Algeria: Uingiliaji wa kijeshi nchini Niger utatishia utulilvu wa eneo zima
Mkuu wa Jeshi la Algeria ameonya kuhusu jaribio la kuivamia kijeshi Niger na kusema kuwa uvamizi wowote wa kijeshi wa madola ya kigeni nchini Niger utatishia utulivu na usalama wa eneo zima la Sahel ya Afrika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Brigedia Jenerali Said Chengriha, Mkuu wa Komandi Kuu ya Jeshi la Algeria alisema hayo jana Jumanne katika Mkutano wa 11 wa Usalama wa Kimataifa huko Moscow mji mkuu wa Russia na huku akionya dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi wa kigeni nchini Niger amesema kuwa, kuivamia kijeshi nchi hiyo ya magharibi ya Afrika kwa kiwango chochote kile kutapelekea kukosekana zaidi utulivu katika ukanda wa Sahel Afrika. Lakini wakati huo huo amesema nchi yake inaunga mkono juhudi za kidiplomasia za kurejesha utawala wa Katiba nchini Niger.
Jenerali Chengriha ameongeza kuwa, hali ya sasa katika eneo la Sahel barani Afrika ni matokeo ya moja kwa moja ya mgogoro wa Libya na uingiliaji wa kigeni katika eneo hilo tangu mwaka 2011 kama ambavyo pia hali hiyo mbaya kwenye ukanda huo inachangiwa pia na vita baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vilivyoanza tarehe 15 Aprili mwaka huu wa 2023.

Jumatano ya tarehe Julai 26, jeshi la Niger lilifanya mapinduzi na baadaye kumuweka kizuizini rais wa nchi hiyo, Mohammed Bazoum.
Katika upande wa eneo la ardhi, Niger ndiyo nchi kubwa zaidi katika eneo la Afrika Magharibi. Ina ukubwa wa kilomita mraba milioni 1.3 na ina wakazi milioni 24 ambao takriban wote ni Waislamu.