ya vita vya mwaka 1967 utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mikakati ya kuibadilisha Haram ya Nabii Ibrahim na kuifanya maabadi na eneo la ibada la Wayahudi. Utawala huo pia umekuwa ukifanya njama za kubadili utambulisho wa mji huo na kuweka maandishi ya Kiebrania katika maeneo ya kale na ya kihistoria katika jitihada za kuufanya uonekane kuwa ni wa Kiyahudi. Mji huo una misikiti 50 ya kale na mipya, na mashuhuri zaidi ni Msikiti Mkuu wa Nabi Yunus (as) kandokando ya kaburi na Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. Chimbuko na maana ya jina la Hebron linalotumiwa kwa ajili ya mji wa al Khalil ni urafiki, ambayo pia ndiyo maana ya jina la Alkhalil na laqabu ya Nabii Ibrahim (as), yaani Ibrahim Khalilullah.
Miongoni mwa matukio muhimu na ya kihistoria ya mji huo ni pamoja na mauaji ya umati yaliyofanywa na Mzayuni Baruch Goldstein dhidi Waislamu wa mji huo katika siku ya Idul Fitri mwaka 1994. Baruch Goldstein ambaye ni Myahudi wa Marekani aliyehamia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, aliingia katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim katika mji wa al Khalil na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa katika ibada ya Swala. Waislamu 29 waliuawa shahidi na wengine 125 walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya kinyama.