Sababu za kubakia na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
(last modified Sat, 10 Feb 2018 10:55:47 GMT )
Feb 10, 2018 10:55 UTC
  • Sababu za kubakia na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 39 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea mwaka 1979 kwa uongozi wenye busara wa Imam Ruhullah Khomeini; mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala dhalimu na kibarala wa mfalme Shah. 11/02/2018

 

Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Tumo katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, mapinduzi ambayo licha ya njama na mipango michafu ya maadui zake yamebakia na kudumu hadi leo na kuendelea mbele yakiwa imara na madhubuti kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Hivi sasa Mapinduzi haya yanaingia katika mwaka wake wa 40 yaani miongo minne, huku nguzo za mapinduzi haya zikijikita na kuwa imara zaidi na kupiga hatua katika njia za kivitendo kwa ajili ya kufikia malengo na matukufu yake.

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, wananchi wa Iran wakiwa na azma na irada ya kupigiwa mfano walichukua uamuzi wa kuusambaratisha na kuupindua utawala kibaraka wa Kipahlavi na wakafungua ukurasa mpya wa historia ya nchi hii. Mapinduzi haya yalianza kwa msingi wa matukufu makubwa ya kibinadamu, kiutu na Kiislamu na yakapata ushindi kwa msuko wa Mwenyezi Mungu na umoja wa kalima na hadi hivi sasa yameweza kusonga mbele na kuvuka vizingiti, vitisho na njama tata na za kila namna za maadui.

Kukataa dhulma, kupinga udikteta na ubeberu, kutaka kuweko utawala wenye misingi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kuwa na jamii huru na yenye kujitawala kupitia Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni mambo ambayo maadui wa ndani na nje hawakuweza kuyastahamili hata kidogo. Ni kwa muktadha huo, ndio maana maadui hawa wakakusanya nguvu na kuanza kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu wakiwa na chuki na adawa na mfumo huu unaotawala hapa nchini.

Hata hivyo pamoja na njama na hatua za ukwamishaji mambo za maadui, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiongozwa na Imam Khomeini MA katika muongo wa kwanza na baadaye kwa uongozi wa Ayatullah Ali Khamenei, katika muongo wa pili na wa tatu yamefanikiwa kupitia na kuvuka tufani na mawimbi makubwa na kwa kusimama kidete kulikoleta ushindi mkabala na mashinikizo na mibinyo, leo hii mapinduzi haya yanang'ara kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Faili na utendaji wa miaka 39 ya umri wa Mapinduzi ya Kiislamu linaonyesha na kuweka bayana vigezo vya nguvu na maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo daima imekuwa katika hali ya kukwea na kupiga hatua na hivyo kuashiria mustakabali mwema na wenye matumaini.

Crane Brinton mwananadharia wa mapinduzi ameichambua na kuijadili nukta hii katika kitabu chake cha "The autopsy of the Four Revolutions" kwamba, mapinduzi mbalimbali kuna siku yanazaliwa na kuna siku yanakufa.

Crane Brinton anaamini kwamba, katika mapinduzi yote manne ya Ufaransa, Uingereza, Marekani na Russia tunaweza kushuhudia nukta hii ya pamoja.

Kwa mtazamo wake ni kuwa, katika kila mapinduzi, baada ya kupatikana ushindi wa wanamapinduzi, huanza kipindi cha matumaini, shangwe na furaha ambacho hutofautiana na kipindi cha kabla ya mapinduzi hayo. Crane anakitaja kipindi hicho kama ni honeymoon au kipindi cha fungate yaani kipindi cha maelewano mazuri mwanzoni mwa shughuli fulani. Yaani kipindi ambacho utawala uliopita umesambaratishwa na mfumo mpya kuchukua nafasi yake. Hata hivyo kipindi cha fungate kawaida humalizika haraka na kwa kuingia madarakani utawala wenye misimamo ya wastani au wenye misimamo mikali na kuibuka mivutano na migongano ndani ya mapinduzi, kifo cha mapinduzi hayo huandaliwa. Kwa mtazamo huo, kimsingi mapinduzi huwa ni "Homa Kali ya Jamii" yaani huwa ni tukio lisilo la kawaida. Ndio maana kuna haja ya kurejea kwa haraka katika hali na mazingira ya kawaida.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Filihali, kuna watu wengi wanaotaka kufahamu je hatima na majaaliwa haya yameyakumba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran? Na kama sivyo, je sababu hasa ya kubakia mapinduzi haya ni nini?

Hapana shaka kuwa, mapinduzi manne muhimu yaliyotokea duniani kila moja kati ya mapinduzi hayo yalileta mabadiliko na mageuzi katika jamii yake na kuwa na taathira pia. Hata hivyo akthari ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran iwe ni kwa upande wa kudumu na kubakia kwake au katika uwanja wa taathira yake, yalikuwa ni mapinduzi nadra na ya kipekee na siku baada ya siku wigo wa taathira yake umezidi kupanuka na kuongezeka. Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran imekuwa kubwa kiasi kwamba, imevuka mipaka ya nchi hii na kuwa kama upepo mwanana wenye kuleta uhai katika kila kona ya dunia na kuingia katika nyoyo za wenye kiu ya haki na uadilifu.

Fauka ya hayo, mapinduzi haya yameandaa uwanja wa kutokea mwamko na kuundwa harakati za wananchi za kupigania haki na uadilifu. Imam Khomeini MA kutokana na kuzingatia nukta hii muhimu ameandika katika wasia wake:

Haipasi kutilia shaka kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanatofautiana na mapinduzi mengine yote; iwe ni katika kujitokeza kwake, namna mapambano yake yalivyoendeshwa na hata katika msukumo na harakati ya mapinduzi haya.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaamini kuwa, sababu kuu ya kubakia Mapinduzi ya Kiislamu ni neno la haki yaliyonayo mapinduzi haya. Anaongeza kuwa: Neno la mapinduzi ni la haki. Hii ni sifa ya haki. Huu ni kama mti mzuri ambao unaota na kukua katika ardhi nzuri. Mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. (Surat Ibrahim aya ya 24-25). Yaani mti huu si wa kutumia mara moja, kama ilivyo kwa harakati nyingi zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali ulimwenguni kwa jina la Mapinduzi au mapinduzi ya kijeshi au kwa jina jingine na kubadilisha tawala, lakini haya matumizi yake ni mara moja tu. Kwa maana kwamba, utawala unaoingia madarakani baada ya mapinduzi huwa ni wa muda fulani na kisha baadaye hali hurejea kama ilivyokuwa hapo kabla au mbaya kuliko hapo awali. Neno la haki haliko namna hii; neno la haki ni lenye kubakia na kudumu. (Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu mbele ya hadhara ya wananchi wa mkoa wa Azerbaijan 17/02/2010).

Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuonyesha kwake taswira yenye utendaji unaofaa wa dini yalijitokeza kama tukio la kimaanawi na kuweza kuonyesha nafasi ya mafundisho na itikadi za kidini kama ni chimbuko la maarifa na miongozo ya maisha ya mtu binafsi, ya kijamii na kisiasa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakaonyesha uwezo wa bendera ya kimaanawi ya kupambana kwa ajili ya kuondoa satua ya madola ajinabi na yakaitangaza itikadi ya kidini na kupigania malengo matukufu kama ni tukio la kisiasa na kiini cha kiutamaduni. Jukumu hili likawa na umuhimu zaidi kwa kuweko Wilayat al-Faqih  yaani Utawala wa Fakihi na uwezo wa kuongoza wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi na kubakia na kudumu mfumo unaotawala hapa nchini. Wilayat al-Faqih au Utawala wa Fakihi ni nembo ya utambulisho wa mfumo wa Kiislamu na dhamana pamoja na bima ya kubakia na ni kinga ya hatari na mkengeuko tarajiwa.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Ukweli wa mambo ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiwa ni mapinduzi ya kifikra na kiutamaduni katika engo ya kimataifa, yameweza kuiarifisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa, tajiriba ya kipekee na ya kweli ya mfumo wa utawala wa kidini wenye ridhaa ya wananchi. Inapaswa kufahamu kwamba, wananchi kuwa na nafasi katika mfumo huu ni sehemu ya asili ya Uislamu na hakuna kitu nje ya hicho. Uislamu ni kwa ajili ya watu na kwa ajili ya kuwaongoza watu na umeteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wanadamu, na ndio maana daima unazingatia ukweli wa watu.

Dini ya Kiislamu inatambua suala la uwepo wa watu katika kutekeleza na kutetea haki zake kwamba, ni katika misingi ya awali kabisa. Sifa hii imepelekea kuimarika umoja na mshikamano wa wanabnchi katika Mapinduzi ya Kiislamu na hivyo kuwafanya wasimame imara na kutochoka kuhudhuria katika medani mbali. Fauka ya hayo, kila kona ya dunia nyoyo za walimwengu zimekuwa zikidunda  kwa ajili ya dini na Uislamu. Hali hii imepelekea na kuifanya Jamhuri ya Kiisdlamu kuwa kiigizo cha wapigania haki na uhuru duniani na hivyo kuyafanya Mapinduzi haya kuwa hai katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki maalumu umefikia tamati. Nakushuruni kwa kunitegea sikio kwaherini....

Tags