Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (4)
Kusikia kisa cha machungu na mateso ambayo yaliwapata wanawake na watoto wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) baada ya kuuawa shahidi Bwana wa Mashahidi, al-Imam Hussein (as) huumiza moyo wa kila mcha-Mungu na mpigania uhuru na utu wa mwanadamu na huenda kikamfanya ajiulize maswali haya muhimu kwamba je, ni kwa nini Imam Hussein (as) aliamua kuchukua na kuandamana na familia yake katika safari ya Karbala?
Na ni kwa nini hakuwaacha wanawake na watoto hao wa familia teule ya Mtume (saw) mjini Madina ua Makka? Tutajaribu kujibu maswali haya mawili muhimu katika kipindi chetu cha leo, karibuni.
************
Wanahistoria wametoa majibu tofauti kuhusiana na maswali haya na udharura wa kuwepo familia hiyo tukufu katika medani ya vita huko Karbala. Imam Hussein (as) alipotishiwa maisha yake kwa kulazimishwa kumbai Yazid bin Muawiya, aliona ni bora auhame mji wa Mdina, ambapo alifanya hivyo tarehe 28 Rajab mwaka wa 60 Hijiria huku akiwa ameandamana na karibu watu 100 wa Nyumba ya Mtume (saw) na wafuasi wake. Wengi wao walikuwa ni watoto, ndugu wa kike na wa kiume pamoja na wana wa ndugu zake. Baadhi ya watafiti wa historia wanaamini kwamba kutokana na ukweli kwamba Yazid hakuzingatia misingi yoyote ya kidini wala kimaadili, kulikuwepo na uwezekano mkubwa kwamba kama Imam Hussein (as) angeiacha familia yake mjini Madina, mtawala huyo dhalimu angetumia chombo cha dola la Bani Ummayyia kukandamiza, kutesa na kuifunga jela familia hiyo tukufu kwa lemgo la kumlazimisha Imam asalimu amri na hatimaye kumbai dhalimu Yazid. Hivyo uamuzi wa Imam Hussein (as) wa kuandamana na familia yake katika safari hiyo ulikuwa ni uamuzi wa kimantiki kabisa kwa kadiri kwamba kwa muda wa miezi minne familia hiyo ya Mtume (saw) iliishi mjini Makka kwa amani na utulifu kamili pembeni ya mtukufu huyo. Yazid alipotambua kwamba Imam Hussein (as) hakuwa tayari kwa vyovyote vile kumbai mtawala huyo aliyekiuka wazi misingi yote ya kidini, alitoa amri ya kuuawa mjukuu huyo wa Mtume katika mji mtakatifu wa Makka. Imam aliamua kuondoka katika mji huo mtakatifu ili kuepusha kumwagwa damu katika eneo hilo takatifu la Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.
Dalili nyingine inayotolewa na watafiti wa historia kuhuisana na hatua ya Imam hussein (as) ya kuandamana na familia yake katika safari ya Karbala ni kwamba, alipoondoka katiika miji mitakatifu ya Madina na Makka, hakuwa na nia ya kupigana vita. Kama kusudio lake lingekuwa ni kupigana vita bila shaka angeelekea Karbala huku akiwa na jeshi kubwa bila ya kuandamana na wanawake na watoto. Hivyo ni wazi kuwa hakuwa na nia yoyote ya kupigana vita kwa kuandamana na msafara uliojumuisha wanawaka, mabinti, watoto wadogo na hata watoto wachanga wa kunyonya. Wakati watu wa Kufa mjini Iraq walipofahamu kuwa Imam Hussein (as) alikuwa amekataa kumbai Yazid, walimwandikia maelfu ya barua wakitangaza uungaji mkono wao kwake na kumtaka afike mjini hapo na kuasisi hapo makao yake. Imam aliyehisi kutokuwepo tena amani na usalama kwake na familia yake mjini Makka aliamua kuhamia katika mji huo wa Kufa. Hapa pia Imam hakuona haja ya kuiacha familia yake mjini Makka kwa sababu hakuwa na nia yoyote ya kwenda kupigana vita mjini Kufa, bali ilikuwa ni safari ya kuhajiri kwa kawaida. Hivyo kuandamana kwake na familia yake lilikuwa ni jambo la kawaida na kimantiki kabisa. Mbali na dalili hizo, kuna nukta nyingine muhimu kuhusiana na sababu ya Imam Hussein (as) kuandamana na familia yake katika safari ya Karbala, nayo ni kwamba Imam alitaka kulinda na kuhfadhi Imam wa baada yake kutokana na hatari ya kuuawa na pia kufikisha ujumbe muhimu wa Ashura ambapo wafiwa wakiongozwa na Bibi Zeinab (as) walitekeleza vyema jukumu hilo. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as), Ali bin Hussein, al-Imam Sajjad (as) alichukua nafasi hiyo muhimu ya kuuhudumia umma wa Kiislamu. Kwa matakwa yake Mwenyezi Mungu, Imam Sajjad (as) alikuwa mgonjwa wakati wa kupiganwa vita vya Karbala na hivyo hakupata fursa ya kushiriki moja kwa moja katika vita hivyo. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein na wafuasi wake wema (as), maadui waliyashambulia mahema ya familia ya Mtume (saw) kwa lengo la kutaka kumuua Imam Sajjad (as). Pamoja na hayo, Bibi Zainab alisimama kishujaa mbele ya maadui hao na hivyo kuwazuia kutekeleza njama yao hiyo chafu dhidi ya mtukufu huyo. Nafasi ya Bibi Zainab (as) baada ya vita vya Karbala ilikuwa muhimu kiasi kwamba wanahistoria wanaamini kwamba kama bibi huyo mtukufu asingekuwepo katika medani ya vita ya Karbala Siku ya Ashura, basi tukio hilo chungu la Ashura lingefukiwa katika jangwa hilo na hivyo kufanya mapambano ya Imam Hussein (as) kutokuwa na natija yoyote. Bani Ummayyia walikuwa wakitaka kwa kumuua Aba Abdillahil Hussein, waizime kabisa sauti ya Tauhidi na ibada ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuuzika Uislamu halisi ulioletwa na Mtume Mtukufui (saw) katika jangwa la Karbala. Walihangaisha, kutesa na kuitembeza kama mateka familia ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu katika miji tofauti na kutoka nyumba hadi nyingine kwa madhumuni ya kutaka kuimarisha misingi ya utawala wao lakini kinyume na walivyotarajia, msafara huo wa mateka kutoka Kufa kuelekea Sham, uligeuka na kuwa wa kuwafikishia watu wote ujumbe wa Imam Hussein (as) na wakati huohuo kufichua kashfa na uozo wa Yazid. Kabla ya hapo Muawiyya alikuwa amefanikiwa kuficha misingi ya uozo huo wa utawala wa Bani Ummaiyya mbele ya watu wa Sham. Lakini wakati msafara wa mateka hao wa Nyumba ya Mtume ukiongozwa na Bibi Zainab, ulipowasili katika malango ya mji huo na hotuba za bibi huyo mtukufu kutikiza mbingu za mji huo, sauti za mivunjiko ya masanamu ya utawala wa Bani Ummayyia yaliyokuwa yametengenezewa wakazi wa mji huo zilianza kusikika. Ni kutokana na ukweli huo ndipo hotuba ya Bibi Zainab (as) ilipomalizika, Yazid aliingiwa na hofu na kuanza kutetemeka na kujaribu kuwatupia wengine mzigo wa jinai zake dhidi ya familia na ukoo huo mtukufu wa Mtume (saw), lakini hakufanikiwa katika hilo na ndio maana laana na chuki ya Mwenyezi Mungu itaendelea kumuandama milele, yeye pamoja na babu zake.