Muungano wa upinzani DRC wakataa kufanya mazungumzo na serikali
Muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekataa ombi la kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Joseph Kabila.
Patrick Mayombe Mwenyekiti wa muungano wa upinzani huko DRC amesema kuwa, wanapinga takwa la Rais Joseph Kabila la kuweko mazungumzo na wapinzani kwani wanaona kama ni aina fulani ya hadaa.
Amesema kuwa, wapinzani wanaona kuwa, kufanyika mazungumzo hayo ni juhudi za kutaka kumbakisha madarakani Rais Kabila ambaye muhula wake wa uongozi unamalizika na kunapaswa kufanyika uchaguzi Novemba mwaka huu.
Taarifa ya muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imebainisha kwamba, njia pekee ya kuiepusha nchi hiyo na sokomoko la kisiasa inalokabiliwa nalo ni kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa.
Kwa miezi kadhaa sasa, jamii ya kimataifa imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa huko Congo DR, huku waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila wakitaka zoezi hilo lisogezwe mbele wakisisitiza kuwa mazingira ya sasa hayaruhusu kufanyika uchaguzi.
Hivi karibuni Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ilisema kuwa huenda Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akasalia madarakani hata baada ya kumalizika muhula wake iwapo uchaguzi mkuu hautafanyika mwezi Novemba mwaka huu.