Sep 19, 2023 13:23 UTC
  • Baraza Kuu la UN kujadili mgogoro wa Sudan kesho Jumatano

Jumatano wiki hii Septemba 20, kutakuwa na kikao maalumu kandoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kukusanya misaada na kuonesha uungaji mkono kwa watu wa Sudan.

Tukio hilo linakuja wakati ambapo mapigano makali yanayoendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mwishoni mwa wiki yamesababisha vifo vya raia.

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya UN, OCHA imesema, “Wadau wetu wa masuala ya kibinadamu pia wanatuambia kuwa mapigano mapya huko Darfur Kusini yamewakosesha makazi watu wengi katika jiji la Nyala.”

Watu wanaendelea kuyahama maeneo yao, huku zaidi ya milioni 5.1 wakiwa tayari wamekimbia makazi yao tangu katikati ya Aprili. Watu milioni 4.1 wamekuwa wakimbizi ndani ya Sudan na zaidi ya milioni 1 wamelazimika kutafuta hifadhi nje ya nchi.

Waandishi wa habari wameambiwa, “familia mpya zilizokimbia makazi zinawasili katika maeneo ambayo tayari yalikuwa yanakabiliwa na changamoto kutokana na vurugu.”

OCHA inasema tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, takribani watoto 435 wameripotiwa kuuawa na wengine 500 wamekufa kutokana na njaa - ingawa idadi ya kweli inaweza kuwa kubwa zaidi.

Mpango wa misaada ya kibinadamu wa dola bilioni 2.6 kwa Sudan, ambao unalenga kusaidia watu milioni 18, hadi sasa umefadhiliwa kwa asilimia 25 tu.

Tags