Kiongozi wa mapinduzi Niger: Niko tayari kumwachia huru Bazoum
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101450-kiongozi_wa_mapinduzi_niger_niko_tayari_kumwachia_huru_bazoum
Kiongozi wa mapinduzi nchini Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, amekutana na ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu wa Nigeria, huku mashinikizo za kikanda na kimataifa yakiongezeka dhidi ya utawala wa kijeshi wa Niamey kwa shabaha ya kurejesha utawala wa kikatiba.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 25, 2023 03:08 UTC
  • Kiongozi wa mapinduzi Niger: Niko tayari kumwachia huru Bazoum

Kiongozi wa mapinduzi nchini Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, amekutana na ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu wa Nigeria, huku mashinikizo za kikanda na kimataifa yakiongezeka dhidi ya utawala wa kijeshi wa Niamey kwa shabaha ya kurejesha utawala wa kikatiba.

Duru za habari zinasema, Tiani amesisitiza katika mazungumzo ya pande hizo mbili kwamba hapingi suala la kuachiliwa huru rais aliyezuiliwa, Muhammad Bazoum, lakini amekataa kurejea kwake madarakani.

Ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu wa Nigeria unaoongozwa na Abdullahi Bala Lau, uliwasili mjini Niamey Jumatano wiki hii na kukutana na Jenerali Abdourahamane Tiani katika ziara yake ya pili tangu baada ya mapinduzi hayo.

Awali baraza la kijeshi linalotawala Niger lilikaribisha upatanishi wa ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu wa Nigeria kwa shabaha ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Niger.

Katika muktadha wa juhudi zinazohusiana na utatuzi wa mgogoro Niger, Abdulsalami Abubakar, rais wa zamani wa Nigeria na mkuu wa ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) katika mazungumzo na baraza la kijeshi la Niger, amesema mkuu wa baraza la kijeshi la nchi hiyo, Jenerali Abdourahamane Tiani, amekataa ombi la ujumbe huo la kumrejesha madarakani Rais Muhammad Bazoum.

Vinara wa mapinduzi ya kijeshi, Niger

Mkuu wa ujumbe wa ECOWAS ameongeza kwamba, Tiani amesema kuwa, kuachiliwa Bazoum kunawezekana iwapo makubaliano yatafikiwa, lakini hatarejeshwa madarakani.

Tiani pia amesisitiza katika mazungumzo hayo kuwa muda wa kipindi cha mpito ni miaka 3, na ametoa wito wa kufunguliwa mipaka iliyofungwa na kurejeshwa umeme nchini Niger kutoka nchi jirani ya Nigeria.