Sep 17, 2023 04:37 UTC
  • Al-Shabaab ya Somalia yaitishia Marekani, yasema italipiza kisasi

Kiongozi mwandamizi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia ameionya Marekani kufuatia shambulizi la anga la hivi karibuni lililofanywa na ndege za kivita za US kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Mahad Karate amedai kuwa, Marekani ni kizingiti katika kupatikana uthabiti nchini Somalia, na kwamba Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) imekuwa ikiwalenga raia wasio na hatia katika hujuma zake nchini Somalia.

Karate amesisitiza kuwa, wanachama wa al-Shabaab watalipiza kisasi kwa shambulio la anga la Marekani la Septemba 6 katika eneo la el-Laheley karibu na mji bandari wa Kismaayo, mkoa wa Lower Juba. Amedai kuwa shambulio hilo liliua makamanda watatu wa al-Shabab na raia watano wakiwemo watoto wanne.

Kamanda huyo wa ngazi ya juu wa kundi la kigaidi la al-Shabaab ameongeza kuwa, "Tutalipiza kisasi cha mauaji ya watu wetu hata kama itachukua muda gani. Hii ni katika hali ambayo, kundi hilo la kitakfiri limekuwa likilenga pia raia katika hujuma zake za kigaidi. 

Kadhalika ripoti kadhaa za shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International zinaonesha kuwa, jeshi la Marekani linaendelea kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Aidha utafiti uliofanywa hivi karibuni na asasi isiyo ya kiserikali ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab, na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.

Tags