Ujumbe na Ibra Tunazopata Katika Tukio la Ashura
Assalamu alaykum wasikilizaji wetu wapenzi warahmatullahi wabarakatuh. Mapambano ya Imam Hussein (as) na wafuasi wake waaminifu yalichukua muda usiotimia hata siku moja; na shakhsia wote hao wakubwa na waliokomboka wakauliwa shahidi na jeshi kubwa la Yazid mwana wa Muawiyah, mwana wa Abu Sufyan.
Pamoja na hayo, harakati na vuguvugu hilo adhimu na takatifu limebakisha mafunzo, ujumbe na ibra chungu nzima kwa Waislamu na wanadamu wote duniani, kwa sababu harakati ya Ashura inatokana na fitra na maumbile ya kiutu na akili timamu ya urazini; na mengi yaliyomo kwenye ujumbe wake yanawahutubu walimwengu wote. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wanafikra na wanasiasa wengi wasio Waislamu wameandika vitabu na makala kadha wa kadha kuhusu malengo matukufu ya Hussein Ibn Ali (as) na kumwenzi mtukufu huyo. Katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa leo tutagusia baadhi ujumbe na mafunzo yaliyomo kwenye harakati adhimu ya Ashura.
Mapambano ya Imam Hussein (as) yalikuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; na yeye Imam alitawakali na kumtegemea Allah pekee katika mapambano yake hayo na ikawa sahali na wepesi kwake kuvumilia tabu zote zilizomfika kwenye harakati hiyo ya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuanzia kabla, wakati na baada ya siku ya tukio la Ashura, huo ndio msingi alioutilia mkazo mara kadhaa yeye mwenyewe pamoja na wafuasi wake. Wakati anaagana kwa majonzi na watu wa nyumba yake, kwa imani thabiti aliyokuwa nayo kwa Mola wake, Hussein Ibn Ali aliwahutubu watu wake: "Jueni kwamba Allah ndiye mlinzi wenu na ndiye atakayekuhifadhini; karibuni hivi atakuokoeni na shari ya maadui na ataufanya mwisho wenu uwe wa kheri". Wakati anakaribia kuuawa shahidi pia Imam huyo shahidi alimuelekea Mola wake na kusema: "ewe Mola wangu, mimi nimeridhia hukumu yako na nimejisalimisha kwa uamuzi na irada yako. Hakuna mwabudiwa yeyote ghairi yako, ewe kimbilio la kila mtafuta kimbilio". Kwa hakika imani na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu ndiko kulikomfanya Imam Hussein (as) na wafuasi wake watende kila walilotenda kwa ikhlasi na kwa kutaka radhi za Mola; na Yeye Allah akaifanya kumbukumbu ya mapambano yao idumu daima dawamu.
Imani hiyo thabiti na kumtegemea Mwenyezi Mungu Muweza na Mwenye hikima viliwapa ushujaa wa kuweza kusimama imara kukabiliana na jeshi la batili; na hilo ni somo na funzo jengine la harakati ya Ashura. Katika usiku wa Ashura wakati Hussein Ibn Ali (as) alipowaeleza wafuasi wake kwamba kutokana na hatari ya mauati isiyo na shaka inayowakabili mbele yao kama wanataka kuondoka kwenye medani ya vita waitumie fursa ya giza hilo la usiku kunusuru maisha yao, kutokana na imani ya kweli juu ya Allah na shauku ya kufa shahidi waliyokuwa nayo, masahaba hao waaminifu walisisitiza kwamba watasimama katika njia ya haki na kumhami mtukufu huyo hadi pumzi yao ya mwisho. Mmoja wao Saad Ibn Abdullah alitamka haya kumwambia Imam Hussein (as): “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, kama nitajua kwamba nitauawa mara sabini na mwili wangu utachomwa moto kisha jivu langu lipewe uhai tena katu sitoacha kukupa msaada, bali kila nitapopewa uhai tena nitasimama kukusaidia…” Kutokana na kuwa na moyo wa aina hiyo, wafuasi wa Imam Hussein (as) walipambana kuilinda dini ya Allah na kumhami mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Kupigania haki, ukombozi, izza na heshima ni ujumbe na mafunzo muhimu ya tukio la Ashura kwa walimwengu wote wa kila zama. Kipimo alichotumia Imam Hussein (as) katika mapambano yake kilikuwa ni kusimamisha haki na uadilifu na kuishinda batili na dhulma. Yazid, alikuwa mtawala mwovu na asiye na ustahiki, aliyeshika hatamu za ukhalifa wa Waislamu kidhulma; na kumtaka Imam Hussein ampe mkono wa bai’a na kuukubali ukhalifa wake kwa nguvu. Mtukufu huyo alilizungumzia jambo hilo kwa ushujaa na kwa uwazi kabisa aliposema: “Tambueni kwamba mchafu huyu mwana wa haramu amenifanya nichague moja kati ya mawili: ama nivute upanga na kuwa tayari kwa vita au nivae vazi la udhalili na kumpa mkono wa bai’a Yazid; lakini udhalili uko mbali na sisi; kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mtume wake, waumini na malezi safi tuliyokulia hayaturuhusu kukubali udhalili”. Katika mahali pengine, Hussein Ibn Ali (as) anasema: “Kufa kwa izza na heshima ni bora, kuliko kuishi kwa udhalili na unyonge”. Kwa utaratibu huo, mtukufu huyo aliwaonyesha watu njia ya heshima na ukombozi na kukuelezea kuishi kwa madhila katika pingu za dhulma kuwa ni sawa na kuwa mfu”. Kwa hivyo ili kukomboka na kuwa huru inatupasa kupambana kuwatokomeza madhalimu na wavamizi kwa ajili ya kuwa na izza, uhuru na uadilifu. Malengo haya matukufu yana thamani aali na ya juu mno kiasi kwamba pale inapobidi, inampasa mtu awe tayari kujitolea mhanga roho yake na kila alichonacho ili aweze kuyafikia.
Kuyafikia malengo aali na matukufu kama uadilifu, heshima na uhuru kunathibiti kwa kukidhi masharti yake; na bila shaka muhimu zaidi kati ya masharti hayo ni basira ya uono mpana na uelewa. Mapambano ya Ashura yameonyesha kuwa pasi na kuwa na basira na uono mpana na wa mbali, hata weledi na wenye vipawa katika jamii hushindwa kubaini njia ya haki na muelekeo sahihi wa kufuata. Ni kama ilivyotokea Karbala, ambapo watu waliomwandikia barua ya wito Imam Hussein (as), walimgeuka mtukufu huyo wakajipanga safu moja kupambana naye isipokuwa watu 72 tu ndio walioweza kumaizi na kuitambua njia sahihi, wakajitolea mhanga roho zao kuuhami Uislamu na Imam Hussein na hivyo kumbukumbu yao kubakia milele katika historia. Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameifanyia upembuzi wa kina ibra hiyo ya Ashura kwa kueleza kwamba: "Umma wa Kiislamu una sababu ya kujiuliza, kwamba ilikuwaje baada ya miaka hamsini tangu kuaga dunia Mtume, ilifika hadi katika nchi ya Kiislamu Waislamu haohao wakiwemo mawaziri wao, maamiri wao, majemedari wao, maulamaa wao, maqadhi wao na maqarii wao wa Qur'ani walikusanyika Kufa na Karbala wakamwaga damu kwa kumuua kikatili na kinyama namna ile kipenzi cha Mtume wao huyo? Lazima mtu atafakari kwa kina na kujiuliza, kwa nini ikawa hivyo?... Laiti kama weledi watachukua hatua kwa wakati, kwa kufanya linalotakiwa, historia itaokoka; na akina Hussein Ibn Ali hawatofikishwa Karbala..." Yeye mwenyewe Imam Hussein (as) amewahutubu maulamaa wakiwa ndio viongozi wa kifikra na kidini wa jamii kwamba: "Enyi kundi la maulamaa wa dini! Kama hamtotusaidia na kuwa sauti moja na sisi katika kusimamia uadilifu na haki, madhalimu watapata nguvu zaidi dhidi yenu na kuchukua hatua zaidi za kuuzima mwenge wa nuru ya Utume".
Wakati Imam Hussein (as) alipoondoka Madina alimkabidhi wasia ndugu yake Muhammad Hanafiyyah ambao sehemu yake moja inasema: "...Mimi nimetoka kwa ajili ya kuurekebisha umma wa babu yangu Muhammad SAW; na ninataka kuamrisha mema na kukataza mabaya na kufuata mwenendo wa babu yangu Muhammad SAW na baba yangu Ali bin Abi Talib (as)". Mtukufu huyo alihisi kuwa dini ya babu yake iko hatarini na hakuna vinginevyo vya kufanya isipokuwa kuamrisha mema na kukataza mabaya; na huu pia ni moja ya ujumbe mkuu wa Ashura. Ni kwa sababu hii ndiyo maana alipokuwa akibariziana na jeshi la batili katika medani ya Jihadi huko Karbala, mtukufu huyo alitamka kwa ushujaa: "Ikiwa dini ya Muhammad haisimami na kudumu ili kwa kuuliwa mimi, basi enyi panga nichukueni". Imam Hussein (as) anaashiria moja ya madhara ya kuachwa faradhi hiyo muhimu katika zama zake kwa kueleza kwamba: "Sasa inabidi Uislamu upigiwe fatiha kwa Waislamu kutawaliwa na watawala kama Yazid. Nilimsikia babu yangu Mtume wa Allah akisema: Ukhalifa ni haramu kwa ukoo wa Abu Sufyan; na kama iko siku mtakuja kumwona Muawiyah amepanda juu ya minbari basi muueni. Lakini watu wa Madina walimwona kwenye minbari ya Mtume hawakumuua na sasa Mwenyezi Mungu amewasalitishia Yazid fasiki". Kabla ya hapo, Imam Ali (as) pia alieleza katika wasia wake wa mwisho kuhusu umuhimu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya aliposema: "Msiache kuamrisha mema na kukataza mabaya kwani watakutawalieni waovu kisha kadiri mtavyoomba dua hamtajibiwa".
Japokuwa katika mapambano ya Ashura ni wanaume waliopigana vita na kuuawa shahidi, lakini wanawake, nao pia walitoa mchango mkubwa katika Siku ya Ashura yenyewe na baada ya tukio hilo pia. Tokea awali, Imam Hussein (as) aliandamana na wanawake katika safari yake ya kuelekea Makka na baadaye Karbala. Kuhusiana na hilo alisema: "Mwenyezi Mungu amepanga watu wa nyumba yangu pamoja na wanawake wawe nami muda wote". Katika tukio la Karbala pia wanawake walitoa mchango katika kuwapa moyo wanaume pamoja na kuhudumia majeruhi. Lakini mchango wao muhimu zaidi ulianzia pale, kama ilivyoonekana mbele ya macho, lilipomalizika tukio la maafa ya Ashura. Wanawake wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW walifichua kwa ushujaa ufisadi wa utawala wa Yazid kila pale walipoweza kufanya hivyo na kubainisha malengo ya mapambano ya Ashura. Kati ya wanawake hao, mchango wa Bibi Zainab (as) ndugu wa Imam Hussein (as) ulikuwa hauna mfano wake. Alipokuwa mbele ya hadhara ya watu wa mji wa Kufa, Bibi Zainab alitoa hotuba iliyowafanya watu hao wajute mno na kuona aibu kubwa mpaka wakakaribia kufanya uasi dhidi ya utawala, ambapo utawala huo wa kifasiki ulimzuia mtukufu huyo asiendelee kuwahutubia watu. Alipofikishwa kwenye kasri la Liwali wa Kufa Ubaidullah Ibn Ziyad, Bibi Zainab (as) alitolewa maneno ya vijembe na ya kutaka kumdunisha. Lakini mtukufu huyo alielezea kwa ufasaha mkubwa kuuawa shahidi Imam Hussein (as) na wafuasi wake kwa kusema: "Mimi sijaona lolote zaidi ya uzuri tu. Mashahidi wa Karbala walikuwa watu ambao Mwenyezi Mungu alikuwa amewachagulia kufa shahidi". Binti huyo wa Ali bin Abi Talib, alizungumza kwa ushujaa mkubwa pia katika kasri la Yazid, na katika sehemu moja ya hotuba yake alimuelekea mtawala huyo fasiki na kumwambia: "ewe Yazid fanya hila na vitimbi vyovyote vile utakavyo, lakini kadiri utavyofanya hila, hutoweza katu kuuondoa utajo wetu kwenye kumbukumbu na wala hutoweza kamwe kuufuta wahyi wetu". Katika harakati ya mapambano yake makubwa, ni namna hivyo wapenzi wasikilizaji Imam Hussein (as) aliutumia uwezo mkubwa wa wanawake wakubwa na mashujaa wa Nyumba yake kwa ajili ya tablighi na kuyatangaza mapambano yake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../