Kiongozi wa upinzani nchini DRC, Fayulu, amethibitisha kuwa atawania kiti cha urais
(last modified Sun, 01 Oct 2023 07:14:04 GMT )
Oct 01, 2023 07:14 UTC
  • Martin Fayulu
    Martin Fayulu

Kiongozi mwandamizi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Martin Fayulu, alithibitisha jana Jumamosi mjini Kinshasa kwamba atagombea katika uchaguzi wa rais wa Desemba 20.

"Muungano wa Lamuka ("Amka", kwa Kilingala) umeamua nigombee urais," Fayulu amewaambia waandishi wa habari.

"Tutaendelea kupigania uwazi katika uchaguzi. Hatukupata fursa ya kukagua daftari la wapiga kura lakini tutakuwa macho wakati wa upigaji kura", aliongeza mpinzani huyo ambaye anasema ushindi wake uliibwa wakati wa uchaguzi wa rais wa Desemba 2018 ambapo Tshisekedi alitangazwa mshinidi.

Kufikia Julai 2022, chama chake cha Ecidé (Ushiriki wa Raia na Maendeleo), ambacho ni cha muungano wa Lamuka, kilikuwa kimemtangaza Martin Fayulu kuwa mgombea wake rasmi katika uchaguzi ujao wa rais.

Fayulu anadai kuwa kati ya wapigakura milioni 43.9 waliojiandikisha, kutakuwa na "kura milioni 10 bandia". Amesema safari hii hakutakuwa na wizi wa kura kwani watajipanga kukabiliana na jaribio lolote la kutumia wapiga kura bandia.

Fayulu anasisitiza kwamba kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi wa urais 2018, ambapo aliibuka wa pili. 

Rais wa DRC Félix-Antoine Tshisekedi

Chama cha Fayulu cha Ushiriki wa Raia na Maendeleo, ambacho ni sehemu ya Muungano Lamuka, kinasema orodha ya wapiga kura sio sahihi na kwa sasa kimekataa kushiriki chaguzi za ubunge, mikoa na mitaa.

Chama hicho kinadai kuwa kati ya wapiga kura milioni 43.9 kwenye orodha ya wapiga kura, baadhi ya milioni 10 ni "wa kubuni".

Hivi karibuni   Rais wa DRC Félix-Antoine Tshisekedi akihutubu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alisema uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.

Tags