Jun 29, 2016 13:23 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano kati ya jeshi na waasi Sudan Kusini

Makumi ya watu wameuawa katika wimbi jipya la mapigano kati ya askari wa jeshi la serikali na waasi katika mji wa Wau nchini Sudan Kusini.

Taarifa ya serikali ya Juba imesema kuwa, watu 43 wameuawa katika mapigano hayo ya wiki jana katika mji wa Wau, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Makuei Lueth, msemaji wa serikali ya Sudan Kusini amesema watu 39 miongoni mwa waliouawa ni raia na askari polisi wanne. Amekariri kuwa Sudan ndiyo inayounga mkono harakati za makundi ya waasi kuzusha mapigano na machafuko katika nchi hiyo jirani yake, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa vikali na serikali ya Khartoum. Jumamosi iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alitoa taarifa akilaani mapigano yaliyozuka upya huko Sudan Kusini na kuzitaka pande zinazopigana kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa shabaha ya kutatua hitilafu zao.

Sudan Kusini imekumbwa na mzozo wa ndani tangu mwezi Disemba mwaka 2013. Mwezi Agosti mwaka jana, serikali ya Sudan Kusini na waasi walisaini makubaliano ya amani na kusimamisha mapigano, hata hivyo pande hizi zimekuwa zikikiuka makubaliano hayo mara kwa mara.

Tags