Oct 05, 2023 03:16 UTC
  • Tunisia yakataa msaada wa kifedha wa Umoja wa Ulaya

Rais Kais Saied wa Tunisia amekataa kupokea msaada wa kifedha wa Umoja wa Ulaya (EU) uliokusudia kupiga jeki bajeti ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, sanjari na kuisaidia kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Tunisia TAP, Rais Saied amesema taifa hilo halina haja na msaada huo wa kifedha kutoka Ulaya, kwa kuwa EU ilikiuka makubaliano ya pande mbili yaliyosainiwa miezi michache iliyopita.

Rais wa Kais Saied amesema, "Tunisia inapinga tangazo la EU, si kwa kuwa fedha zilizotangazwa ni chache, lakini kwa kuwa pendekezo lililotolewa linakwenda kinyume na hati ya maelewano iliyosainiwa mwezi Juni."

Amesema Tunisia ipo tayari kwa ushirikiano, lakini haitakubali kupokea kitu kinachofanana na fedha chache sadaka kwa kuwa huko ni kukoseana heshima.

Mwezi Juni mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulitangaza azma ya kuipa Tunisia Yuro milioni 105 kwa madai ya kusaidia kukabiliana na ongezeko kubwa la wahamiaji, kukuza uchumi wake uliodorora na kuokoa fedha za serikali. EU hapo awali iliahidi kuwa itaipa Tunisia zaidi ya Yuro bilioni moja.

Wahamiaji Tunisia

Aidha familia za wanasiasa wa upinzani nchini Tunisia waliofungwa jela, waliuponda vibaya msaada uliotolewa kwa Tunis na Umoja wa Ulaya na kusema kuwa, mpango huo umetokana na mtazamo potofu na usio na tija. 

Kadhalika walionya kuwa, fedha hizo hazitoisaidia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kusitisha uhamiaji haramu. Rais Kais Saied wa Tunisia alisema hivi karibuni kuwa, nchi hiyo haitokubali kufanywa mlinzi wa mipaka ya nchi za Ulaya, wakati huu ambapo safari za wahamiaji haramu kwenda Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania zikiwa zimeongezeka.

 

Tags