26 wauawa katika shambulizi la magaidi Oicha, mashariki ya DRC
(last modified Tue, 24 Oct 2023 13:54:02 GMT )
Oct 24, 2023 13:54 UTC
  • 26 wauawa katika shambulizi la magaidi Oicha, mashariki ya DRC

Genge moja linaloaminika kuwa la kigaidi limefanya mashambulizi na kuua makumi ya watu katika mji wa Oicha, mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Meya wa Oicha, Nicolas Kikuku amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, waliofanya mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo ni waasi wa kundi la ADF.

Kikuku ameeleza kuwa, mbali na watu 26 kuuawa katika shambulizi hilo la jana usiku, wengine kadhaa wamejeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali ya mji huo ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Haya yanajiri siku chache baada ya mapigano makali kushuhudiwa kati ya waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makundi mengine ya waasi katika Wilaya ya Masisi jimboni Kivu Kaskazini.

Aidha shambulio hilo limekuja wiki chache baada ya Jeshi la Uganda na lile la DRC kukubaliana kuendelea na operesheni dhidi ya waasi hao wa Allied Democratic Forces (ADF) kwa miezi mingine minne. Operesheni hiyo ilianza Desemba 2021 na ilitarajiwa kudumu kwa miezi 6 pekee.

Ramani ya DRC inayoonesha mkoa wa Kivu Kaskazini

Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha harakati zao kwenye misitu mashariki mwa Kongo DR kwa zaidi ya miongo miwili sasa, na wamekuwa wakifanya mashambulizi ndani ya nchi hiyo na wakati mwingine ndani ya ardhi ya Uganda.

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limelitangaza kundi la ADF kuwa ni tawi lake katika eneo la Afrika ya Kati. Jeshi la Uganda UPDF kwa kushirikiana na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likipambana na makundi ya wabeba silaha kwa karibu miaka miwili sasa.

Tags