Ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mwanadamu wa Leo
(last modified Fri, 09 Feb 2018 05:46:16 GMT )
Feb 09, 2018 05:46 UTC
  • Ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mwanadamu wa Leo

Licha ya kupita miaka 39 sasa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran lakini mapinduzi hayo na taathira zake kikanda na kimataifa yangali yanajadiliwa hadi sasa katika duru mbalimbali za kisiasa, vyuo vikuu na vyombo vya habari kote duniani.

Historia ya baada ya mwezi Bahman 1357 Hijria Shamsia yaani tarehe 11 Februari mwaka 1979, imejaa matukio mengi yanayoonesha mabadiliko na mageuzi makubwa yaliyotokea hapa nchini na ilhamu na ujumbe mpya wa mapinduzi hayo kwa mwanadamu wa leo. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979 hayakutoa changamoto kwa siasa za kibeberu za Marekani na madola mengine ya kibeberu tu bali kutokea na kuendelea kuwepo kwake kwa karibu miongo minne sasa kumeandamana na thamani na mafundisho kwa ajili ya mwanadamu wa sasa ambayo mvuto wake unaongezeka siku baada ya siku. 

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanatofautiana na mapinduzi mengine katika kutokea kwake, aina ya mapambano na katika malengo yake. Suala hilo limeyafanya yatofautiane na mapinduzi mengine yaliyotokea duniani katika ujumbe, matokeo na mafanikio yake. Kama ilivyo zilzala au volkano, kila mapinduzi huwa na taathira za kiwango fulani kikanda na kimataifa na vilevile huwa na ujumbe unaowakilisha stratijia yake. Vilevile kadiri mapinduzi yanavyokuwa na mvuto mkubwa ndivyo ambavyo huvutia idadi kubwa zaidi ya wanadamu, kuungwa mkono na kuwa kigezo cha kuigwa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo sifa yake kuu ni kutegemea mwenendo na fikra safi za Mitume wa Mwenyezi Mungu hususan Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na hamasa kubwa kama ile ya siku ya Ashura, yalitokea katika kipindi ambacho fikra za kiliberali na kisoshalisti zilikuwa zimeanza kupoteza mvuto wake na kuleta na ujumbe wa heshima, uhuru na utukufu wa mwanadamu. Katika kipindi hicho ambapo wanafikra na wasomi wengi wa mrengo wa kushoto walikuwa wakidai kwamba, Umaksi (Marxism) ndiyo fikra na aidiolojia pekee inayoweza kukusanya pamoja mataifa mbalimbali na kuleta vuguvugu na harakati, Mapinduzi ya Kiislamu ya watu wa Iran yaliwaletea walimwengu ujumbe unaosisitiza kuwa, Uislamu ndio mfumo ambao mbali na kuwa na uwezo wa kuratibu mapambano dhidi ya dhulma na uonevu, vilevile unaweza kutatua matatizo ya jamii ya mwanadamu katika zama tata za sasa na kuongoza jamii kwa njia bora zaidi. 

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyofanyika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, masuala ya kiroho, maadili na kuhuisha utamaduni na utambulisho wa kidini, yalitegemea itikadi za Kiislamu na yakapata ilhamu kutoka kwenye mafundisho ya dini hiyo. Mapinduzi hayo yalitegemea imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja na utawala wake mutlaki, ulazima wa kusalimu amri kwake Yeye, imani ya wahyi na ufunuo wa Mwenyezi Mungu SW na mchango wake mkuu katika sheria na kanuni za utawala. Mapinduzi hayo yalitokea katika eneo ambalo kwa miaka mingi limekuwa medani ya michezo michafu ya madola ya kikoloni na baadaye tawala za kifalme na za kurithishana utawala, suala ambalo lilivuruga kabisa mahesabu ya madola ya kinyonyaji. Kwa sababu hiyo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitoa ilhamu na somo kubwa kwa harakati za kupigania uhuru na haki na wapenda demokrasia na kujitawala kote duniani.

Sifa ya kupambana na dhulma ni miongoni mwa ujumbe muhimu za Mapinduzi ya Kiislamu kwa mwanadamu wa sasa. Katika uga wa eneo la Mashariki ya Kati, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikutambua kuundwa dola haramu na bandia la Israel kuwa msingi mkuu wa dhulma, jinai na ukatili na kuanzisha harakati ya kutetea haki zilizoghusubiwa za Palestina. Sura ya kimataifa ya ujumbe huo muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilidhihiri katika mapambano yake dhidi ya ubeberu wa kimataifa na mabeberu wa Mashariki na Magharibi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Mapinduzi hayo na matunda yake makubwa yaani Jamhuri ya Kiislamu, sambamba na kufanya jitihada za kutokomeza dhulma na kuzisaidia harakati za kupigania haki na uadilifu kote duniani, yakawa na uhusiano na ushirikiano mzuri na mataifa mbalimbali. 

Umoja wa Kiislamu na kuishi kwa amani na wafuasi wa dini nyingine ni miongoni mwa ujumbe muhimu za Mapinduzi ya Kiislamu. Tangu hapo mwanzoni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweka mbele kaulimbiu ya kuwepo umoja na mshikamano baina ya Waislamu wa madhehebu zote na kutilia mkazo udharura wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi na mataifa ya Waislamu. Vilevile Jamhuri ya Kiislamu na kwa kutegemea misingi yake mikuu mitatu ya siasa za kigeni, yaani heshima, hekima na maslahi, ilitilia mkazo suala la kuwa na ujirani mwena na nchi zote jirani.

Pamoja na hayo yote tunaweza kusema kuwa, ujumbe muhimu zaidi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa mwanadamu wa leo ambao hata wachambuzi wanakiri kuwa ndio mkubwa na muhimu zaidi wa mapinduzi hayo, ni kurejesha masuala ya kiroho katika dunia iliyokuwa imezama katika umaada na kuingiza tena dini na mafundisho yake katika masuala ya kisiasa na kijamii. Ujumbe huu si kwa jamii za Kiislamu pekee bali kwa kiumbe mwanadamu aliyepoteza mwelekeo na kuzama katika ustaarabu wa kimaada. Mapinduzi ya Kiislamu yalikuja na ujumbe unaowataka watu wa dini, fikra na aidiolojia tofauti kuzingatia tena mafundisho ya dini, maadili na masuala ya kiroho kwa ajili ya kuondoka katika mkwamo wa dunia ya kimaada. Matatizo ya kimaadili, visa vingi vya kujinyonga na maradhi ya kiakili na kinafsi yanaendele kushuhudiwa katika nchi na jamii nyingi za kimaada. Mwanadamu katika jamii hizo amekuwa mpweke na mwenye mashaka mwengi ya kinafsi licha ya kuwa na nyenzo karibu zote za maisha bora ya kimaada. Wimbi la watu kujielekeza katika hurafa na dini bandia linashika kasi katika dunia ya sasa na hapana shaka kuwa, suala hilo ni ishara ya haja ya mwanadamu kwa masuala ya kiroho na ujumbe wa ufunuo na Wahyi. Mwelekeo huu wa dunia ya sasa hususan huko Magharibi kwa dini bandia na hurafa utamtumbukiza mwanadamu huyo katika mkwamo mpya, na Uislamu pekee ndio unaoweza kujaza ombwe huo wa kiroho. Hii ndiyo tafsiri ya kuenea kwa kasi Uislamu duniani hususan katika nchi za Magharibi kama zinavyoonesha takwimu za taasisi mablimbali za kimataifa.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni jitihada za kurejesha masuala ya kiroho katika dunia ya kimaada

Uislamu ni dini inayoundwa na itikadi, ibada na sheria za masuala ya mtu binafsi na jamii. Mafundisho ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu yanasisitiza kuwa, njia ya kuelekea Akhera na kwenye ufanisi wa milele ni mwenendo, matendo na utekelezaji wa majukumu yetu hapa duniani. Kwa sababu hiyo mafundisho ya kimaadili, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kadhalika ya Uislamu yana programu na ratiba kamili inayokidhi mahitaji yote ya mwanadamu kwa njia sahihi na ya kimantiki. Lisa Lathe ambaye ni Mtaalamu wa Masuala ya Mashariki (Orientalist) wa Chuo kikuu cha Vienna nchini Austria anaitaja sifa hiyo ya Uislamu kuwa ndiyo sababu kuu inayowavutia zaidi wanadamu katika dini hiyo na kusema: "Ongezeko la wafuasi wa Uislamu kote duniani linatokana la ukamilifu na sifa yake ya kupigania uadilifu."

Ili kuweza kukabiliana na taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuzuia ujumbe wake kufika kwa harakati za kupigania uhuru, haki na uadilifu, madola ya kibeberu yalianzisha wimbi la kuchafua sura ya Uislamu na kuwatisha watu na Uislamu baada tu ya ushindi wa mapinduzi hayo hapa nchini.

Harakati hiyo ilifanyika kwa lengo la kuwazuia wanadamu kupata ujumbe safi wa Uislamu halisi. Hata hivyo njama hizo za kuchafua sura safi ya Uislamu na hujuma ya kipropaganda dhidi ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ziliwafanya watu wengi waanze kudadisi na kutaka kujua hakika na kweli kuhusu Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na hatimaye kukubali hakika na kweli. Hii ndiyo maana ya kupeleka nje Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo yanatoa ujumbe kwamba, dini inaweza kusimamia masuala yote ya kisiasa, kijamii na kadhalika ya kila siku ya mwanadamu na kupambana na aina zote za dhulma, uonevu na ukosefu wa usawa. Suala hili halina maana ya kuingilia masuala ya watu wa nchi nyingine bali lina maana ya kujibu na kukidhi mahitaji na kutoa majibu kwa maswali mengi ya kifkra ya mwanadamu mwenye kiu ya kupata maarifa ya mbinguni.                 

Tags