Vijana, Walinzi Imara na wa Daima wa Mapinduzi ya Kiislamu
(last modified Sun, 03 Feb 2019 11:41:24 GMT )
Feb 03, 2019 11:41 UTC
  • Vijana, Walinzi Imara na wa Daima wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ujana ni kipindi kinachong'aa cha maisha ya mwanadamu ambacho japokuwa si kirefu lakini athari zake zinabakia muda mrefu na huwa na taahira kubwa katika maisha ya kiumbe huyo.

Tunapochunguza historia tunaona kwamba, vijana wamekuwa na mchango mkubwa katika harakati na mageuzi makubwa ya kihistoria. Katika kipindi cha mwanzoni mwa Uislamu wakati Mtume Muhammad (saw) alipotangaza waziwazi dini hiyo ya Mwenyezi Mungu, vijana walikuwa safu ya kwanza kumwamini na kumsaidia mtukufu huyo. Vijana walitumia fitra na maumbnile yao safi kujiunga na mageuzi makubwa ya Mtume Muhammad (saw) na dini ya Uislamu kiasi kwamba mtukufu huyo anawasifu kwa kusema: 

اِنَّ اللهَ بَعَثَنی بَشیراً وَ نَذیراً فَحالَفَنیِ الشُّبّانُ و خالَفَنیِ الشُّیوخُ.  

Mwenyezi Mungu alinituma mimi ili niwe mtoa bishara njema na muonyaji, vijana walijiunga nami na wazee walinipinga.

جوانان و انقلاب اسلامی

Hii leo pia baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanyika kwa ajili ya kutekeleza haki na uadilifu, vijana ndio walio mstari wa mbele wa harakati hiyo na wana mchango muhimu na mkubwa katika mageuzi hayo. Imam Ruhullah Khomeini pia alikuwa akiamini kwamba, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulitokana na mchango mkubwa na kujitolea kwa vijana na amesema kuwa: "Nyinyi vijana mumeifikisha hapa harakati hii kwenye ushindi kutokana na nguvu ya imani yenu na mnapaswa kulinda nguvu hiyo ya imani. Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya taifa kubwa la Iran na nyingi vijana wenye ari, werevu na hima kubwa. Nyinyi vijana mmeifikisha harakati hii kwenye ushindi na kufanikiwa kung'oa mizizi ya ufisadi kwa kiasi fulani nchini Iran. Kwa matakwa yake Mola Mlezi, mtaweza pia kukamilisha harakati hii na kung'oa kikamilifu mizizi ya uovu hapa nchini."   

Japokuwa katika kipindi cha utawala wa kifalme wa Shah Pahlavi vijana walikuwa wakiunda sehemu kubwa ya jamii ya Iran, lakini utawala huo ulizuia shughuli huru za kisiasa, kijamii na kiutamaduni za tabaka hilo kwa ukandamizaji, mbinyo na sera za kidikteta; na katika upande mwingine utawala huo ulifanya jitihada za kupotosha na kupindisha fikra na vipawa vya vijana ili wasijishughulishe zaidi na masuala ya nchi yao. Katika uwanja huu miongozo na harakati ya Imam Khomeini na vigogo wengine wanamapinduzi ilikuwa na mchango mkubwa katika kuwaamsha na kuwazindua vijana. Wakati huo vijana wengi walijiunga na harakati na makundi ya siri yaliyokuwa yakisimamiwa na vigogo wa vuguvugu la Mapinduzi. 

Mwaka 1356 Hijria Shamsia (1978) kizazi cha vijana cha Iran kiliyaona mambo kiliyokuwa kikiyatafuta kwa miaka mingi kama utambulisho wa Kiislamu, kupigania uhuru na uadilifu na kupinga dhulma katika nara na kaulimbiu za harakati za mageuzi za Imam Khomeini. Kwa utaratibu huo kizazi hicho kiliamua kujiunga na harakati hiyo na kuingia katika medani ya mapambano kwa kadiri kwamba, mwanzoni mwa vuguvugu la Mapinduzi ya Kiislamu hapo mwaka 1979 vijana ndio waliokuwa mstari wa mbele wa harakati hiyo.

جوانان در انقلاب اسلامی

 

Tangu wakati huo vijana walishika usukani wa harakati za maandamano na mikusanyiko iliyokuwa ikifanyika dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah katika miji na vijiji vya Iran. Vijana walipata utambulisho wa kitaifa na kidini katika harakati hiyo na kuhisi majukumu ya kutengeneza mustakbali mpya wa Iran. Mahudhurio makubwa ya vijana wanamapinduzi wa Iran katika tukio la tarehe 13 Aban, ushiriki wao mkubwa katika mapigano ya mitaani, mahudhurio yao katika harakati ya kuteka pango la ujasisi la Marekani mjini Tehran (ubalozi wa Marekani) na kutwaa kambi na vituo kadhaa vya jeshi la Shah na vilevile kushiriki kwa wingi vijana katika vita vya miaka 8 ya kujitetea kutakatifu dhidi ya mashambulizi ya Saddam Hussein ni kielelezo cha mchango mkubwa na utakaobakia hai wa tabaka hilo katika Mapinduzi ya Kiislamu na historia ya sasa ya Iran. Harakati za vijana katika vyuo vya kidini, vyuo vikuu, harakati za kisiasa na kadhalika na mawasiliano yao na matabaka mengine ya wananchi viliyafanya maeneo hayo hususan misikiti kuwa ngome imara za mapambano dhidi ya dhulma na utawala wa kidhalimu wa Shah.

Wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 8, vijana walikuwa bega kwa bega na matabaka mengine ya wananchi katika kulinda na kutetea nchi yao na Jamhuri changa ya Kiislamu licha ya wengi miongoni mwao kuwa na umri mdogo. Vijana wengi wa zama hizo waliamua kusitisha masomo katika vyuo vikuu na kuelekea katika medani za vita na baadhi yao walishika nafasi za juu kama ukamanda wa majeshi na uongozi wa vita. Akieleza sifa kuu za vijana wa kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: "Kujipinda katika ibada, kutumia busara na mantiki, ushujaa na ukakamavu, kujitolea, kusimama kidete na kuona mbali ni miongoni mwa sifa aali za vijana hawa zilizowafanya simba wa mchana na wafanya ibada nyakati za usiku, na kwa sababu hiyo hayati Imam Khomeini alilitaja suala la kulea na kukuza vijana kama hawa kuwa ndio ushindi mkubwa kulizo mwingine."

جوانان در جنگ تحمیلی عراق علیه ایران

Kama ambavyo walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, vilevile vijana walikuwa na nafasi muhimu katika kudumisha na kuimarisha mapinduzi hayo. Baada ya kumalizika vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na mabeberu kwa kumchochea Saddam Hussein kwa shabaha ya kuyaua Mapinduzi ya Kiislamu na dola changa la Kiislamu nchini Iran, vijana walibeba majukumu mazito ya kuijenga upya nchi yao. Katika vita hivyo vya kulazimishwa idadi kubwa ya raia waliuawa, maelfu walijeruhiwa na miundombinu ya nchi vilikuwa vimeharibiwa. Hivyo viongozi na wananchi walijifunga kibwebwe kwa ajili ya kuijenga upya nchi. Wakati huo tabaka la vijana ndilo lililotoa mchango mkubwa zaidi  kwa ajili ya kustawisha uchumi na kukomesha utegemezi wa nchi kwa madola ya kigeni. Katika miaka hiyo ya baada ya vita vya kulazimishwa, vijana walifanya kazi kubwa ya jihadi hususan katika maeneo ya vijijini na miji midogo ya kujaribu kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na vita.

Katika miaka iliyofuata pia Iran ilipiga hatua kubwa katika masuala ya kielimu na kisayansi na suala hilo liliakisi harakati kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran katika njia ya maendeleo na ustawi. Anga huru na ya wazi iliyoletwa na Mapinduzi ya Kiislamu katika jamii hususan baina ya tabaka la vijana ilistawisha vipawa na moyo wa kujiamini baina ya Wairani.

جوانان ایرانی بعد از انقلاب اسلامی در مجامع علمی متعددی در جهان مقام آورده اند.

Hii leo vijana wa Iran ya Kiislamu wanaoelewa umuhimu wa elimu na maendeleo wanajipinda katika kutafuta elimu kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu na kila siku tumekuwa tukisikia habari za uvumbuzi na ubunifu wa vijana wasomi na wanasayansi hodari wa Iran. Nishati ya nyuklia ni miongoni mwa nyenzo muhimu sana kwa ajili wa ustawi wa nchi mbalimbali na madola makubwa yametumia nishati hiyo hata katika kutengeneza silaha za mauaji ya halaiki. Hata hivyo madola hayo hayo awali hayakutaka Iran ya Kiislamu iwe na uwezo wa kupata nishati hiyo muhimu tena kwa matumizi ya kiraia na ustawi wa kielimu. Madola hayo hayakutosheka na hayo bali yalikabiliana na irada ya Iran ya Kiislamu ya kutaka kuwa na uwezo wa nishati ya nyuklia kwa kuwaua kigaidi wasomi na wanasayansi vijana wa Iran kama Shahidi Mustafa Ahmad Roushan na Mhandisi Majiid Shahriyari. Hata hivyo njama hizo hazikufua dafu na leo hii Iran ya Kiislamu inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi chache duniani zenye uwezo wa kurutubisha madini ya uranium na kuzalisha nishati ya nyuklia.

Hii leo wasikilizaji wapenzi kutokana na vipawa, uwezo, ubunifu na imani yao kubwa kwa Uislamu na matukufu yake, vijana wa Iran wanahesabiwa kuwa miongoni mwa makundi bora zaidi ya jamii katika nchi mbalimbali. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana nchi za Magharibi zikaamua kulilenga tabaka hilo muhimu kwa propaganda chafu na kueneza utovu wa maadili na ufuska kwa shabaha ya kupotosha vipawa vya vijana na kuvielekeza katika mkondo usio sahihi. Hata hivyo vijana wa Iran wameonesha kuwa, daima wataendela kuwa nguzo muhimu na fahari ya Jamhuri ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusu vijana wa Iran kwamba: "Mustakbali wa taifa ni wenu nyinyi. Kama mtaendelea kukuza na kustawisha sifa hizi hapana shaka kuwa nchi hii itafika kwenye kilele cha ukamilifu katika miaka michache ijayo. Maadui na wanaolitakia mabaya taifa walikuwa na lengo la kufuta kabisa jina la Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu baina ya vijana, na Marekani idhibiti mambo yote ya nchi hiyo. Waliendeleza mashambulizi yao ya aina zote kwa lengo hilo lakini hii leo tunakabiliana na kizazi cha vijana ambacho imani yake, vipawa vyake na uwezo wake ni mkubwa zaidi kuliko wa kizazi cha kabla yake, na tabaka hili limejizatiti zaidi kwa ajili ya kumfukuzilia mbali adui kuliko kizazi cha kabla yake."        

Tags