Waziri Araghchi yupo Misri kujadili Gaza, uhusiano wa Tehran-Cairo
(last modified Mon, 02 Jun 2025 06:46:52 GMT )
Jun 02, 2025 06:46 UTC
  • Waziri Araghchi yupo Misri kujadili Gaza, uhusiano wa Tehran-Cairo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi yuko katika mji mkuu wa Misri, Cairo, kwa ajili ya kufanya mazungumzo na maafisa wakuu wa nchi hiyo, juu ya uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri pamoja na maendeleo katika eneo la Asia Magharibi, yakiwemo mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA, Waziri Araghchi aliwasili mjini Cairo Jumapili usiku. Anatazamiwa kukutana na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri, na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Badr Abdelatty.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, majadiliano hayo yatahusu uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Cairo, pamoja na matukio ya kimataifa na kieneo, hususan vita vya Gaza ambako Israel inaendeleza jinai dhidi ya Wapalestina.

Viongozi wa nchi mbili hizi wamekuwa wakisisitiza juu ya ulazima wa kukomeshwa mara moja hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na uchokozi na uvamizi wa Israel dhidi ya Lebanon na Syria.

Kadhalika maafisa wakuu wa Iran na Misri mara kwa mara wamekuwa wakisisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Cairo katika nyuga mbali mbali.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri Badr Abdul Ati, walijadili maendeleo ya kikanda na mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Walisisitiza kuwa kuna haja ya kukomeshwa mashambulizi ya utawla wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Baada ya kuitembelea Misri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameratibiwa kuzuru Lebanon.