Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (3)
Miongoni mwa maswali yanayoulizwa kuhusiana na harakati ya mapambano Imam Hussein (as) ni kwamba, kwa nini Imam Hassan al Mujtaba (as) alifanya suluhu na Muawiya bin Abi Sufiyan lakini Imam Hussein (as) hakufanya suluhu na Yazid bin Muawiya?
Maulamaa wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia na wataalamu wa historia wanaamini kwamba, Imam Hassan na Imam Hussein (as) wote wawili walikuwa wakifuatilia lengo moja lakini hali na mazingira ya jamii ya Kiislamu katika zama za watukufu hao wawili yalihitilafiana na hayakuwa sawa na ya aina moja; hivyo kulihitajika mbinu na njia tofauti za kulinda Uislamu. Ni kwa kuzingatia suala hilo muhimu yaani kutofautiana mazingira na hali ya jamii ya Kiislamu katika zama za Imam Hassan na Hussein (as) ndiyo maana wanahistoria wananaamini kuwa, kama Imam Hassan (as) angekuwa katika mazingira na hali kama ile ya kipindi cha Imam Hussein, hapana shaka kuwa angepambana na utawala wa kidhalimu, kama ambavyo pia Imam Hussein pia aliheshimu suluhu na mapatano ya Imam Hassan na Muawiya kwa kipindi cha miaka 10 aliyoishi katika utawala wa Muawiya bin Abu Sufiyan baada ya kuuawa shahidi kaka yake Hassan al Mujtaba (as).
Kwa ujumla kuna mambo matatu muhimu yaliyokuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapambano ya Imam Hussein (as) ambayo yote yalikuwa na sura tofauti katika zama za suluhu ya Imam Hassan (as) na Muawiya.
Kwanza ni kuwa serikali dhalimu na ya kifisidi ya wakati huo ilimtaka Imam Hussein atoe mkono wa bai'a ya kiapo cha utiifu kwa mtawala wa wakati huo. Yazid aliwaamuru magavana wake kwamba: "Mlazimisheni Hussein kutoa mkono wa bai'a na kiapo cha utiifu tena bila ya huruma na bila kulegeza kamba." Wanahistoria wengine wanasema, Yazid bin Muawiya alimtaka gavana wake wa Madina kuchukua kiapo cha utiifu kutoka kwa Imam Hussein la sivyo ampelekee kichwa chake. Imam Hussein (as) alikataa katakata kufanya hivyo kwa sababu kukubali utawala wa Yazid fasiki na fisadi kulikuwa na maana ya kuhalalisha utawala huo wa kidhalimu na kujuzisha utawala wa kurithishana baina ya watawala madhalimu na wasiokuwa na dini kama Yazid. Kinyume chake, Muawiya hakumtaka Imam Hassan (as) kula kiapo cha utiifu kwa utawala wake, na suala hili lilikuwa miongoni mwa masharti ya suluhu na mapatano yaliyofikiwa kwamba, Muawiya bin Abi Sufiyan asimtake Imam Hassan kula kiapo cha utiifu na kumpa mkono wa bai'a. Haikuthibitika kwenye historia kwamba Muawiya bin Abi Sufiyan alimtaka Imam Hassan (as) au mtu yeyote mwingine kati ya Ahlubaiti wa Mtume kula kiapo cha utiifu na kutoa mkono wa bai'a. Kwa msingi huo suala la ulazima wa kula kiapo cha utiifu na kutoa mkono wa bai'a ambalo lilimfanya Imam Hussein asimame kupambana na Yazid halikuwepo katika zama na kipindi cha Imam Hassan al Mujtaba (as).
Jambo la pili ni kuwa, katika zama za Imam Hussein kulijitokeza watu wasiopungua elfu 18 wa mji wa Kufa huko Iraq waliotangaza kuwa wako tayari kusimama pamoja na Imam na kupambana na utawala dhalimu na fisadi wa Yazid bin Muawiya. Watu wa mji huo walikuwa wamechoshwa na utawala katili na wa kidhalimu wa miaka 20 wa Muawiya na walishuhudia kwa macho mienendo iliyokuwa kinyume na mafundisho ya Uislamu ya mtawala huyo. Walipoona Yazid akiidhihirisha waziwazi ufuska, kunywa pombe hadharani na kukejeli mafundisho ya Uislamu, walimwandikia barua Imam Hussein na kutangaza kwamba wako tayari kumsaidia katika harakati na mapambano yake dhidi ya utawala huo. Hivyo walimwalika huko Kufa. Yazid alipopata habari hiyo alimbadilisha gavana wake wa Kufa na kumsimika Ubaidullah bin Ziyad mahala pake ili akandamize na kuvunja azma yao ya kushirikiana na Imam Hussein (as). Mauaji, ukandamiza sambamba na kuwanunua baadhi ya vinara wa mji huo kwa vishawishi kama pesa, milki na vyeo, hatimaye viliwalazimisha wengi kati ya watu wa Kufa kumwacha Imam peke yake na wafuasi wachache lakini waliokuwa na imani madhubuti kama jabali. Hata hivyo barua na miito ya watu wa mji wa Kufa ilikuwa imetimiza hujja kwa Imam Hussein na kama asingeitikia wito huo basi historia ingemhukumu vingine.
Katika zama za Imam Hassan (as) mji wa Kufa ulikuwa na mazingira tofauti kabisa. Ulikuwa mji wa watu waliochoka na kuchoshwa na vita na hitilafu kubwa za kiitikadi na kimirengo. Kuliwapo watu kama wale waliokuwa na fikra za kundi la Khawarij waliokuwa na fikra finyu na potofu kuhusu Uislamu kwa upande mmoja, na katika upande mwingine aghlabu ya wakazi wa mji huo walikuwa wamechoshwa na vita vilivyoanzishwa na Muawiya dhidi ya utawala na serikali halali ya Imam Ali bin Abi Twalib (as). Hali na mazingira ya kipindi hicho ya Kufa yalikuwa mabaya kwa kadiri kwamba, hata Imam Hassan (as) hakuweza kutembea kwa amani na usalama mjini humo na daima alivaa ngao ya chuma ya kumlinda mishale na mashambulizi ya ghafla ya maadui zake.
Jambo la tatu ambalo lilimfanya Imam Hussein (as) asimame kupambana na Yazid bin Muawiya ni suala la kuamrisha mema na kukataza maovu. Ni kweli kwamba, watawala karibu wote wa ukoo wa Banii Umayya walikuwa madhalimu, watu waliozama katika ufuska na ufisadi, makatili na waovu lakini Yazid alikuwa daraja nyingine kabisa katika ufuska, dhulma na kukengeuka mafundisho ya dini. Kwa mfano tu kabla ya suluhu, Muawiya alimtumia Imam Hassan (as) waraka uliokuwa umetiwa saini yake tu na kumwambia Imam aandike masharti yote ayatako kwa ajili ya makubaliano hayo. Alihidi kwamba atayatekeleza yote na kufuata sheria za Kiislamu. Japokuwa Imam Hassan alijua vyema kwamba, mtu laghai na mwenye uchu wa madaraka kama Muawiya asingetekeleza ahadi zake, lakini alitaka Umma wa Kiislamu upate kuona na kushuhudia uhabithi na uhalifu wa kiongozi huyo kwa macho na tajiriba. Katika kipindi chote cha miaka 20 ya utawala wake Muawiya hakutekeleza vipengee vya makubaliano ya suluhu na kadiri muda ulivyopita ndivyo alivyotengana na kujiweka mbali zaidi na mafundisho ya Kiislamu. Alibadili sheria nyingi za Kiislamu, akadhulumu haki za raia na kumwaga damu za Waislamu wasio na hatia yoyote. Pamoja na hayo Muawiya alikuwa mjanja na laghai na hakuwa akidhihirisha ufuska na ufisadi wake hadharani na kadamnasi. Tofauti na Muawiya, Yazid mwanaye habithi na katili alikuwa akilewa na kucheza kamari hadharani. Alikua akicheza na mbwa na nyani katika majlisi ya utawala wake. Yazid hakusita hata kufanya madhambi makubwa kama kushambulia al Kaaba kwa mabomu, kuvamia mji mtakatifu wa Madina na kuruhusu askari wake kubaka na kunajisi wake na watoto wa masaha wa Mtume Muhammad (saw).
Ni mazingira haya ndipo Imam Hussein (as) aliposimama kuamrisha mema na kukataza maovu akikumbusha hadithi ya babu yake yaani Mtume Muhammad (saw) aliyesema: Mwislamu anayeona mtawala dhalimu anayehalalisha vitu vilivyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na kuvunja ahadi zake au akapinga Suna za Mtume na akatawala kwa dhulma na uonevu lakini hakukataza mambo hayo kwa ulimi na mkono wake, basi Mwenyezi Mungu atamuingiza mahala pa mtawala huo dhalimu, yaani motoni. Hapa ndipo Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as) aliposimama na kuamua kupambana na Yazid bin Muawiya akiwa pamoja na wapiganaji 72 na watu wa familia ya Mtume (saw).