Falsafa na historia ya Idul Adha
Mwezi 10 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah ni moja ya siku kuu zenye baraka nyingi ambazo umuhimu wake umesisitizwa katika aya za Mwenyezi Mungu za Qur'ani Tukufu na Hadith za Mtume na Maimamu watoharifu.
Idul Adh'ha ni moja ya sikukuu kubwa za Waislamu bali hii ndiyo sikukuu kubwa zaidi kuliko hata ya Idul Fitr ya Mfunguo Mosi. Sikukuu hii imeitwa Idul Adh'ha kwa sababu neno "al Adh'ha" lina maana ya kurefuka mwanga wa asubuhi na mchana. Ni vile kurefuka mwanga wa jua baada ya kuchomoza wakati wa asubuhi na kuingia kipindi cha kabla ya adhuhuri. Wakati huo ndio huitwa Dhuha. Kipindi hicho cha dhuha ndicho kinachotumiwa na mahujaji kuchinja wanyama na kufanya udh'hiya katika siku ya kumi ya mwezi wa Mfunguo Tatu na jina la Idul Adh'ha yaani sikukuu ya kuchinja limetokea hapo.
Kimsingi sikukuu ya Idul Adh'ha ni kwa ajili ya Mahujaji walioko kwenye ardhi ya Wahyi. Kuchinja pia ni wajibu kwa Mahujaji tu lakini pia ni sunna iliyotiliwa mkazo sana kwa wale ambao wako nje ya maeneo ya amali za Hija. Kwa hakika, falsafa ya Idul Adh'ha ni kuyapeleka matamanio ya mwili na nafsi ya Hujaji kwenye madhabahu ya kuchinja huko ili mwenye kuhiji awe msafi asiye na chembe ya madhambi, mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kabla ya siku ya nahr yaani siku ya kumi ya Mfunguo Tatu, huwa imetangulia siku ya tisa yaani siku ya Arafa. Katika sunna za siku hii ya Arafa yaani mwezi 9 Mfunguo Tatu, kumesuniwa kufanya anali nyingi za kheri kama kusoma dua iliyonasibishwa na Imam Husain AS. Tunapoisoma dua hiyo huwa tunapata fursa ya kutambua uudhaifu wetu na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hayo huwa ni maandalizi ya kuingia kwenye sikukuu ya Mfunguo Tatu yaani mwezi 10 Dhul Hijja ambayo ndani yake huwa tunajitolea nafsi zetu na kuchinja na kuyatupilia mbali matamanio ya kidunia na kumuoimba Allah atumiminie rehema Zake.

Hapa sasa wapenzi wasikilizaji tunapenda kuangalia historia fupi ya sikukuu hii kubwa katika Uislamu. Idul Adh'ha ni sikukuu ambayo ilikuwepo karne nyingi hata kabla ya kuanza kuandikwa historia ya mwanadamu. Suala hili la kuchinja na kutoa muhanga limekuwepo muda mrefu mno. Wanadamu wa zamani walikuwa wakitoa dhabihu za wanyama na hata wanadamu kwa ajili ya kutabaruku na kuomba msaada wa miungu yao. Kuchinja na kutoa kafara ni jambo la zamani sana na limekuwepo tangu zama za Nabii Adam Abul Bashar yaani baba wa wanadamu wote (AS) na ilizingatiwa kuwa ni miongoni mwa misingi ya kidini ya kaumu na nyumati zilizotangulia. Kumerekodiwa matukio mengi ya kihistoria kuhusu suala hili la kutoa kafara. Hapa tutatoa mifano kadhaa.
1- Tuanze na kafara ya wana wa Nabii Adam AS, yaani Qabil na Habil. Kafaraya watoto hao wa Nabii Adam AS inahesabiwa kuwa ndiyo kafara ya kwanza kutolewa hapa duniani. Kafara hiyo imebainishwa kwa uwa katika aya za 27 hadi 30 za Surat al Maadia. Kwa muhtasari sana ni kwamba, wana wawili wa kiume wa Nabii Adam AS walioitwa Qabil na Habil, walikuwa wakulima na wachungaji kwa utaratibu. Yaani Qabil alikuwa mkulima na Habil alikuwa mchungaji. Walikuwa na wanyama wengi na maeneo chungu nzima ya kilimo, ya maji na ya malisho ya wanyama. Nabii Adam AS aliwaamuru kutoa kafara katika njia ya Mwenyezi Mungu. Qabil alichagua mnyama bora kabisa wa kumtoa kafara katika njia ya Mwenyezi Mungu lakini Habil alichagua makapi ya ngano ya hali ya chini kwa ajili ya kafara hiyo. Kafara ya Qabil ilikubaliwa na ya Habil haikukubaliwa na hilo lilimtia husda na choyo kikubwa habil na moto wa hasira na chuki uliwaka katika nafsi yake kiasi kwamba ilimsukuma hadi kumuua ndugu yake baba mmoja mama mmoja kutokana na husda na chuki kubwa aliyokuwa nayo. Habil akafanya kwa mara ya kwanza kabisa dhambi kubwa ya kuua katika historia yote ya mwanadamu na aliangamia hapa duniani na Akhera pia atapata adhabu kali.
2- Wakati Nabii Nuh AS alipoandaa kafara maalumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya gharika kuu. Nabii Nuh AS alichinja wanyama wengi katika njia ya Allah baada ya kuokoka kimiujiza kwenye gharika hiyo. ***Mfano mwingine ni namna Nabii Ibrahim AS alipojitolea kumtoa muhanga mwanawe wa pekee, yaani Nabii Ismail AS kwenye kisa maarufu ambayo kimeelewa pia katika aya za 102 hadi 107 za Surat al Swaffat.
3- Katika vitabu vyao vya historia Mayahudi wamenukuu kwamba, wakati wa Nabii Musa AS kulikuwa na aina mbili za utoaji kafara. Moja ilikuwa ni kafara ya damu na nyingine ilikuwa ni kafara isiyo ya damu. Kafara ya damu iligawika sehemu tatu, kafara iliyochomwa moto ambapo mnyama aliyechindwa alikuwa habakii chochote isipokuwa ngozi yake tu. Pili ilikuwa kafara kwa ajili ya kusamehewa madhambi na sehemu ya kafara hiyo ikichomwa moto na sehemu iliyobakia wakipewa makuhani na kafara ya tatu ilikuwa ni kwa ajili ya kuwa salama na kuwa mzima mwilini na watu walikuwa wanakhitarishwa kula au kutokula nyama ya mnyama aliyetolewa kafara.
4- Amma kafara isiyo ya damu kwa mujibu wa itikadi hizo za Mayahudi ni ya kumwachia mnyama jangwani ada ambayo Waarabu nayo waliiga kutoka kwa Bani Israili na wakifanya hivyo kwa ajili ya kujikurubisha kwa miungu yao. Mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu yalipiga marufuku na kuharamisha ada na dasturi hiyo ya kijahilia kama ilivyokuja kwenye aya ya 103 ya Surat al Maida kwa majina ya Bahira na Saiba.
5- Kwa upande wa Wakristo nao, wao wanaamini kuwa kafara inamuhusu Masih Isa tu. Wanadai kuwa Isa Masih alijitoa muhanga damu yake ili kuwabebea dhambi wanadamu na ndio maana moja ya misingi muhimu ya dini ya Kikristo kwa uchache kila mwezi mara moja au kila mwaka mara moja waende kwa kasisi na mchungaji kumpa sadaka na kukiri madhambi yake yote aliyetenda katika kipoindi hicho ili mchungaji na kasisi huyo amsamehe madhambi yake kwa itikadi yao.
6- Katika upande wa Waarabu wa zama za ujahilia pia, wakati wakuu wa makabila walipokuwa wanafika Makka, wakazi wa mji huo walikuwa ndio wenyeji wao na makundi yote mawili yaliamini kuwa ni wajibu wao kuchinja ngamia, ng’ombe na kondoo kwa ajili ya kafara ya mifugo yao na kuwalisha masikini na wenye njaa. ***Idul Adh'ha kama Idul Fitr, ni moja ya sikukuu kubwa za Waislamu ambayo inaitwa pia kwa majira ya Yaumun Nahr na Yaumul Adh'ha. Idi hizi mbili zilipewa umuhimu mkubwa sana na Bwana Mtume Muhammad SAW na Maimamu watoharifu AS.
7- Amma tukija katika mambo ambayo yanapaswa kufanywa katika sikukuu ya Idul Adh'ha ambayo ni miongoni mwa sikukuu kubwa na muhimu katika Uislamu, tunapenda hapa kunukuu mafundisho ya viongozi watukufu wa Uislamu. Imenukuliwa kwamba, kila wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa anatoka nyumbani kwake kwa ajili ya Sala za Idul Fiftr na Idul Adh'ha alikuwa akivaa nguo mpya na akipaza sauti yake kwa takbira.
Imepokewa pia hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS akisema kwamba mtu anatakiwa kustaftahi na kula chochote kabla ya kwenda kusali Sala ya Idul Fitr lakini kwa sikukuu ya Mfunguo Tatu yaani Idul Adh'ha astaftahi baada ya kurudi kutoka kwenye Sala ya sikukuu hiyo.

Kama ilivyopokewa, si wajibu kuchinja kwa wale ambao hawakwenda Hija lakini kuchinja siku ya 10 ya Mfunguo Tatu ni sunna iliyogogotezwa na kuhimizwa mno na Mtume Muhammad SAW na Maimamu watoharifu. Imepokewa hadithi kwamba siku moja Umma Salama (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) alikwenda kwa Bwana Mtume SAW na kumwambia Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Idul Adh'ha imeshawadia na mimi sina fedha za kununulia mnyama wa kuchinja, je nikope na kutoa sadaka? Mtume akasema: Kopa; kwa sababu mkopo huo umeshalipwa.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.