Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya fremu ya vikwazo kwa Niger
-
Josep Borrell
Umoja wa Ulaya umepitisha mfumo wa kuwawekea vikwazo viongozi wa serikali ya kijeshi iliyochukua mamlaka ya uongozi huko Niger mwezi Julai mwaka huu.
Baraza la Umoja wa Ulaya limeeleza kuwa, fremu hiyo inauruhusu Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo shakhsia na vyombo vyote vilivyohusika na vitendo vya kutishia amani, utulivu na usalama wa Niger, kudhoofisha mfumo wa katiba, demokrasia, utawala wa sheria, au kukiuka haki za binadamu n.k huko Niger.
Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo ulilaani tangu awali mapinduzi ya kijeshi yaliyojiri huko Niger. "Kwa uamuzi huu tuliofikia, Umoja wa Ulaya unaimarisha uungaji mkono wake kwa jitihada za ECOWAS na kutuma ujumbe wa wazi kwa wafanyamapinduzi kwamba: Mapinduzi ya kijeshi huambatana na gharama," amesema Borell.
Mapema mwezi Julai mwaka huu kundi la wanajeshi nchini Niger, wakiongozwa na Kanali Amadou Abdramane, walichukua udhibiti wa nchi na kutangaza kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum, kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Tangu wakati huo jamii ya kimataifa imeeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya mambo nchini Niger na kutaka kurejeshwa utawala halali wa kidemokrasia nchini humo. Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeiwekea vikwazo Niger na kutishia kutumia nguvu dhidi ya wanajeshi wafanya mapinduzi.