Sudan: Kuongezwa muda vikosi vya UNAMID ni mkinzano
Kwa mara nyingine tena serikali ya Sudan imekosoa vikali hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza muda wa kuhudumu vikosi vya kimataifa vya kusimamia amani huko Daruf UNAMID kwa mwaka mmoja zaidi.
Omer Dahab, mjumbe wa Sudan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema hatua ya kuongezewa muda wa mwaka mmoja vikosi hivyo ni mkinzano wa moja wa moja usiozingatia matakwa ya serikali ya Khartoum. Amesema hatua hiyo inakiuka makubaliano ya pande tatu kati ya Sudan, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ya kuanza kuondolewa vikosi hivyo vyenye askari 20,000 kutoka nchi 30 duniani nchini Sudan mwaka jana 2015, huku akipuuzilia mbali ripoti ya UN kuwa hali bado sio shwari katika jimbo la Darfur.
Ripoti ya pamoja ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa ilitoa wito wa kuviongezea vikosi hivyo vya kimataifa vya kusimamia amani muda mwingine wa mwaka mmoja, kuanzia jana Juni 30 hadi Juni 30 mwaka ujao wa 2017, azimio ambalo lilipasishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana. Vikosi vya pamoja vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa UNAMID vilitumwa huko Darfur mwaka 2007 kwa lengo la kulinda raia na kurudisha utulivu katika eneo hilo.