Nov 15, 2023 14:56 UTC
  • Mahakama: Ni kinyume cha sheria kwa UK kuwapeleka Rwanda watafuta hifadhi

Mahakama ya Juu ya Uingereza imesema mpango wa serikali ya London wa kuwapeleka nchini Rwanda wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo unakiuka sheria.

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo leo Jumatano ikisisitiza kuwa, mpango huo unawaweka katika hali hatarishi wakimbizi hao, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao waliikimbia nchi yao ya Rwanda na kuwarejesha huko ni kuwaweka hatarini.

Uamuzi huo ni pigo kwa mpango wa serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak wa kutekeleza sera tatanishi na yenye kuchupa mipaka dhidi ya wahamiaji.

Uamuzi wa leo umekuja baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufaa iliyosema pia kuwa mpango wa kuwatuma waomba hifadhi nchini Rwanda ni kinyume cha sheria.

Majaji wote watano katika Mahakama ya Juu ya Uingereza wametoa uamuzi wao kuhusu pingamizi hilo leo Jumatano, na sasa Waziri Mkuu Rishi Sunak atakuwa chini ya mashinikizo kutoka chama chake ambacho kinataka nchi hiyo ijiondoe kwenye Mkataba wa Ulaya kuhusu haki za binadamu, ECHR.

Mahakama ya Rufaa pia ilisema kupelekwa wahamiaji walioko Uingereza nchini Rwanda kunakiuka kifungu cha 3 cha Mkataba wa Ulaya wa haki za binadamu, unaokataza mateso na unyanyasaji au udhalilishaji.

Mpango huo wa serikali ya Uingereza umekuwa ukipingwa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, wanaosema Rwanda haiwezi kuwa nchi salama kwa wakimbizi na wahamiaji hao.

Tags