Waliouawa katika mapigano ya hivi karibuni S/Kusini waongezeka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10366-waliouawa_katika_mapigano_ya_hivi_karibuni_s_kusini_waongezeka
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya hivi karibuni nchini humo imeongezeka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2016 10:47 UTC
  • Waliouawa katika mapigano ya hivi karibuni S/Kusini waongezeka

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya hivi karibuni nchini humo imeongezeka.

Michael Makuei amesema kuwa, idadi ya wahanga wa mapigano ya hivi majuzi kati ya vikosi vya serikali na makundi yanayobeba silaha katika mji wa Wau kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini inazidi kuongezeka na kwamba vyombo husika vimeanzisha uchunguzi ili kutambua watu waliouliwa katika mashambulizi hayo.

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema hadi kufikia sasa watu wasiopungua 43 wameshauawa na kwamba serikali imeunda kamati ya ngazi ya juu ya watu wanane inayoongozwa na Waziri wa Afya wa Sudan Kusini ili kuchunguza hali ya kibinadamu katika mji wa Wau na kisha kuwasilisha matokeo ya uchunguzi huo kwa serikali.

Mapigano hayo yalianza hivi karibuni baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kumuuzulu Gavana wa mji wa Wau. Hatua hiyo iliyakasirisha baadhi ya makundi katika eneo hilo, suala lililozusha mapigano hayo.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya kimataifa yametangaza kuwa karibu watu elfu 12 wakazi wa Wau wamekimbilia katika vituo vya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye mji huo kwa ajili ya kutafuta hifadhi; huku maelfu ya wengine pia wakipata hifadhi katika kambi za wakimbizi katika maeneo ya vijijini.