Kuendelea kwa safari ya kukomesha utumwa nchini Marekani
(last modified Sat, 19 Nov 2022 14:56:54 GMT )
Nov 19, 2022 14:56 UTC
  • Kuendelea kwa safari ya kukomesha utumwa nchini Marekani

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika kipindi cha Makala ya Wiki ambacho leo kitazungumzia ubaguzi na ubaguzi wa rangi wa kimfumo huko Marekani.

Baada ya kupita miaka 160 tangu kukomeshwa kwa utumwa huko Marekani, ubaguzi wa rangi na aina mbalimbali za utumwa bado zinashuhudiwa katika nchi hiyo. Katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika hivi karibini nchini Marekani, mbali na raia kuwachagua wabunge na magavana, raia wa majimbo matano ya nchi hiyo walitoa maoni yao kuhusu iwapo aina zote za utumwa ni kinyume cha sheria au la. Zaidi ya asilimia 89 ya washiriki katika uchaguzi huo wa tarehe 8 mwezi huu wa Novemba walipiga kura ya "ndiyo" kwa maandishi yaliyosema: "Utumwa wa aina zote ni marufuku". Wapiga kura wengi katika majimbo ya Tennessee, Alabama, na Oregon ambao wameidhinisha kufanyika marekebisho ya katiba zao, wamefanya hivyo kwa viwango tofauti vya uungaji mkono, na idadi ndogo ya waliojitokeza kwa ujumla.

Utumwa ulikomeshwa huko Marekani mnamo 1865 baada ya karne mbili na nusu. Hata hivyo baadhi ya aina za utumwa zingalipo hadi sasa katika jamii za nchi hiyo. Wafungwa nchini Marekani hawatambuliwi kuwa ni "watumwa," lakini wanaharakati wa kukomeshwa aina zote za utumwa katika majimbo matano ya Alabama, Louisiana, Oregon, Tennessee, na Vermont wanasema, matendo wanayofanyiwa wafungwa wengi katika jela za nchi hiyo ni sawa na utumwa. Kwa sasa, wafanyakazi 800,000 hawalipwi kwa kazi wanazofanya katika jela za Marekani. Wafungwa wanaofanyishwa kazi katika majimbo saba, hawalipwi mishahara kabisa.

Savannah Eldridge wa Mtandao wa Kitaifa wa Kukomesha Utumwa nchini Marekani (Abolish Slavery National Network) anasema, "Watu wengi huuliza kwa nini huu usiitwe utumwa ilhali ni utumwa halisi. Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, watu weusi walitumiwa kama watumwa kama sehemu ya mfumo wa adhabu na magereza." Wanaounga mkono mageuzi wanasema, sheria hizi ni za kinyonyaji na lazima zikomeshwe. Watafiti wa masuala ya haki za binadamu nchini Marekani wanaamini kwamba, mfumo huu una mizizi katika karne za utumwa wa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika. Katika miaka ya baada ya kukomeshwa rasmi utumwa, zilipitishwa sheria ambazo zililenga hasa kuwakandamiza watu weusi na kuwapeleka magerezani ambako walipaswa kufanya kazi kama mapunda. Curtis Ray Davis, ambaye alitumia kipindi cha miaka 25 ya umri wake akifanyishwa kazi ya bure katika gereza la Louisiana kwa tuhuma za mauaji ambayo hakuyafanya anasema katika kitabu cha kumbukumbu zake alichokipa jina la Slave State: Evidence of Apartheid in America kwamba: "Marekani haijawahi kuwa na siku isiyokuwa na utumwa."

Davis alilazimishwa kufanya kazi mbalimbali katika gereza maarufu la Jimbo la Louisiana. Alifungwa katika gereza lililopewa jina la "Angola" kwa kumbukumbu ya watumwa wa Kiafrika wa Angola waliokuwa wakipelekwa huko kwa kazi za utumwa miaka mingi iliyopita. Curtis Ray Davis ameandika katika kitabu cha "Nchi ya Watumwa' kwamba: "Nilifanya kazi kwa miaka 25 na nikarudi nyumbani nikiwa  na dola 124."

Savannah Eldridge, kutoka "Mtandao wa Kitaifa wa Kutokomeza Utumwa" anasema: "Ingawa utumwa umepigwa marufuku, lakini ukweli ni kwamba kilichofanyika ni kuhamishwa umiliki wa watumwa pekee yake, na sasa umiliki wa watumwa umehamishwa kutoka umiliki wa mtu binafsi na kupelekwa kwenye utumwa unaofadhiliwa na serikali."  

Magereza ya kibinafsi ni jukwaa lingine kuu la kazi ya kulazimishwa huko Marekani. Marekani ina zaidi ya magereza 200 ya kibinafsi yenye wafungwa zaidi ya laki moja na elfu 30. Wafungwa katika jela hizo hufanya kazi kwa saa nyingi katika mazingira magumu na kuzalisha faida ya dola bilioni 5 kwa mwaka kwa ajili ya wamiliki wa magereza hizo za kibinafsi nchini Marekani, lakini wanalipwa senti 20 hadi 40 tu kwa saa kwa kazi wanazofanya. Inatupasa kusema pia kwamba, kazi ya kulazimishwa nchini Marekani wanafanyishwa watu wa kundi jingine kubwa. Kwa sasa, zaidi ya watu 100,000 wanasafirishwa kwenda Marekani kutoka nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kufanyishwa kazi za kulazimishwa au utumwa wa ngono. Baya zaidi ni kwamba "wafanyakazi" hawa hawalipwi chochote mkabala wa "kazi" zao. Kwa sababu hiyo, baadhi ya wachambuzi wanalitaja jambo hili kuwa ni "utumwa wa kisasa au utumwa mamboleo wa Marekani". Julai mwaka huu, muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za binadamu ulituma ripoti maalumu yenye kurasa 21 kwa Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, ukitaka Marekani ishinikizwe ili ikomeshe ubaguzi wa rangi na sera za kukanyaga haki za binadamu katika magereza ya nchi hiyo.

Curtis Ray Davis mwandishi wa kitabu cha Slave State: Evidence of Apartheid in America

Katika ripoti yake, muungano huo uliandika maelezo kuhusu madhara ya kijamii na ya kudumu katika jamii za watu weusi na matokeo haribifu ya vifungo vya kibaguzi vya Wamarekani weusi vinavyotokana na sera za ubaguzi wa rangi. Vilevile inaeleza uharibifu mkubwa na wa aina tofauti unaosababishwa na hukumu kali za magereza na kufungwa jela katika jamii za watu weusi kwa lengo la kuondoa mienendo yote ya ubaguzi wa rangi katika mfumo wa sheria wa Idara ya Magereza ya Marekani. Katika ripoti hiyo kumezungumziwa ukatili unaofanyika katika seli za mtu mmoja, mienendo ya kuamiliana na wafungwa kama watumwa, kuwatumikisha kazi za lazima, na kufungwa wazazi wa familia za watu weusi kama baadhi ya mifano ya ukiukaji wa haki za binadamu na sera za ubaguzi wa rangi za serikali ya Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya muungano wa mashirika yanayotetea haki za binadamu, Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza, Agosti 8, mwaka huu wa 2022, ulianza mchakato wa kupitia upya ni kwa kiwango gani Marekani inafuata na kutekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi wa Rangi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa sera za ubaguzi wa rangi katika magereza ya Marekani, hasa jela za Kusini mwa nchi hiyo, imethibitishwa kuwa idadi ya watu weusi wanaofungwa ni mara tano zaidi ya wazungu katika magereza ya serikali. Katika majimbo kama Alabama, Arkansas, Florida, Georgia, Louisiana, Mississippi, Carolina Kaskazini, Carolina Kusini, (North Carolina, South Carolina) na Texas, ambapo jamii za watu weusi ni asilimia 38 ya jumla ya watu wote, watu weusi wanaunda asilimia 67 ya jumla ya wafungwa wanaoshikiliwa katika magereza za majimbo haya.

Idadi ya watu weusi wanaofungwa katika seli na vifungo vya upweke ni mara nane zaidi ya watu weupe katika katika magereza ya majimbo hayo, na uwezekano wa kushikiliwa wafungwa hao katika seli na vifungo vya upweke kwa muda mrefu sana ni mara 10 zaidi ya wazungu. Kinachoonekana zaidi katika ripoti hii ni kuwa magereza nyingi za Marekani hazifuati viwango vya chini kabisa vya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia wafungwa.

Watu weusi wanaendelea kuwa wahanga wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani

Kwa ujumla tunapaswa kusema kuwa, misingi ya serikali ya Marekani inasimama juu ya ubaguzi wa rangi. Tangu mwanzoni, wahamiaji wa Ulaya walisimamisha msingi wa ustaarabu wa Marekani kwa kuwaua wenyeji wa bara la Amerika na kuwalazimisha wengine kuwa wakimbizi, na baadaye waliendeleza ustaarabu wao kwa kuwanyonya watumwa weusi kupitia mfumo wa utumwa. Inatupasa pia kuweka wazi kwamba, licha ya sifa zote ambazo zimetolewa kwa Abraham Lincoln kutokana na kukomesha utumwa nchini Marekani, lakini ukweli ni kwamba, Lincoln hakupinga ubaguzi wa rangi, bali alitetea suala la kukomeshwa utumwa na kudumisha ubaguzi wa rangi kulingana na maslahi yake ya kisiasa. Wakati huo vita kati ya Kaskazini na Kusini katika miaka ya 1860 viliwapa matumaini watumwa weusi wa Kusini, na wengi wao waliyakimbia maeneo ya Kusini wakielekea Kaskazini na kujiunga na jeshi la Lincoln. Hatimaye, vita kati ya Kaskazini na Kusini viliisha kwa ushindi wa Kaskazini kutokana na eneo la Kaskazini kuwa na viwanda na idadi kubwa zaidi ya jamii ya watu, na wakati huo ndipo lilipotolewa Tangazo la Ukombozi wa Watumwa nchini Marekani. Hata hivyo uhuru huo pia haukuwa na faida kwa watumwa wa Marekani. Kwa sababu baada ya hapo watu weusi waliokuwa watumwa bila ya rasilimali ya aina yoyote, sasa walikuwa wakihitajia chakula, makazi, kuoa na kadhalika. Hawakuwa na ujuzi wowote wa masuala ya viwanda ili waajiriwe viwandani huko Kaskazini mwa Marekani, wala hawakupewa kazi na ajira maeneo ya Kusini kwa sababu wazungu wa maeneo hayo waliwatambua weusi hao kuwa ndio sababu ya kushindwa kwao.

Harakati za kupinga utumwa, Tangazo la Ukombozi wa Watumwa, na sheria za Bunge la Congress havikukomesha ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Kwa sababu hiyo, aina mbalimbali za ubaguzi wa rangi ziliendelea kushuhudiwa nchini humo hadi mwishoni mwa miaka ya 1960. Vuguvugu la kupigania haki za kiraia lililoongozwa na Martin Luther King lilimaliza rasmi ubaguzi huo wa rangi. Hata hivyo ubaguzi wa rangi bado unaendelea katika taasisi, idara na utamaduni wa Marekani. Weusi bado wanatambuliwa kuwa raia wa daraja la pili na tabaka la chini la jamii ya Marekani. Ubaguzi katika ajira, ukosefu mkubwa wa kazi baina ya Wamarekani weusi ikilinganishwa na wazungu, asilimia kubwa ya umaskini na kutojua kusoma na kuandika, idadi kubwa ya wafungwa weusi, unyanyasaji na ubaguzi wa polisi, n.k., yote hayo ni dhihirisho la ubaguzi wa rangi wa kimfumo unaoendelea kufanyika nchini Marekani. Mienendo ya kitaasisi ya Wamarekani dhidi ya watu weusi inaonesha kuwa, ukatili dhidi ya watu wa tabaka hilo haujakoma hata baada ya kupita zaidi ya karne moja na nusu baada ya Tangazo la Ukombozi.