Sep 23, 2023 07:42 UTC
  • Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 27 wa al-Shabaab Galmudug

Jeshi la Somalia limetangaza habari ya kuangamiza makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika jimbo la Galmudug, katikati mwa nchi.

Taarifa ya jana Ijumaa ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) imesema: Zaidi ya  Makhawarij (wanamgambo wa al-Shabaab) 27 wameuawa katika operesheni ya Jeshi la Taifa la Somalia.

Wizara ya Ulinzi ya Somalia imeeleza kuwa, operesheni hiyo ilifanyika katika vijiji vya Balal-Dheer, El-Gambar, na Mililiqo katika jimbo hilo la katikati mwa nchi la Galmudug. 

Habari zaidi zinasema kuwa, ngome tatu za al-Shabaab zimeshambuliwa na kuharibiwa kikamilifu kwenye operesheni hiyo, pamoja na magari na silaha za kijeshi zilizokuwa zinatumiwa na magaidi hao wakufurishaji.

Maiti za magaidi wa al-Shabaab

Haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (ENDF) kusema kuwa limeua wanachama 462 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika mji wa Rabdhure, kusini magharibi mwa Somalia. Hii ni baada ya baada ya kundi hilo la kigaidi  kudai kuwa limewauwa wanajeshi 178 wa Ethiopia huko magharibi mwa Somalia. 

Operesheni hizo dhidi ya al-Shabaab zimeshtadi wakati huu ambapo Umoja wa Afrika unaendelea na awamu ya pili ya kuondoa wanajeshi wa umoja huo (ATMIS) kutoka nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags