Kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Muhammad Baqir (as)
(last modified Sun, 18 Jul 2021 05:31:02 GMT )
Jul 18, 2021 05:31 UTC
  • Kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Muhammad Baqir (as)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalum kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW.

Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa Waislamu wote ulimwenguni hususan wafuasi wakweli wa Ahlul-Baiti (AS) ninakukaribisheni kwa pamoja tutupie jicho japo kwa mukhtasari historia na maisha ya mtukufu huyu. Karibuni.

 

Mwezi 7 Mfunguo Tatu Dhulhijja ni miongoni mwa siku za kumbumbuku za mmoja wa watu watukufu ambao ni kigezo bora kwa wanadamu. Katika siku hii, ulimwengu wa Kiislamu ulitumbukia kwenye majonzi makubwa baada ya kumpoteza mtu mtukufu, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Baqir AS. Imam Muhammad bin Ali al-Baqir AS, ni Imamu wa Tano katika silsila ya Maimamu watoharifu 12 wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Baqir alizaliwa tarehe 3 Mfunguo Tano Safar mwaka 57 Hijria katika mji wa Madina. Mwaka 95 Hijria Imam Baqir AS alichukua Uimamu wa kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS. Imam huyu alichukua jukumu zito la Uimamu kwa muda wa miaka 19 mpaka alipouawa shahidi kwa kupewa sumu katika siku kama ya leo, kwa amri ya Hisham bin Abdul Malik, Khalifa na kiongozi wa Bani Umayyah na kuzikwa katika makaburi matakatifu ya Baqii katika mji mtakatifu wa Madina huko Saudi Arabia. Katika zama ambazo Imam Baqir AS alikuwa akijishughulisha na kazi ya kufundisha na kulea wanafunzi katika mji wa Madina, kipindi hicho watu walikuwa na kiu kali ya kutafuta elimu na walikuwa wakihudhuria kwa wingi darsa zake mjini Madina na kunufaika na bahari ya elimu ya kiongozi huyo wa Waislamu.

Bwana mmoja aliyejulikana na watu wote kwamba ni mtu wa Sham, baadhi ya wakati alikuwa akijumuika na wanafunzi wa Imam Baqir AS na kushiriki katika darsa zake. Hata hivyo Bwana huyo alikuwa akijulikana kwamba, ni mmoja wa wapinzani wakali wa Ahlul Bayt AS.

 

Siku moja Bwana huyo alikwenda kwa Imam Baqir AS na kumwambia: "Mimi siwapendi Ahlul Bayt. Lakini kutokana na kuwa wewe una umahiri wa kuzungumza na umebobea pia katika elimu mbalimbali, ninakuja katika darsa zako ili nistafidi na elimu yako tu, lakini mimi si katika wafuasi wako." Imam Baqir AS alimtazama Bwana yule kwa tabasamu kisha akamwambia: "Hakuna kitu ambacho kitajificha kwa Mwenyezi Mungu."

Siku zikasonga. Kila mara Bwana yule alipopata fursa alikuwa akimtolea maneno ya kejeli, dhihaka na kumvunjia heshima Imam Baqir AS. Baada ya kupita siku nyingi, Bwana yule alipatwa na maradhi. Ndugu zake walifanya kila wawezalo kumtafutia matibabu, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda. Maradhi yake yakawa makali zaidi na zaidi na kumdhoofisha siku baada ya siku, kiasi cha kumfanya ashindwe hata kutembea na hivyo kubakia kitandani. Usiku mmoja akiwa katika hali mbaya ya maradhi, aliota ndoto ya ajabu na ya kutisha. Alikurupuka kutoka usingizini na kuwaita watu wake wa karibu na kuwaambia:

"Nimeota ndoto ya ajabu. Nikiwa usingizi nimeota roho yangu imetenganishwa na mwili wangu na kuona lahadha na muda wa mauti yangu ukiwa umewadia. Lakini katika sekunde hiyo, mara nikamuona Muhammad bin Ali yaani Imam Baqir (AS) akiniombea shufaa. Mwenyezi Mungu akaikubali dua yake na mimi nikarejea duniani. Sasa ninakuombeni muendee kwa Muhammad Baqir na mumtafadhalishe aje hapa. Laiti ningelikuwa na nguvu za kutembea basi mimi mwenyewe ningelienda kwake, lakini nasikitika hali yangu ni dhaifu na hainiruhusu kufanya hivyo."

Ndugu zake wakiwa wamepigwa na butwaa wakamuuliza kwa mshangao mkubwa, kwani wewe si katika wapinzani wake wakubwa? Bwana yule akawaambia ndugu zake: "Mimi nilikuwa nikimfanyia uadui siku zote lakini hakuna wakati ambapo alikasirika na kuudhika na vitendo vyangu hivyo vibaya, na badala yake alikuwa ni mwenye subira kubwa na alistahamili na kuvumilia kushiriki kwangu katika darsa zake. Yeye ni mtu mwema na ni shakhsia mkubwa ambaye hata nimemuona katika ndoto akiniombea dua, kwa hakika ni jambo la kushangaza sana."

 

Habari za kuugua Bwana yule zilimfikia Imam Baqir AS na baada ya kutekeleza Swala ya faradhi ya al-Fajir alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Bwana yule. Aliingia nyumbani kwake na kutoa salamu. Kisha akamuita Bwana yule kwa jina lake. Bwana yule wa Sham aliposikia sauti ya Imam, ikawa ni kana kwamba amefufuka. Imam akamsogelea na kwa upole akamsaidia kunyanyuka kitandani na akakaa kitako. Kisha Imam akawataka ndugu zake watengeneze dawa maalumu na kisha yeye mwenyewe akamnywesha Bwana yule. Kama alivyosema Imam, Bwana yule alipata nafuu na kupona baada ya siku chache. Siku ya kwanza tu alipopata nguvu ya kutembea, moja kwa moja alikwenda kwa Imam. Alikaa mbele yake kwa heshima na adabu hali ya kuwa machozi yanamtiririka na akamtaka Imam amsamehe makosa yake yote ya kumkosea adabu na kumkejeli na kisha akasema: "Nashuhudia kwamba, wewe ni Hujja wa Mwenyezi Mungu kwa watu. Kila mtu ambaye anashikamana na asiyekuwa wewe atakosa uongofu."

Maisha ya Imam Muhammad Baqir AS yameuachia umma wa Kiislamu mambo yenye thamani kubwa. Kwa upande mmoja, Imam Baqir alipigania kuimarisha misingi na itikadi za kidini kwa watu, na kwa upande wa pili alitumia mbinu za kutoa hoja za kimantiki na thabiti ili kubatilisha fikra potofu zilizokuwa zinaenezwa katika umma wa Kiislamu. Imam Baqir AS ndiye aliyeanzisha mapinduzi makubwa ya kifikra katika ulimwengu wa Kiislamu.

Imam Muhammad Baqir AS alikitumia kipindi cha maisha yake mjini Madina kueneza elimu na maarifa ya dini sambamba na kulea wanafunzi ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi na wanazuoni wakubwa. Imam alikuwa akibanisha matawi ya elimu kwa umahiri wa hali ya juu ambapo Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu walifunga safari za mbali kumkusudia yeye mjini Madina wakitokea katika pembe mbalimbali za dunia. Walielekea kwa mtukufu huyo ili kunufaika na dafina, hazina na bahari pana ya elimu aliyokuwa nayo. Mkakati mkuu wa Imam Muhammad Baqir AS ulikuwa ni kuimarisha misingi ya kiutamaduni na kiitikadi ya watu. Imam Baqir aliweka jiwe la msingi la harakati kubwa ya kielimu na kiutamaduni na kuandaa mazingira ya kuasisiwa Chuo Kikuu cha Kiislamu.

Imam Muhammad Baqir (as) amezikwa katika makaburi ya Baqii

 

Miongoni mwa mambo mengine yaliyopewa kipaumbele na Imam Baqir AS ni kusimama kidete kutetea haki na wakati huo huo kupambana kwa nguvu zote na dhulma. Imam Baqir alibainisha na kufichua uovu wa watawala wa Bani Umayyah katika minasaba na fursa mbalimbali alizopata. Imam Baqir alikuwa akiamini kwamba, viongozi na watawala wana nafasi katika ufanisi au kunakamika na kuharibikiwa watu katika jamii wanazoziongoza. Katika zama hizo, watawala wa Bani Umayyah walishughulishwa zaidi na kuimarisha tawala zao kwa kupambana na mizozo ya kisiasa iliyokuwepo baina yao. Hivyo hali hiyo kwa kiasi fulani ilitoa fursa ya kuenezwa mafundisho ya kiutamaduni na kiitikadi ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Moja ya hatari zilizokuwa zikiukabili umma wa Kiislamu wakati huo ni fikra za kupandikiza zilizoingizwa katika umma huo. Hivyo kazi kubwa ya Imam Baqir ilikuwa ni kupambana na fikra hizo potofu kwa hoja za kimantiki na alitumia Qur'ani, sunna za Bwana Mtume na sira za Ahlul Bayt kuwa nguzo na marejeo makuu ya kutatua migogoro ya kifikra na kiitikadi iliyoukumba umma wa Kiislamu. Aliwaongoza watu vizuri kwa kutumia chemchemi hizo tajiri na zenye thamani kubwa.

Mbali na kubobea katika elimu, Imam Baqir AS alipambika pia kwa sifa bora za kimaadili na ukamilifu wa kibinadamu. Hata lakabu yake ya Baqir nayo inaashiria kubobea na kutabahari kwake mno katika elimu. Baqir ni neno la Kiarabu lenye maana ya ubukuaji, uchimbuaji na upambanuaji wa kina. Muhammad bin Abdul Fattah, mmoja wa wanavyuoni wa madhehebu ya Hanafi anasema: Imam Baqir alipewa lakabu ya Baqirul Ulum (mchimbua elimu) kutokana kwamba alikuwa akifukua hazina zilizokuwa zimejificha za maarifa na hekima.

Amma ukosoaji wa mtukufu huyo kwa maovu yaliyokuwa yakitendwa na watawala wa Bani Umayyah hayakuwafurahisha watawala hao. Mtawala dhalimu wa wakati huo Hisham Abdul-Malik alikuwa akimbana sana Imam na wafuasi wake, na mara nyingi alitoa hukumu ya kuuawa wafuasi wa Imam. Mtawala huyo alitoa amri ya kuletwa Imam Baqir AS katika makao makuu ya utawala wake yaani Sham kutoka Madina. Kuwepo Imam huko Sham kulileta nishati na harakati kubwa za kielimu hasa kwa watu waliokuwa na kiu ya kutafuta elimu na kujifunza maarifa ya Uislamu. Jambo hilo liliongeza mapenzi ya watu kwa Imam. Kuona hivyo, Hisham akatoa amri ya Imam kurejeshwa tena Madina. Hata hivyo, moto wa chuki na uadui wa Hisham haukuzimika katika moyo wake. Hatimaye katika siku kama ya leo Hisham akatoa amri wa kupewa sumu Imam Baqir AS na hivyo Imam akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote ulimwenguni hususan wapenzi na maashiki wa  Ahlul Bayt AS kwa mnasaba wa kukumbuka siku alipouawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags