Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini na Msingi wa Utawala wa Faqihi
Alfajiri ya tarehe 12 Bahman 1357 Hijria Shamsia (11 Februari 1979) ilikuwa siku ya matarajio makubwa na kusibiri kwa hamu kulikoandamana na wasiwasi na hofu kubwa.
Baada ya kipindi cha miaka isiyopungua 14 wananchi wa Iran walikuwa wakisubiri kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini akitokea uhamishoni huko Ufaransa. Hata hivyo ukatili na jinai za utawala wa kidikteta wa Shah ambao ulikua umetishia kuitungua ndege itakayombeba Imam Khomeini kutoka Paris uliwatia wasiwasi mkubwa wananchi Waislamu wa Iran. Pamoja na hayo kutokana na kuogopa hasira za wananchi, utawala wa kidikteta wa Shah haukuwa na ujasiri wa kutekeleza vitisho hivyo na ndege iliyokuwa imembeba Imam ilitua salama na kupokewa kwa shangwe kubwa na mamilioni ya Wairani. Tukio hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya Iran na ulikuwa mwanzo wa kuanguka kikamilifu utawala tegemezi wa Shah katika kipindi cha chini ya wiki mbili.
Kurejea nchini Imam Khomeini kuliambatana na thamani aali za kibinadamu na Kiislamu ambazo wananchi Waislamu wa Iran walisabilia kila walichokuwa nacho kwa ajili ya kuhakikisha kwamba zinatekelezwa hapa nchini kama vile uadilifu, uhuru, kujitawala, kupambana na dhulma na kadhalika. Hata hivyo tunaweza kusema kuwa, hadiya kubwa zaidi ya Imam Khomeini kwa taifa la Iran na Umma wa Kiislamu kwa ujumla ni kubuni utawala wa Kiislamu kwa kutegemea nadharia ya "utawala wa faqihi". Mjadala kuhusu nadharia ya utawala wa Kiislamu, kiongozi wake na sifa zake umekuwepo kwa karne kadhaa zilizopita kati ya wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu wa madhehebu zote mbili za Shia na Suni. Hata hivyo ubunifu na kazi kubwa iliyofanywa na hayati Imam Khomeini katika uwanja huo ni kuweka misingi ya kielimu na ushahidi wa kimaandishi na kimantiki wa nadharia hiyo. Imam hakutosheka na kuweka nadharia hiyo katika maandishi na kuithibitisha kwa hoja za kidini na kimantiki bali pia aliitekeleza kivitendo. Miaka mingi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini aliandika kitabu cha "Utawala wa Fahihi" akieleza nadharia hiyo.
Utawala wa Fahiqi kwa lugha nyepesi zaidi una maana ya mwanazuoni, msomi na mtaalamu wa Uislamu aliyekamisha masharti ya uongozi kusimamia na kuendesha masuala ya jamii. Huyu ndiye anayeitwa faqihi mtawala. "Waliyu Faqiih" au Faqihi Mtawala kwa hakika ni naibu na kaimu wa Imam wa Zama (as) katika zama za ghaiba. Imam Khomeini alitumia hadithi nyingi zilizopokewa katika uwanja huu kuithibitisha nadharia ya utawala wa faqihi.
Zimepokewa hadithi nyingi sana kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti wake katika uwanja huu. Mtume Muhammad (saw) amewatambua maulamaa na wanazuoni wema waliokamilisha masharti kuwa ni makhalifa wake na warithi wa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Vilevile khalifa na wasii wake, yaani Imam Ali bin Abi Twalib amewataja maulamaa kuwa ni viongozi wa watu. Anasema: "Kwa mujibu wa hukumu ya Mwenyezi Mungu na Uislamu, ni wajibu kwa Umma baada ya kufariki dunia kiongozi wake, usifanye lolote ila baada ya kumchagua kiongozi mchamungu, anayejua sheria na Suna za Mtume ili akusanye mali za umma, asimamishe ibada ya Hija na Swala za Ijumaa…". Kwa msingi huo suala la kuchagua kiongozi anayefaa na mstahiki kwa ajili ya jamii ya Kiislamu linapaswa kutangulia mbele ya jambo lolote jingine. Hadithi mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Imam wa Zama, Mahdi (AF) inawataja wanazuoni wa sheria (fiqhi) za Kiislamu kuwa ndio manaibu wa mtukufu huyo katika kusimamia na kuongoza masuala ya Umma wa Kiislamu. Anasema: "Katika matukio mbalimbali rejeeni kwa wapokezi wa hadithi zetu, wao ndio hoja yangu kwenu na mimi ni hoja ya Mwenyezi Mungu."
Kwa mujibu wa hadithi hii tukufu ni kwamba, Waislamu wanalazimika kurejea na kuwafuata wataalamu wa hadithi na maarifa ya Kiislamu katika masuala mbalimbali yanayotokea hapa duniani.
Kumetolewa hoja nyingi za kuthibitisha udharura wa kuwepo faqihi mtawala ambazo zimeelezwa na hayati Imam Khomeini katika vitabu na maandishi yake mengi. Miongoni mwa hoja hizo ni kwamba, katika jamii ambayo watu wake wengi ni Waislamu wanaoamini thamani na maadili ya Kiislamu, ni jambo la kawaida kwamba waongozwe na serikali au utawala wa Kiislamu, kwa sababu maisha ya kijamii na ukamilifu wa mtu binafsi na jamii katika jamii kama hiyo vimo katika utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu zinazooana na imani na itikadi yao. Kwa msingi huo kiongozi wa serikali na utawala kama huo anapaswa kuwa mtu mwenye ujuzi na utaalamu wa elimu na maarifa ya Kiislamu, mwadilifu na mchamungu. Huyu ndiye anayeitwa "Waliyul Faqiih" au faqihi mtawala. Katika kitabu chake cha Tahrirul Wasilah, Imam Khomeini ameandika kwamba: "Katika kipindi cha ghaibu na kutokuwepo Imam wa Zama (af), manaibu wake ambao ni wataalamu wa sheria za Kiislamu yaani wasomi wa fiqhi waliokamilisha masharti ya kutoa fatwa na kuhukumu baina ya watu, ndio wanaoshika nafasi yake katika utekelezaji wa masuala ya kisiasa na kiserikali na mambo mengine yote yanayofanywa na Imam (as)."
Katika kitabu chake cha Utawala wa Faqihi, hayati Imam Ruhullah Khomeini pia ametoa hoja nyingine inayokaribia na hiyo iliyotangulia kuthibitisha udharura wa kuwepo utawala wa Kiislamu na faqihi mtawala. Anasema, mbali na masuala ya kiibada na ya mtu binafsi, dini ya Uislamu pia ina masuala ya kijamii na kisiasa yanayowajibisha kuwepo serikali na mtawala mwenye ujuzi na utaalamu wa sheria za Kiislamu. Ameandika katika kitabu hicho kwamba: "Kila mtu anayetazama kiujumla sheria za Kiislamu anatambua kuwa, mbali na kuwa ibada ni wadhifa wa mwanadamu mbele ya Muumba wake, katika ibada hizo pia kuna masuala ya kisiasa na kijamii yanayohusiana na mambo ya kidunia. … Vilevile kuna masuala mengi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayoonesha kwamba Uislamu si ibada pekee bali dini ya Uislamu ililetwa kwa ajili ya kuasisi serikali ya kiadilifu yenye sheria na kanuni za kiuchumi, sheria za mahakama na kadhalika…" Imam Khomeini pia anaashiria udharura wa kueneza uadilifu, elimu na malezi, kulindwa mipaka, kukusanya ushuru na kodi, kutoa maamuzi na hukumu, kulindwa nidhamu na kanuni, kuamrisha mema na kukataza maovu na kadhalika na kufikia natija kwamba: "Kuendelea kuwepo masuala haya kunaleta udharura wa kuwepo serikali na utawala ambayo mtawala wake atachunga sheria za Mwenyezi Mungu na kutoa dhamana ya utekelezaji wake." Hapana shaka kuwa, mtawala wa serikali na utawala kama huo si mwingine isipokuwa faqihi, mwanazuoni na mtaalamu wa sheria za Kiislamu anayesifika kwa kuwa na taqwa, uchambungu na uadilifu.
Katika sehemu nyingine ya kitabu cha Utawala wa Faqihi, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu anathibitisha utawala wa faqihi kwa kusema: "Sisi tunaamini wilaya na utawala wa Kiislamu na tunaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) anapaswa kuainisha khalifa na kiongozi wa baada yake na alimuainisha kiongozi huyo… Jambo linalolazimisha kuainisha khalifa ni utawala na serikali. Tunataka kuwepo khalifa na mtawala ili atekeleze sheria. Sheria zinahitaji mtekelezaji wake. Hivi ndivyo ilivyo katika nchi zote duniani na kutunga sheria pekee hakuna faida yoyote na hakuwezi kudhamini saada na ufanisi wa mwandamu. Hivyo basi baada ya kutungwa sheria kuna ulazima wa kuwepo mtekelezaji wake."
Kwa msingi huu sheria na mafundisho ya Qur'ani na Hadithi hususan masuala ya kisiasa na kijamii hayawezi kuwa na faida kwa Waislamu isipokuwa pale yatakapotekelezwa na mtawala mwenye ujuzi, mwadilifu na mchamungu ambaye atadhamini saada na ufanisi wa watu wa jamii husika. Kisha Imam Khomeini anasema: Kama ambavyo Mtume Muhammad (saw) ameamrishwa kutekeleza sheria na kuweka nidhamu na kanuni za Uislamu, vilevile Mwenyezi Mungu SW amemfanya rais na mtawala wa Waislamu ni akawajibisha kumtii. Wanazuoni waadilifu pia wanapaswa kuwa viongozi na watawala, kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni na kuweka mfumo wa kijamii."
Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, kila mwanazuoni na mtaalamu wa fiqhi hawezi kuwa kiongozi wa jamii na Umma wa Kiislamu. Imam J"afaru Swadiq (as) anasema katika hadithi yake mashuhuri kwamba: "Watu wanalazimika kumfuata faqihi mchamungu, anayelinda dini, anayekwenda kinyume na hawaa na matakwa yake ya kinafsi na anayetii amri za Mwenyezi Mungu." Imam Khomeini anaeleza baadhi ya sifa za faqihi mtawala akisema: "Mtu anayetaka kuwa mtawala wa Waislamu na naibu wa Amirul Muuminina (as) anapaswa kuwa msafi asiyetafuta dunia kwa udi na uvumba japokuwa ni halali. Kwa sababu wakati huo hatakuwa mtunzaji wa amana ya Mwenyezi Mungu na hawezi kuaminiwa." Sharti jingine linalotajwa na hayati Imam Khomeini kwa ajili ya faqihi mtawala ni ujuzi na uwezo wa kusimamia masuala ya nchi. Kifungu cha tano cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinasisitiza kuwa: "Katika zama za ghaiba ya Imam wa Zama, kiongozi wa Umma katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anapaswa kuwa faqihi mwadilifu, mchamungu, mtambuzi wa masuala ya zama zake, shujaa, mudiri na mweledi…"
Nukta muhimu inayopasa kuashiria hapa kuhusu faqihi mtawala ni kuwa, pale anapokosa moja kati ya masharti na sifa za uongozi kama uadilifu, ushujaa, takwa na uchamungu, hupoteza nafasi na cheo hicho papo na hapo na hii ni miongoni mwa tofauti muhimu za mtawala katika mfumo wa Kiislamu na katika mifumo mingine ya utawala na uongozi sawa iwe ya kidikteta au kidemokrasia. Kuhusu suala hilo Imam Khomeini anasisitiza kuwa: "Faqihi mtawala mwenye sifa hawezi kufanya kinyume, na kama atasema neno moja tu la uongo au kwenda kinyume hatua moja atakuwa amepoteza uongozi wake…"
Hapa inaeleweka kwamba, utawala wa faqihi ni msingi imara na aali ambao sheria za Uislamu zimeainisha mipaka, sifa na masharti yake.