Aug 11, 2023 07:56 UTC
  • Jarida la Wall Street: Imarati imetuma silaha kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko Sudan

Jarida la Kimarekani la Wall Street Journal limefichua katika ripoti yake kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu unatoa misaada ya kijeshi kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinavyopigana na jeshi la Sudan kwa miezi kadhaa sasa.

Gazeti hilo limesema kuwa, ndege ya mizigo ya Imarati ilitua katika uwanja wa ndege wa Uganda mwanzoni mwa mwezi Juni, na imethibitishwa kuwa ilikuwa imebeba silaha na zana za kivita, wakati ambapo nyaraka rasmi zilionyesha kuwa ndege hiyo ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu ya Imarati kwa wakimbizi wa Sudan. 

Gazeti hilo la Marekani limewanukuu maafisa wa Uganda wakisema kwamba, ndege hiyo ya Imarati iliruhusiwa kuendelea na safari yake hadi uwanja wa ndege wa Um Jaras mashariki mwa Chad, na wamethibitisha kwamba walipokea amri kutoka kwa wakuu wao ya kuacha kukagua safari za ndege kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu na kwamba walikatazwa kutopiga picha yoyote ya ndege hizo.

Wall Street Journal limesema kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanashutumu Vikosi vya Msaada wa Haraka - vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, kuwa vimefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia.

Sudan

Kulingana na gazeti hilo, UAE unacheza kamari yake kwa kutoa msaada kwa vikosi vya Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kwa ajili ya kulinda maslahi yake nchini Sudan, kufaidika na eneo la kimkakati kwenye Bahari Nyekundu na Mto Nile, na kupata hifadhi kubwa ya dhahabu ya Sudan.

Gazeti hilo la Marekani limekumbusha kuwa waangalizi wa Umoja wa Mataifa hapo awali waliishutumu UAE kwa kutuma silaha kwa vikosi vya Jenerali mstaafu wa Libya, Khalifa Haftar, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani, mabomu ya kuongozwa na leza na magari ya kivita.

Tags