Nov 07, 2023 13:22 UTC
  • Wanafunzi 13 wauawa wakisherehekea Maulidi Nigeria

Kwa akali wanafunzi 13 wa madrasa ya Kiislamu wameuawa katika shambulizi la wabeba silaha katika jimbo la Katsina, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hayo yamesemwa leo Jumanne na Habibu Abdulkadir, mratibu wa kisiasa katika Wilaya ya Musawa ambaye ameeleza kuwa, wanafunzi hao wameuawa na genge la watu waliokuwa wamejizatiti wa silaha wakiwa katika sherehe za Maulidi ya Mtume Muhammad SAW.

Ameeleza kuwa, genge hilo lilivamia kijiji cha Kusa katikati ya jimbo la Katsina Jumapili iliyopita, na kuanza kuwamininia risasi wanafunzi hao, ambapo 13 miongoni mwao wameuawa, mbali na wengine zadi ya 20 kujeruhiwa.

Afisa huyo wa serikali za mitaa katika Wilaya ya Muswada amesema wahalifu hao walishambuliwa na wanakijiji waliojitolea kuwasaidia maafisa usalama kulinda doria baada ya kutekeleza shambulizi hilo, na hivyo kuwazuia kuwateka nyara wanafunzi wengine.

Jimbi la Katsina limekuwa likishuhudia hujuma za wabeba silaha wanaolenga wanafunzi

Magenge hayo yenye maficho katika majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna, na Niger yamekuwa yakishambulia vijiji na kuteka nyara wanafunzi, kufanya mauaji, uporaji na kuchoma moto nyumba za wanavijiji katika majimbo hayo. 

Hivi karibuni, wanafunzi kadhaa walitekwa nyara kaskazini magharibi mwa Nigeria katika jimbo la Kaduna ambako magenge ya wahalifu awali yaliwateka watoto kadhaa kwa ajili ya kudai kikomboleo.

Aghalabu ya magenge hayo yana mfungamano na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon.

Tags