Jul 16, 2024 16:50 UTC
  • Hamasa ya Imam Hussein (as)

Nukuu za historia zinasema, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib, mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW) aliingia Karbala siku ya Alhamisi tarehe Pili Muharram, 61 Hijiria.

Alipoingia kwenye ardhi hiyo, Imamu Hussein (AS) aliuliza watu waliokuwa katika msafara: “Ardhi hii inaitwaje? Walimwambia inaitwa Karbala! Imam Hussein (as) aliwaambia: "Teremkeni kwenye vipandwa vyenu! Hapa ndipo mahali pa kushusha mizigo yetu, hapa ndipo damu zetu zitakapomwagwa, na hapa ndipo mahali pa makaburi yetu. Haya niliambiwa na babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu."

Baada ya kuyasikia haya, masahaba wa Imam Hussein (as) waliteremka kwenye vipandwa vyao na kushusha mizigo na samani zao. Hurr bin Yazid al Riyahi, aliyekuwa akiongoza jeshi la Yazid pia alisimama na jeshi lake na kupiga kambi eneo hilo mkabala wa msafara wa Imam.

Imam Hussein aliwakusanya watoto wake, ndugu zake na watu wa familia yake kisha akamuomba dua akisema: "Ee Mola wangu Mlezi! Sisi ni kizazi cha Mtume wako, Muhammad. Bani Umayyah wametufukuza kwenye Haram ya babu yetu, na kutufanyia uovu. Mola wangu! Tulinde na madhalimu na utupe ushindi juu yao."

Kisha Imam Hussen aliwageukia masahaba zake na kusema: “Haya ndiyo majaaliwa yetu mnayoyaona. Nyakati zimebadilika. Uovu unadhihirika wazi, na hakuna kilichobakia katika fadhila na matukufu ya kibinadamu. Watu wanaishi katika maisha ya fedheha na udhalili. Ni vyema kwa mtu mwenye imani kujitoa mhanga katika mazingira kama haya ya fedheha na kukimbilia kwenye neema ya kukutana na Mola wake.

Katika mazingira kama haya, sikioni kifo isipokuwa saada, ufanisi na maisha  na madhalimu hawa si chochote isipokuwa mateso na taabu."   

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Imamu Hussein anasema: "Watu ni watumwa wa dunia, na dini yao imo katika ndimi zao. Huifuata dini maadamu inakidhi mahitaji ya maisha yao. Wanapopatwa na majaribio na misukosuko watu wanaoshikamana na dini huwa wachache."

Kwa maneno hayo, Imamu Hussein (as) anaashiria suala la majaribio na mitihani katika maisha ya wanadamu, ambayo ndiyo njia bora ya kujua ukweli, itikadi na dhati ya shakhsia za watu. Wako watu wengi wanaojionyesha kuwa ni waumini wanaojivika sura na joho la dini na uchamungu, lakini dhati za watu hawa haziwezi kutambuliwa, isipokuwa kwa majaribio na mitihani ya mabalaa na mashaka, na wakati maslahi yao ya kimaada na hata maisha yao yanapokuwa hatarini!

Sasa, mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu anakabiliana na adui wa Uislamu na yuko tayari kuuawa, kutoa mhanga familia yake, kwa ajili ya Allah SW. 

Omar Ibn Saad aliyekuwa kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya aliingia Karbala akiwa na wapanda farasi elfu nne wa Kufa, siku ya tatu ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria, na akamtuma mwakilishi wake kwa Imam Hussein na kusema: Muulize kwa nini amekuja katika eneo hili?

Imamu Hussein (as) alimjibu mjumbe wa Umar bin Saad na kusema: "Watu wa mji huu wameniandikia barua wakinitaka nije hapa. Kwa hiyo ikiwa hupendi kuja kwangu hapa Kufa, nitakwenda sehemu nyingine."

Omar bin Saad, ambaye alikuwa akijua hadhi ya juu ya Imamu Husein (sa) miongoni mwa Waislamu, na aliogopa kupigana vita na shakhsia huyo adhimu, alisema baada ya kusikia ujumbe huo kwamba: “Natumai Mwenyezi Mungu atanipa udhuru wa kutopigana naye." Baada ya hapo kulifanyika mazunguumzo ya ana kwa ana kati ya Imamu Hussein (as) na Omar bin Saad. Imam alimwambia: "Ewe mwana wa Saad! Unataka kupigana vita nami huku ukinijua na unajua vyema baba yangu ni nani? Hivi humuogopi Mwenyezi Mungu ambaye marejeo yako ni kwake? Je, hutaki kuwa pamoja nami na kuachana na Bani Umayyah, kwa sababu kitendo hiki kinamfurahisha zaidi Mwenyezi Mungu?"

Omar bin Saad alijibu kwa kusema: Ninaogopa kwamba katika hali hii wataharibu nyumba yangu huko Kufa.

Imam alisema: Nitakujengea nyumba kwa gharama yangu mwenyewe.

Bin Saad akasema: Ninaogopa kwamba wataninyang'anya shamba na mitende yangu.

Imam alimwambia: Nitakupa shamba bora zaidi huko Hijaz kuliko lile ulilonalo huko Kufa.

Omar bin Saad akasema: Mke wangu na mtoto wangu wako Kufa, na ninaogopa kwamba watauawa.

Baada ya kusikia visingizio vyake na kukata tamaa kwamba hawezi kutubu na kurejea, Imam (as)  alimwambia kwa masikitiko kwamba: "Kwa nini unang'ang'ania sana kumtii shetani! ... Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba hutapata ngano ya Iraq isipokuwa kiasi kidogo."

Historia inasema kuwa, baada ya kumuua mjukuu huyo wa Mtume na familia yake, Umar bin Saad alikwenda kwa gavana wa Yazid, Ubaidullah bin Ziyad kuomba malipo aliyopahidiwa ya utajiri na utawala wa eneo la Rei. Hata hivyo Ubaidullah alichana mkataba wa kumpa utawala wa Rei baada ya kutekeleza mauaji ya Imam na baadaye akauawa bila ya kufaidika na utajiri wa eneo hilo kama alivyoambiwa na Imam Hussein (as). Hivyo akawa amepata hasara ya dunia na Akhera.. Wassalam alaykum Warahmatullahi wabarakatuh... 

Tags