Wananchi wa Kano Nigeria waandamana kulaani jinai za Israel Ukanda wa Gaza
Maelfu ya Waislamu na waungaji mkono wa Palestina katika mji wa Kano, Nigeria wameandamana na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iranpress, jana jioni watu, wanazuoni wa Kiislamu wa Kisunni na Kishia, wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya wanasiasa wa Nigeria walishiriki katika maandamano ya kupinga utawala wa Kizayuni katika mji Kano, Nigeria.
Waandamanaji hao wamesisitiza juu ya ulazima wa kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.
Washiriki wa maandamano hayo dhidi ya Wazayuni walishika mabango mikononi mwao yaliyosomeka: "Serikali ya Nigeria lazima ikate uhusiano na utawala wa Israel," "Kano inasimama na Palestina," "Mauti kwa Israel," na "Sisi sote ni Wapalestina." ".
Vijana wa Nigeria katika mji wa Kano pia waliimba kwa umaridadi na kwa pamoja wimbo mashuhuri wa "Salaam Farmandeh" katika maandamano ya kuunga mkono muqawama wa Palestina na watu madhulumu wa Gaza.
Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakiandamana kila mara na kusisitiza uungaji mkono wao mkubwa kwa wananchi wa Palestina na muqawama wao dhidi ya uvamizi wa Israel na jinai zake.
Wiki iliyopita pia, Waislamu katika Jimbo la Bauchi la Nigeria walifanya maandamano wakipeperusha bendera za Palestina huku wakitoa nara za "Tunaunga mkono Hamas," "Tunaunga mkono Palestina," "Mauti kwa Israel na Mauti kwa Marekani".