Sep 22, 2023 02:41 UTC
  • Jeshi la Ethiopia lasema limeua magaidi 462 wa al-Shabaab Somalia

Kwa akali wanachama 462 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waliuawa mwisho mwa wiki nchini Somalia, Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (ENDF) limethibisha hayo na kueleza kuwa, magaidi hao waliuawa katika shambulizi lililotibuliwa katika kambi ya askari wa Ethiopia wanaohudumu chini ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS).

Kwa mujibu wa jeshi la Ethiopia, makabliano baina yake na wanamgambo wa al-Shabaab lilitokea katika mji wa Rabdhure, kusini magharibi mwa Somalia, ambapo wanamgambo hao walikuwa wamepanga kuishambulia kambi hiyo ya jeshi la Ethiopia kwa kutumia magaidi 12 waliojifunga mabomu.

Taarifa ya jeshi la Ethiopia imesema askari hao wanaohudumu chini ya mwavuli wa ATMIS walitoa kipigo kikali dhidi ya magaidi wa al-Shabaab na kuua 462 miongoni mwao.

Haya yanajiri siku chache baada ya duru za habari za kundi la kigaidi la al-Shabaab kutangaza kuwa, genge hilo limewauwa wanajeshi 178 wa Ethiopia huko magharibi mwa Somalia. Aidha kundi hilo lilidai kuwa limewatia nguvuni wanajeshi wengine wa Ethiopia na kudai kuwa jeshi la Ethiopia limeshindwa kusonga mbele. Kadhalika magaidi wa al-Shabaab walidai kuharibu zana na silaha za wanajeshi wa Ethiopia katika hujuma hiyo ya kigaidi.

Maiti za magaidi wa al-Shabaab

Hata hivyo Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (ENDF) limekadhibisha madai hayo ya al-Shabaab na kuyataja kuwa ya uongo na kipropaganda. Limesema karibuni hivi litatoa ripoti kamili itakayoakisi uhalisia wa mambo kuhusiana na tukio hilo.

Haya yanajiri wakati huu ambapo Umoja wa Afrika unaendelea na awamu ya pili ya kuondoa wanajeshi wa umoja huo kutoka Somalia. Mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja liliidhinisha kikosi cha ATMIS kuwasaidia Wasomali hadi majeshi yao yatakapopata nguvu na kuwajibika kikamilifu kwa usalama wa nchi hiyo, hadi mwishoni mwa mwaka ujao 2024.

Tags