Nov 12, 2023 12:29 UTC
  • Waalgeria wasusia bidhaa za Ufaransa wakiwatetea Wapalestina

Uhalifu na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza kwa msaada wa nchi za Magharibi zimewafanya wananchi katika nchi mbalimbali wasusie bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Ulaya na Marekani.

Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) limeripoti kuwa, kampeni ya kususia bidhaa zenye chapa za mashirika na makampuni yanayouunga mkono na kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel imeshika kasi kubwa nchini Algeria kiasi kwamba, hakuna vinywaji vya kigeni katika maduka na migahawa ya Algiers, mji mkuu wa nchi hiyo, na katika soko la vipodozi. Wafanyabiashara wa Algiers wanasema, watu wamesusia kabisa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka Ufaransa. 

Abdelkader Jannadi, mtaalamu wa masuala ya uchumi wa Algeria anasema kuwa, mafanikio ya kampeni za kususia bidhaa zenye chapa za makampuni ya Ufaransa yanayouunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kuwatetea Wapalestina na kusimamisha mchakato wowote wa mapatano na utawala katili wa Israel ni fursa kwa Algeria kuboresha ustawi wa uzalishaji wa ndani na kupunguza bei ya bidhaa mbalimbali.

Algeria imekuwa miongoni mwa watetezi wakubwa wa haki za taifa linalodhulumiwa la Palestina na imekuwa ikiunga mkono kadhia ya Quds kwa njia mbalimbali.

Waalgeria wanaiolaumu Ufaransa kwamba inaunga mkono uhalifu wa Israel Ukanda wa Gaza.

Mapema mwezi huu wa Novemba, Bunge la Algeria lilipasisha sheria ambayo inamruhusu Rais wa nchi, kama ikilazimu, kuingia vitani na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuwatetea wananchi wasio na hatia wa Palestina.

Bunge la Algeria lilipasisha sheria hiyo kwa kura za 100% na hivyo kumruhusu rais wa nchi hiyo kuingia vitani na utawala wa Kizayuni ikibidi kwa minajili ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina.

Algeria pia imetangaza kusitisha shughuli zote za michezo na za kitamaduni zinazofadhiliwa na serikali ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao sasa wanakabiliwa na mashambulizi ya anga na mzingiro wa Israel.

Tags