Nov 11, 2019 10:33 UTC
  • Wiki ya Umoja wa Kiislamu-4: Nafasi ya Umoja katika kuepusha chuki dhidi ya Uislamu

Katika ulimwengu wa leo chuki dhidi ya Uislamu, au kwa jila la kiingereza Islamophobia, ni jambo linalopewa uzito na kuenezwa kwa namna maalumu katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi.

Propaganda hizo chafu zinaenezwa kwa madhumuni ya kuwadhihirishia walimwengu sura isiyokuwa sahihi kwamba Waislamu ni watu wanaotumia mabavu na ugaidi katika kufikia malengo yao. Kwa kuzingatia propaganda hizo chafu, Umma wa Kiislamu unapasa kuimarisha umoja na mshikamano wake ili kuzima njama hizo za maadui.

Kwa mnasaba huu adhimu wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo inaadhimishwa kwa lengo la kuenzi uzawa na maulidi ya Mtume Mtukufu saw, tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambao katika siku hizi wamo katika maadhimisho haya matukufu. Tunapasa pia kumshukuru Imam Khomeini (MA), Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa kuanzisha na kutangaza Wiki ya Umoja wa Kiislamu kutokana na Riwaya mbili tofauti za ndugu wa Kisuni na Kishia kuhusiana na uzawa wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Khomeini (MA) alitangaza  kipindi cha tofauti ya Riwaya mbili hizi kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kuashiria umuhimu wa kuwepo Umoja kati ya makundi yote ya Kiislamu na kuimarisha umoja na udugu miongoni mwao. Neema ya uwepo na ujumbe wa Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) iliepelekea kuongoka mwanadamu na kufuata njia sahihi ya uokovu na bila shaka ujumbe huo wa amani, uadilifu, heshima, maadili bora na kuwatetea wanyonge ni nguzo muhimu za mafundisho ya Kiislamu ya mtukufu huyo (saw), jambo ambalo bila shaka mwanadamu wa leo analihitajia zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Mtume (saw) alikuwa na angali ni 'Rehema kwa Walimwengu' na mbeba ujumbe wa amani na urafiki kwa wanadamu, madhehebu na dini zote za mbinguni.

Qur'ani Tukufu ambacho ni kitabu kinachobeba ujumbe wa uokovu na saada kwa wanadamu wote inasema katika Aya ya 19 ya Surat Aal Imran: Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Kwa maana kuwa Uislamu ndio dini ya hakika na ukweli ambayo inaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Vilevile kwenye kitabu hiki kitakatifu kuna Aya nyingi mno ambazo zinasisitiza kwamba Uislamu ni dini ya rehema na huruma na iliyo na maarifa muhimu na ya kina yanayomuokoa mwanadamu, na kumtaja Mtume kuwa mwokozi na mwongozaji wa jamii ya wanadamu. Kwa msingi huo Mtume amearifishwa kuwa ruwaza na kiongozi mwema na mwenye huruma na upendo si kwa Waislamu pekee bali kwa wanadamu wote duniani. Kwa msingi huo Waislamu wanapasa kufuata mfano wa Mtume (saw) katika maisha yao yote na kuhuisha ujumbe na mafundisho yake kwa sababu yeye ndiye nembo ya Uislamu na aliyepewa na Mwenyezi Mungu jukumu la kuarifisha dini hii yenye upendo na rehema kubwa kwa wanadamu.


Historia inathibitisha ukweli huu kwamba tokea zama za Nabii Adam (as) hadi wakati wa kudhihiri Mwokozi wa Ulimwengu, Imam Mahdi (AF), fitina za wafuasi wa shetani dhidi ya ujumbe wa Uislamu ulioletwa na Mtume Muhammad (saw) zitaendelea kuwepo. Ushahidi uliopo unaonyesha wazi kwamba fitina hizo ambazo zimeongezeka katika zama zetu hizi na ambazo zinaenezwa kwa njia tofauti na mikono ya shetani kupitia wafuasi wake na hasa Wazayuni ambao tokea enzi za kale wamekuwa na chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Mtume Muhammad (saw), zinaenezwa kwa njia ambayo si rahisi kuitambua na  kila siku zinaendelea kudhihiri kwa namna tofauti na mpya.

Hii leo chuki dhidi ya Uislamu na Ushia zimefikia kilele cha propaganda za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi ili kujaribu kuwaonyesha walimwengu kinyume na ukweli, kwamba Uislamu na Waislamu ni sawa na utumiaji mabavu na ugaidi. Kuanzishwa kwa makundi ya kigaidi na kuongezeka vitendo vya mauaji ya kutisha katika nchi za Kiislamu, kumezidisha woga na chuki dhidi ya Uislamu, vitendo ambavyo vinaenezwa na maadui kwa ajili ya kuwafanya watu wauogope Uislamu na Waislamu. Makundi ya kigaidi na kitakfiri kama Daesh na al-Qaida ambayo yameanzishwa na Wamagharibi wenyewe, yameeneza chuki na kuufanya Uislamu uogopwe duniani, ili kuzuia kuenea Uislamu halisi uliwemnguni. Ni wazi kuwa makundi haya yanayotenda jinai za kutisha kwa jina la Uislamu yameanzishwa kwa makusudi ili kudhamini maslahi ya Wamagharibi na wakoloni mamboleo ambao katika kipindi chote cha historia wamekuwa na chuki na uadui mkubwa dhidi ya dini hii ya mbinguni. Kwa kueneza fitina na chuki dhidi ya Uislamu halisi ulioletwa na Mtume Muhammad (saw), maadui hao daima wamekuwa wakifanya juhudi za kutenganisha na hatimaye kuzidhoofisha nchi za Kiislamu. Zinafanya hivyo ili zipate njia ya kuweza kuibua ghasia na hofu miongoni mwa nchi za Kiislamu, kuzigawa na hatimaye kuzidhibiti na kupora maliasili zao. Kwa masikitiko makubwa, baadhi ya nchi vibaraka za Kiislamu kama Saudi Arabia si tu kwamba zinayafadhili kwa hali na mali makundi hayo ya kigaidi yanayoendelea kuharibu jina zuri la Uislamu bali zenyewe zimeingia kwenye medani ya kuua na kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Umma wa Kiislamu kama tunavyoshuhudia jinai hizo zikitekelezwa wazi na nchi hiyo ya kifalme dhidi ya Waislamu masikini wa Yemen na vile vile nchini Bahrain. Inasikitisha kuona kwamba nchi hiyo imeingia katika mapatano na maadui sugu wa Uislamu kama Marekani na utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuaa na kuwachinja kinyama Waislamu bila huruma.

Wimbi hilo la chuki dhidi ya Uislamu mbali na kusababisha dhana mbaya dhidi ya Waislamu, limehatarisha  maisha ya Waislamu wengi wanaoishi katika nchi za Magharibi, na hasa wanawake wa Kiislamu wanaolengwa moja kwa moja kutokana na mavazi maalumu ya sitara wanayovaa. Kwa msingi huo wanawake wa Kiislamu wanalazimika kubakia manyumbani na kutojishughulisha na kazi za nje ya nyumba, kama vile kujishughulisha na masomo na ufundishaji katika vyuo vikuu, jambo ambalo bila shaka huzidisha mashinikizo ya kiuchumi na matatizo mengine mengi katika familia za Kiislamu zinazoishi katika nchi hizo. Mashinikizo na chuki zinazoelekezwa kwa jamii za Kiislamu huwafanya wengi kukimbia nchi hizo na kuhamia kwingine. Ni wazi kuwa Wamagharibi walio na chuki dhidi ya Uislamu wanatambua vyema kwamba uwepo wa Waislamu katika nchi hizo hupelekea Wamagharibi kupata kutambua na kuelewa mafundisho ya Uislamu na hivyo kuchangia kuenea kwa dini hii tukufu ya mbinguni katika nchi hizo, kinyume na wanavyotaka maadui hao wa Uislamu.

Licha ya kuwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu ni jambo chungu kwa Waislamu wote lakini suala hilo limeleta fursa mpya kwa ajili ya Waislamu kuimarisha umoja na mshikamano wao kwa lengo la kukabiliana na mabeberu walio na chuki kubwa dhidi ya Uislamu na wakati huohuo kuwapa fursa ya kuuarifisha Uislamu sahihi mbele ya walimwengu. Umoja na mshikamano bila shaka ndio njia pekee ya kukabiliana na fitina pamoja na mifarakano inayoibuliwa na maadui wa Uislamu na Waislamu wanapasa kutembea kwa uangalifu na mwamko mkubwa katika njia hiyo. Kwa kutilia maanani mazingira nyeti ya hivi sasa, Waislamu wanatakiwa kuimarisha umoja wao kwa kushikamana na mambo ya pamoja na kujiepusha na yale yanayowatenganisha ili kuweza kuzima njama za maadui dhidi yao. Ni wazi kuwa iwapo Waislamu wataimarisha umoja na mshikamano huu miongoni mwao, bila shaka adui hatakuwa tena na fursa ya kueneza chuki, fitina na mifarakano miongoni mwao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 46 ya Suratul Anfal: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.

Kwa hakika mifarakano na migawanyiko kati ya Waislamu huwadhoofisha kwa ndani na kuwakosesha heshima kwa nje na katika jamii. Hivyo Waislamu wanapasa kuwa watiifu na kuimarisha umoja miongoni mwao na iwapo kutatokea jambo lolote linalokwenda kinyume na matakwa yao wanapasa kufanya juhudi za kulitatua na likiwa nje ya uwezo wao wasubiri ili Mwenyezi Mungu awanusuru kama alivyoahidi mwenyewe katika kitabu chake kitakatifu.

Mwenyezi Mungu anaarifisha umoja kuwa sifa muhimu zaidi ya Waislamu kwa kusema katika Aya ya 92 ya Surat al-Anbiyaa: Kwa hakika huu Umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu. Kwa hivyo niabuduni Mimi. Ili kuimarisha umoja katika Umma wa Kiislamu, Mtume Mtukufu (saw) aliwaunganisha Waislamu wa Ansar na Muhajirin chini ya bendera ya umoja na udugu wa Kiislamu. Umoja huo daima ulikuwa ukiwakurubisha zaidi Waislamu hao na kuimarisha nguzo zao za kidini na kiimani na kuratibu miamala yao ya kijamii. Kupitia miongozo na mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw) Waislamu hao waliweza kudhihirisha kwa njia ya kuvutia mno ushirikiano na udugu wao wa Kiislamu, udugu ambao unapaswa kutawala katika jamii ya Kiislamu na ya mwanadamu kwa ujumla.

Wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo ni nembo ya umoja na mshikamano wa Waislamu wote ni fursa ya kipekee na isiyo na mfano wake kwa ajili ya Waislamu kuweza kuondoa tofauti zao ndogondogo zisizo na maana na kushikamana kikamilifu na Qur'ani Tukufu pamoja na mafundisho ya Nabii wa Rehema, Muhammad al-Mustafa (saw) ili kuweza kufikia umoja na mshikamano wa jamii ya Kiislamu.

Kwa mara nyingine,  tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wasikilizaji wetu wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mnasaba huu adhimu wa maadhimisho ya maulidi ya Mtume wetu Mtukufu (saw), huku tukiutakia Umma mzima wa Kiislamu amani, usalama, utulivu, heshima, nguvu na afya njema. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuuondolea Umma huu fitina, mifarakano na shari ya matakfiri ambao wameuletea umma huu unaompenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa nyoyo zao zote, balaa kubwa. Tunamwomba aweze kuufanya Umma huu kuwa Umma bora zaidi kuliko umma nyingine zote, kama alivyoahidi mwenyewe katika Qur'ani Tukufu, na kuufanya uweze kuwashinda maadui wake.

Tags