Nigeria yaahidi kupunguza vikwazo vya ECOWAS dhidi ya Niger
Msemaji wa ofisi ya rais wa Nigeria amesema nchi hiyo pamoja na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS zitapunguza baadhi ya vikwazo zilivyoiwekea Niger.
Ajuri Najilani, ametangaza kuwa, nchi hiyo na ECOWAS zitapunguza kadiri iwezekanavyo vikwazo zilivyoiwekea Niger ili kuepusha athari mbaya za vikwazo kwa raia wa nchi hiyo.
Najilani alitangaza pia siku ya Jumatatu kwamba hatua ya kijeshi dhidi ya Niger sio hatua inayofuata bali ni chaguo la mwisho.
Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS, alisema awali kwamba kuanzisha vita kamili katika bara la Afrika sio kwa maslahi ya nchi yake na nchi nyingine za eneo hilo.
Tinubu alitangaza kwa njia ya isiyo wazi utayarifu wa wanachama wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi kutumia machaguo yote dhidi ya Niger, lakini akasema ECOWAS inafanya juhudi ili kuupatia ufumbuzi wa amani mgogoro wa nchi hiyo.
ECOWAS imeiwekea vikwazo kadhaa Niger na kuashiria uwezekano wa kuingilia kijeshi katika nchi hiyo ili kumrudisha madarakani rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum.
Kwa shinikizo la Ufaransa na Marekani, jumuiya hiyo ya uchumi ya Magharibi mwa Afrika ilisimama dhidi ya Baraza la Kijeshi la Niger lililoshika madaraka ya nchi na kutangaza kuwa inajiandaa kuingilia kijeshi nchini humo ili kumrejesha Bazoum madarakani.
Hata hivyo, kamishna wa ECOWAS alitangaza Ijumaa ya wiki jana kwamba jumuiya hiyo haina mpango wa kuishambulia kijeshi Niger na itajaribu kutumia njia zote za amani ili kumrejesha Mohammed Bazoum madarakani.../