Mahakama ya Juu Nigeria yatupa rufaa za kupinga ushindi wa Rais Tinubu
-
Bola Tinubu
Mahakama ya Juu ya Nigeria imetupilia mbali rufaa zilizowasilishwa kwake na vyama vya upinzani kupinga ushindi wa Rais Bola Tinubu katika uchaguzi tata wa rais wa mwezi Februari mwaka huu.
Rufaa hizo ziliwasilishwa mahamani hapo na wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais, Atiku Abubakar wa chama cha People's Democratic Party na Peter Obi wa Chama cha Leba.
Wanasiasa hao waliwasilisha mahakamani kesi ya kutaka uchaguzi ufutwe kwa madai ya wizi wa kura na mawakala kushindwa kuchapisha matokeo ya uchaguzi kupitia mtandao.
Awali walikuwa wamewasilisha mafaili yao katika Mahakama ya Rufaa za Uchaguzi, ambayo mwezi uliopita ilibariki ushindi wa Tinubu mwenye umri wa miaka 71.
Bola Ahmed Tinubu aliapishwa Mei mwaka huu kuwa Rais wa tano wa Nigeria tokea kurejea kwa utawala wa demokrasia nchini humo mwaka 1999; huku akikabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kiusalama.
Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) ilimtangaza Tinubu aliyegombea uchaguzi wa urais uliofanyika Februari mwaka huu kupitia chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kuwa mshindi wa uchaguzi urais, kwa kupata kura milioni 8.8.
Kwa mujibu watume hiyo, Tinubu alifuatiwa na mshindani wake wa karibu Atiku Abubakar wa chama cha Peoples Democratic Party (PDP) aliyepata kura milioni 6.9 (29% ya kura) huku Obi akiambulia asilimia 25.