Jul 24, 2023 11:27 UTC
  • Waislamu Afrika Kusini wataka jibu la haraka kwa kuvunjiwa heshima Qurani

Waislamu nchini Afrika Kusini wameitaka serikali ya nchi hiyo itoe taarifa ya kulaani vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya.

Waislamu hao wameliambia shirika la habari la Iran Press kuwa, serikali ya nchi hiyo ina wajibu wa kuyatetea na kuyalinda matukufu ya kidini, kwa kuwa Katiba ya nchi hiyo inatambua haki za dini za walio wachache.

Waislamu hao nchini Afrika Kusini wamebainisha kuwa, kwa kuwa bara la Afrika ni makazi ya idadi kubwa ya Waislamu, mataifa ya bara hilo yanapaswa kushirikiana na kutoa sauti moja katika kulaani vitendo vya kudhalilishwa Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Wamesema hatua ya serikali za Ulaya kuruhusu kuvunjiwa heshima Kitabu hicho Kitukufu cha Waislamu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, kwa mara nyingine tena imeonyesha unafiki na undumakuwili wa madola ya Magharibi.

Waislamu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Iran, Iraq, Lebanon, Yemen na Nigeria wamefanya maandamano makubwa na kulaani wimbi la vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark.

Serikali za nchi za Ulaya licha na kushuhudia namna Waislamu katika nchi mbalimbali walivyoghadhibishwa na hujuma hizo, lakini zinaandaa mazingira ya kuendelezwa vitendo hivyo badala ya kukabiliana na uhalifu huo dhidi ya matukufu ya kidini ya Waislamu zaidi ya bilioni mbili.

Waislamu Afrika Kusini wamesema hatua ya watawala wa Ulaya kuruhusu kufanyika vitendo hivyo vya kuvunjia heshima Qurani Tukufu kwa hjimaya ya maafisa usalama, inalenga kuvuruga na kuyeyusha thamani za Uislamu na dini nyinginezo duniani.

Tags