Sep 06, 2023 10:37 UTC
  • Waislamu Nigeria waadhimisha Arubaini ya Imam Hussein AS

Waislamu ya madhehebu ya Shia nchini Nigeria wamefanya marasimu, matembezi na vikao vya kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein (AS).

Kanali ya Press TV imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, maelfu ya watu wameshiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) katika mji wa Suleja, jimbo la Niger, kaskazini mwa Abuja, mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeongoza shughuli hizo za kumbukumbu ya Arubaini ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, aliyeuawa kidhulma katika jangwa la Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria.

Waombolezaji wametembea kilomita kadhaa licha ya jua kali katika mji huo, kuliadhimisha tukio hilo tukufu. Baadhi ya Waislamu wameweka moukib (mahema na vibanda) pembeni ya barabara za mji huo kwa ajili ya kugawa chakula na vinywaji.

Hussein Musa Barde, mwanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akizungumza na Press TV pambizoni mwa matembezi hayo amesema, wamekusanyika kwa wingi kwa ajili ya kuenzi mchango wa Imam Hussein AS katika Uislamu na kusimama kwake kidete dhidi ya dhulma.

Jeshi la polisi la Nigeria huko nyuma limekuwa likiwashambulia Waislamu wanaoshiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS na kuua shahidi na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.

Vikao na matembezi ya tukio la kila mwaka ambalo linaadhimisha siku ya 40 baada ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia yamefanyika leo katika pembe mbalimbali za dunia.

Nasif al-Khatabi, Gavana wa jiji la Karbala nchini Iraq amesema mji huo mtakatifu utapokea wafanyaziara zaidi ya milioni 30 katika Arubaini ya Imam Hussein AS ya mwaka huu.

Tags