Maandamano dhidi ya Wazayuni yashtadi, Israel yafunga balozi zake Rabat, Cairo
Maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, yameilazimisha Tel Aviv kuwahimisha wafanyakazi wa balozi zake katika nchi za Misri na Morocco.
Maandamano hayo yamechachamaa katika kona zote za dunia hasa baada ya mauaji ya makusudi ya Israel katika shambulizi lake la kinyama dhidi ya Hospitali ya al-Mamaadani ambayo ndani yake kulikuweko wagonjwa na majeruhi waliokuwa wameomba hifadhi katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza habari ya kuwaondoa wanadiplomasia na wafanyakazi wa balozi zake katika miji ya Rabat na Cairo ikihofia kuwa watashambuliwa na wananchi wa nchi hizo za Kiarabu wenye hasira.
Hapo jana, maelfu ya wanachuo wa vyuo vikuu mbalimbali vya Morocco walifanya maandamano makubwa na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina hususan mashahidi wa Gaza.
Zaidi ya vyuo vikuu 30 vya Morocco vilifungwa na kutoendesha shughuli za masomo kwa ajili ya kutangaza himaya, uungaji mkono na mshikamano na watu wa Palestina hususan mashahidi wa Ukanda wa Gaza.
Kwa upande mwingine, ofisi ya rais wa Algeria pia imelaani kile ilichokiita "mashambulizi ya makusudi ya vikosi vinavyoikalia kwa mabavu Palestina dhidi ya hospitali ya Gaza".
Jamii ya kimataifa imeendelea kupaza sauti za kulaani shambulizi la anga la Israel katika Hospitali ya al-Maamadani katikati ya Gaza lililoua zaidi ya watu 500 na kuwajeruhi zaidi ya 1,000 wengine. Maandamano ya kulaani jinai hizo yameshuhudiwa pia nchini Iran, Afrika Kusini, Uturuki, Lebanon, Jordan, Syria, Kuwait na hata katika nchi za Magharibi kama Uingereza na Ujerumani.