Sep 18, 2023 02:40 UTC
  • Kutiwa saini mkataba mpya wa usalama; Muungano wa kijeshi kati ya Mali, Niger na Burkina Faso

Baada ya kupita miezi kadhaa ya kushuhudiwa matukio ya kisiasa katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama Mali na Burkina Faso na kuundwa serikali za kijeshi katika nchi hizo; hivi sasa nchi tatu yaani Niger, Burkina Faso na Mali zimesaini mkataba wa pamoja wa usalama ulipewa jina la " Muungano wa Nchi za Sahel."

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za eneo la Sahel zimekuwa zikikabiliwa na harakati za makundi ya kigaidi kutokana na utajiri wao wa rasilimali, nafasi zao za kistratijia, kuwa kwao karibu na mipaka ya Libya sambamba na mabadiliko ya kisiasa na kijamii katika uga wa mfumo wa kimataifa. Kwa kadiri kwamba harakati za makundi hayo kwa muda sasa zimekuwa changamoto na daghadagha kuu kwa nchi za bara la Afrika. 

Makadirio yanaonyesha kuwa, kuna zaidi ya magaidi elfu 10 wa makundi mawili ya Daesh na al Qaida barani Afrika. Ni wazi kuwa, makundi ya kigaidi yanatumia nafasi ya kijiografia, ukubwa na utajiri wa Afrika kwa ajili yya kuttimiza malengo yao na yameligeuza bara hilo kuwa kituo cha kusajili na kutoa mafunzo kwa magaidi kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, umaskini na pia idadi kubwa ya vijana waliopo barani humo. 

Mengi  kati ya makundi hayo yamefanikiwa kuwashawishi na kutoa mafunzo kwa baadhi ya vijana ili kutekeleza hujuma za kigaidi  kwa kuwalipa kiasi kidogo cha pesa na kuwapa ahadi za kuboreshea hali yao ya maisha.

Makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika nchi za Kiafrika

Hali hii imezifanya nchi za Magharibi hususan Ufaransa kurasimisha uwepo wake kijeshi eneo la Sahel na kuendelea kujikita katika nchi za eneo hilo kwa kisingizio cha kusaidia mapambano dhidi ya hujuma za ugaidi na kudumisha amani na usalama katika nchi za eneo hilo; na kama alivyodai Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Ufaransa inataka kulifanya suala la kupambana dhidi ya ugaidi katika nchi za Sahel barani Afrika kuwa jukumu la Ulaya.

Licha ya madai hayo ya Rais wa Ufaransa, jeshi la nchi hiyo halikuwajibika ipasavyo katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika, bali limegonga mwamba katika uwanja huo. Kinyume chake jeshi hilo limetajwa kuhusika mara nyingi katika mauaji ya raia wa kawaida katika nchi kama Mali. Ushahidi wa wazi wa ukweli huu ni shambulio la anga lililohusishwa na vikosi vya jeshi la Ufaransa kwenye sherehe ya harusi huko Mali na kuua watu zaidi ya 100.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

Katika upande mwingine, kuendelea hali ya mchafukoge na hujuma za kigaidi katika nchi za Sahel barani Afrika, na wakati huo huo hatua ya Ufaransa ya kunufaika kisiasa na kiuchumi na maliasili tajiri za nchi hizo kutokana na kuwepo watawala vibaraka kumepelekea kushuhudiwa mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Mali, Niger na Burkina Faso kwenye miezi michache iliyopita. Wanajeshi waliofanya mapinduzi katika nchi hizo wanasema kuwa, wamefanya hivyo lengo lao likiwa ni kuyaangamiza makundi ya kigaidi na kukosoa utendaji wa nchi ajinabi kama Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi. Mapinduzi yote haya pia yameungwa mkono na wananchi wa kawaida. 

Hivi sasa nchi hizo tatu za Sahel zimesaini makubaliano ya pamoja ya usalama. Makubaliano hayo yanaweza kutathiminiwa katika pande mbili. Kwa upande wa ndani, kutiwa saini makubaliano hayo kutazikurubisha zaidi nchi hizo tatu na kuzidisha ushirikiano wa kiulinzi kati yao khususan hivi sasa ambapo Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imetishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya watawala wa Niger ili kumrejeshe madaraka Mohamed Bazoum, Rais aliyepinduliwa wa nchi hiyo. Katika uwanja huo, Mali na Burkina Faso zimetangaza rasmi kuwa shambulio lolote dhidi ya Niger ni sawa na kushambuliwa ardhi za nchi hizo na kwamba zitajibu mapigo. Katika upande mwingine, viongozi wa serikali huko Mali, Burkina Faso na Niger wametangaza kuwa nchi hizo zitalindana iwapo kutajiri uasi au uvamizi wowote kutoka nje. 

Rais wa Niger aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum 

Mota Muhammad Ali mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afrika ameashiria kuwa nchi hizo zinafanya juhudi kupunguza utegemezi wao kwa nchi za Magharibi na kusema: Nchi za Kiafrika zinafanya jitihada ili ziwe huru zaidi ikilinganishwa na siku za nyuma, ili zisitawaliwe na nchi za Magharibi. 

Lakini katika uga wa kikanda na kimataifa, makubaliano ya usalama yaliyofikiwa kati ya Mali, Burkina Faso na Niger yanahesabiwa kuwa ni katika juhudi za  kupambana na makundi ya kigaidi. Ripoti ya Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Afrika inaonyesha kuwa,  uingiliaji kati wa nchi ajinabi barani Afrika umepelekea kuongezeka kwa asilimia 70 idadi ya matukio ya mchafukoge na ukosefu wa amani yanayosababishwa na hujuma za makundi ya kigaidi katika nchi za Sahel. Meja Jenerali Said Chengriha Mkuu wa Majeshi wa Algeria anasema: Uzoefu unaonyesha kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi wa nchi ajinabi katika eneo la Sahel umeshindwa kikamilifu.  

Suala hili limetoa msukumo kwa nchi za eneo la Sahel kufanya kila ziwezalo ili kuimarisha ushirikiano baina  katika vita dhidi ya ugaidi. Aidha muungano huo wa kijeshi wa nchi tatu  unaweza kutathminiwa katika uwanja huo, na inaonekana kuwa katika siku zijazo utapanuka na kuimarika zaidi. 

Tags