Arubaini; kukamilika Ashura
Arubaini ni siku ya kufikia ukamilifu. Ukamilifu wa Ashura ni Arubaini; ukamilifu wa matendo, harakati na juhudi zote. Karbala katika Siku ya Arubaini huwa ni kioo cha waliofikia kilele cha umaanawi kiasi kwamba ulegevu, uzembe, udhaifu na kurejea nyuma huwa havina nafasi tena katika hali hiyo.
Arubaini huwa ni siku ya msafara kurejea Karbala, msafara ambao kwa siku 40 zilizopita umepitia kipindi kigumu cha huzuni na simanzi. Msafara ambao badala ya kuwa kwenye kilele cha kushindwa, unarejea Karbala katika hali ya ushindi na kuwacha sumu ya kushindwa katika kizazi cha Bani Umayyia. Kwa ushindi huo, msafara wa Karbala ulikosoa na kubatilisha nguvu bandia ya maghasibu na kufunua pazia zao za uongo, hila na udanganyifu ili ukweli uweze kubainika wazi. Arubaini ni siku ya kubainika kashfa ya dhulma na kung'ara haki na ukweli.
Jioni ya Ashura na baada ya kuchomwa moto mahema ya wafuasi na familia ya Imam Hussein (as) ambaye ni mjukuu mpendwa wa Mtume Mtukufu (saw), watoto mayatima waliachwa wakihangaika jangwani huku waovu na makatili waliotekeleza mauaji hayo ya kutisha dhidi ya kizazi cha Mtume wakianza kusherehekea ushindi wao wa kidhahiri. Askari wa maadui walikuwa wakicheka kwa sauti za juu huku wakicheza densi. Baada ya kusherehekea kwa muda mrefu na kuchoka hatimaye waliingia kwenye mahema yao na kulala, huku wanawake wachache waliobakia na watoto wa kizazi cha Mtume wakilala nje kwenye baridi kali baada ya mahema yao kuteketezwa moto na maadui. Kesho yake habari za kuuawa kizazi cha Mtume (saw) zilifika katika mji wa Kufa ambako nako sherehe za ushindi bandia zilifanyika. Kwa vifijo, nderemo na vigelegele askari wapandafarasi walikuwa wakipiga makelele na kuimba nyimbo za kutaka kupewa zawadi ya dhahabu na fedha kutokana na kumuua mtukufu wa nyumba ya Mtume, wafuasi na familia yake.
Mateka wa vita au kwa ibara nzuri, familia ya Mtume Mtukufu (saw) walilazimishwa kwenda katika mji wa Kufa katika hali mbaya na ya kusikitisha kabisa. Nguo zao zilikuwa zimeraruka, kutokuwa na mavazi yanayofaa na kupandishwa ngamia ambao hawakufaa kabisa. Walikata masafa ya kilomita 70 hadi 80 kutoka Karbala hadi Kufa kwa tabu na machungu makubwa. Walikuwa wakichapwa mijeledi, kutusiwa na kuudhiwa wakiwa katika hali hiyo. Walitawanya vichwa vya mashaidi wa Karbala kati yao ili wapate kuwatesa zaidi. Kila kitu kilikuwa kimetayarishwa kwa ajili ya kufanyika karamu na sherehe kubwa ya ushindi ambapo ghafla sherehe hiyo ilikatizwa kwa hutuba ya Bibi Zainab (sa). Hakika hutuba hiyo ilizamisha kabisa utukufu na ujabari wa kidhahiri wa Bani Ummayyia mjini Kufa. Zainab (as) hakupangiwa kuzungumza kwenye sherehe hiyo lakini ghafla alitoa hutuba ya kishindo iliyowashangaza wengi. Alizungumza kwa maneno makali na mazito kiasi kwamba hakuna mtu yoyote aliyethubutu kumzuia kuzungumza. Alisimama imara kadiri kwamba wote walikaa kimya huku wakiwa wameshangaa. Hali hiyo ilikatiza ghfla sherehe ya Kufa na ikaamuliwa mateka wote waharakishwe kupelekwa Sham.
Hali ya kuwasili kwao Sham ilikuwa tofauti kabisa na ile ya kuingia kwao Kufa. Hata kama Amir al-mu'mineen Ali (as) alitawala siku moja katika mji wa Kufa, lakini hali ilikuwa tofauti kabisa huko Sham ambako watawala wa Bani Ummayyia walitawala kwa miaka mingi na watu kutokuwa na ufahamu wowote wa Ahlul Beit (as). Kwa miaka mingi propaganda chafu zilikuwa zimeenezwa dhidi ya Imam Ali (as) na Riwaya za Mtume (saw) kupotoshwa. Wakazi wa Sham (syria) walikuwa wakimuita Muawiyya kuwa ni 'Mjomba wa Waumini'. Mateka walipokaribia kuingia katika mji wa Damascus, Licha ya Bibi Zainab na Imam Sajjad (as) kuomba mara kadhaa waingizwe mjini kupitia lango lenye watu wachache zaidi lakini waovu hao waliowakamata mateka walipuuza maombi yao hayo na kuwaingiza mjini hapo kupitia lango lililokuwa na watu wengi zaidi, ili kuwadhalilisha mashahidi kwa kuwezesha vichwa vyao vionekane na wakazi wengi zaidi. Katika mji huo, Yazid alikuwa amejitengenezea kasri kubwa la starehe na anasa zake zilizo nje kabisa ya mafundisho ya Kiislamu. Aliketi kwenye paa la kasri hilo na kujitazamia jinsi vichwa vya mashahidi vilivyokuwa vikivunjiwa heshima. Alipoona vichwa hivyo vinavunjiwa heshima vikiwa vimetundikwa juu ya mikuki alianza kuimba mashairi ambayo yalibainisha furaha yake kubwa kutokana na kile alichokitaja kuwa ulipizaji kisasi dhidi ya kizazi cha Mtukufu Mtume (saw). Katika kipindi kifupi hali ya mambo ilibadilika ghafla. Yazid aliyekuwa amelewa kupindukia, na huku akiwa na majivuno mengi alianza kuyagongagonga meno ya Imam Hussein (as) huku akimwambia kwa kejeli Bibi Zainab (sa): 'Hakika ndugu yako alikuwa na meno meupe'! Ghafla Bibi Zainab alianza kutoa hotuba na hivyo kuvuruga mahesabu yote ya Yazid. Baada ya hotuba hiyo malalamiko yalianza kusikika. Mkristo mmoja aliyekuwa miongoni mwa hadhirina alisimama na kusema kwa mshangao: 'Je, mnasherehekea kuuawa kwa mtoto wa Mtume wenu?! Katika nchi yangu iliyoko kweye kisiwa cha mbali kwenye bahari, kuna kanisa moja ambalo watu hulizuru kwa uchache mara moja kwa mwaka. Ndani yake mna chombo cha dhahabu ambacho kimening'inizwa juu ya paa la mihrabu ya kanisa hilo na humo kuna kucha ambalo linaaminika kuwa ni la kwato la punda aliyekuwa akipandwa na Isa Masih. Kwa msigi huo watu huwa wanalizuru kucha hilo kutokana na heshima waliyonayo kwa Isa Masih, ili hali nyinyi hapa mnamuua mtoto wa Mtume wenu mara tu baada ya kuaga dunia Mtume huyo?!'
Malalamiko hayo yalikuwa mazito mno kwa Yazid, ambaye aliamuru Mkristo huyo akamatwe na kuuawa mara moja. Mzee mwingine pia ambaye alikuwa mjumbe wa Mfalme wa Roma alisimama kwenye hadhara hiyo na kumlalamikia Yazid kwa maneno makali huku akiwa na hasira kubwa. Yazid pia aliamuru auawe. Kwa msingi huo mazingira ya Sham yalibadilika mara moja. Yazid alipoona kuwa ameshindwa kukabiliana na hali hiyo ya malalamiko yaliyokuwa yakiongezeka, aliamuru juzuu za Qur'ani zitawanywe miongoni mwa watu waliokuwa hapo ili washughulishwe na kusoma Qur'ani na kutozungumzia tena mauaji ya kutisha ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Ili kutuliza hali ya mambo na kujaribu kuonyesha sura bandia ya huruma aliamuru nyumba moja itengwe kwa ajili ya Ahlul Beit wa Mtume (as) wapate kuombolezea humo kuuawa kwa mjukuu huyo wa Mtume na wafuasi wake. Watu walikuwa wakiingia nyumbani humo kwa makundi makundi huku wakisikiliza hotuba ya kuhuzunisha na kusikitisha ya Bibi Zainab (sa) kuhusiana na jinsi watu wa Nyumba ya Mtume walivyouawa kinyama na maadui wa Uislamu, jambo ambalo mwishowe lilikuwa na madhara kwa Yazid na kizazi cha Bani Ummayyia. Hivyo alijaribu kujiweka mbali na mauaji ya Imam Hussein (as) kwa kusema: 'Mimi sikuridhia mauaji ya Hussein, hatukuwa na hitilafu zozote!'
Tunapasa kuzingatia nukta hii hapa kwamba tokea mwanzoni, kizazi cha Bani Ummayyia kilifanya juhudi kubwa kubadilisha hali ya mambo kwa manufaa yao na kwa madhara ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) na wakati huohuo kuhalalisha kila hatua ya uadui waliyoichukua dhidi ya watukufu hao. Kwa kadiri kwamba mwaka wa 61 Hijiria wakati ambapo watu walikusanyika katika jangwa la Karbala kwa ajili ya kumuua Imam Hussein (as) walikuwa wakidhani kwamba wangeingia Peponi moja kwa moja kwa mauaji hayo. Kuhusiana na suala hilo mwanahistoria mashuhuri, Yaa'qubi anaandika: 'Tokea tarehe saba Muharram, kila siku karibu watu 20,000 walikuwa wakioga katika Mto Furati ili wapate kumuuua Imam Hussein (as) kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kupata ridhaa Zake. Tokea wakati wa Mtume hadi wakati wa kuuawa shahidi Imam Hussein (as), Bani Ummayyia walifanya njama kubwa kwa kipindi cha miaka 51 kwa ajili ya kumshinda Imam Ali (as) na Ahlul Beit kwa ujumla na walibuni Riwaya na Hadithi nyingi za uongo ili kufikia lengo hilo. Miongoni mwa Riwaya hizo ni kuwa walikuwa wakisema: 'Wakati Malaika Jibril alipokuwa akimteremkia Mtume alikuwa akimwambia, mfikishie Muawiyya salamu za Mwenyezi Mungu.'
Tunapasa kufahamu kwamba kadiri walivyokuwa wakibuni Hadithi za uongo kwa lengo la kuimarisha nafasi yao pia walikuwa wakibuni Hadithi kwa ajili ya kukivunjia heshima na utukufu kizazi cha Mtume (saw). Kwa kadiri kwamba wakati Imam Ali ambaye kwa mujibu wa Aya ya 61 ya Surat Aal Imran alikuwa mfano wa moyo wa Mtume (saw), alipouawa shahidi katika Msikiti wa Kufa, watu wengi walishangaa na kujiuliza, je, kwani Ali alikuwa akifanya nini msikitini?! Lakini Ashura na kuuawa shahidi kwa njia ya kinyama Imam Hussein bin Ali (as) kulibadilisha kabisa hali hiyo potovu ya kisiasa. Katika Siku ya Arubaini msafara wa mateka uliwasili kwa kishindo na ushindi huko Karbala na hivyo kushinda na kukidhalilisha kizazi cha Bani Ummayyia.
Msafara huo uliwasili sehemu hiyo baada ya kupata mateso, udhalilishwaji, machungu, matusi, majeraha, dharau na vitisho kwa muda wa siku Arubaini. Msafara huo uliingia mjini hapo kwa ushindi mkubwa tofauti kabisa na jinsi ulivyoondoka sehemu hiyo Siku ya Ashura. Msafara huo ulirejea Karbala ili kujadidisha agano na uaminifu wao kwa mashahidi waliouawa kidhulma na maadui na wakati huohuo kuwatangazia walimwengu ujumbe wa Mtume Mtukufu (saw).
Ni kutokana na jambo hilo ndipo Siku ya Arubaini inapokamilika na kupata maana yake halisi. Arubaini katika Qur'ani Tukufu pia ina maana ya kukamilika jambo. Mwenyezi Mungu anachukulia mwanadamu kutimu miaka 40 kuwa kipindi cha kilelel cha kubaleghe kwake kiakili. Anasema katika aya ya 15 ya Surat al-Ahqaaf: Hata anapofika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda.
Na vilevile anasema katika aya ya 142 ya Surat al-A'raaf kuhusiana na ahadi yake kwa Nabii Musa: Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Inafahamika wazi kuwa siku 40 ni siku ya kufikia ukamilifu. Ukamilifu wa Ashura ni Arubaini. Ukamilifu wa mambo yote yaliyotoweka ni ukamilifu wa juhudi na jitihada zote.
Katika siku ya Ashura Mwenyezi Mungu alimpa Imam Hussein (as) urithi wa Mitume wote, katika Siku ya Arubaini urithi huo ulikabidhiwa historia. Ashura ni maonyesho ya utoaji wa Mwenyezi Mungu kwa Imam Hussein (as) na Arubaini ni maonyesho ya utoaji wa Imam Hussein kwa mwanadamu na historia.
Ni kwa msingi huo ndipo tunasoma katika Ziara ya Arubaini kwamba Mwenyezi Mungu alimpa shahada Imam Hussein (as) ili kwa damu yake aweze kuwaokoa wanadamu kutokana na ujahili na kutokuwa na uelewa na pia kuwaokoa kutokana na upotovu.
Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.