Visa vya utesaji watu Burundi vyaitia hofu UN, yataka hatua zichukuliwe
(last modified Sun, 26 Nov 2023 02:24:01 GMT )
Nov 26, 2023 02:24 UTC
  • Visa vya utesaji watu Burundi vyaitia hofu UN, yataka hatua zichukuliwe

Kamati ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu dhidi ya Utesaji, CAT imetamatisha kikao chake cha 78 mjini Geneva, Uswisi kwa kutoa mahitimisho ya ripoti za mataifa sita ikiwemo Burundi ambayo inaonesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Mateso na adhabu za kikatili zisizoheshimu utu.

Taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR imemnukuu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Claude Heller, akisema kamati imeshtushwa na madai ya kuaminika ya unyanyasaji, kuteswa, kunyongwa bila haki na watu kutoweshwa nchini Burundi tangu mzozo wa kisiasa wa 2015.

Halikadhalika imeshangazwa na ripoti zinazoendelea kutolewa za mauaji ya kiholela yanayoripotiwa kufanywa na askari wa vikosi vya usalama, vikosi vya jeshi, Ofisi ya Usalama wa Taifa, na tawi la vijana la chama tawala lijulikanalo kama Imbonerakure. 

Kamati hiyo pia imeonesha wasiwasi mkubwa juu ya madai ya mateso na utesaji unaofanywa na makundi hayo hasa katika majengo ya Huduma ya Taifa ya Ujasusi karibu na kanisa kuu la mji mkuu wa kibiashara Bujumbura, vituo vya polisi, magereza, na vituo vingine vya kuwekea watu kizuizini.

Waandishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mateso wakihutubia waandishi wa habari 

“Serikali iwe na udhibiti mkali dhidi ya polisi na vikosi vya usalama ili kuzuia mauaji ya kiholela, kuchunguza tuhuma zote za mauaji ya kiholela, na kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu wale waliohusika,” amesema Bi. Heller.

CAT imeitaka serikali ya Burundi ichunguze kila kesi ya madai ya mateso au utesaji kwa kutumia chombo kisichoegemea upande wowowte huku ikiiomba pia serikali hiyo ihakikishe kuwa washukiwa, ikiwa ni pamoja na wale walio katika nafasi za uongozi, wanafikishwa mahakamani ipasavyo na ikiwa watapatikana na hatia, wapewe adhabu inayofaa kulingana na uzito wa kosa.

Nchi zingine zilizohusihwa kwenye ripoti hiyo ya Kamati ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu dhidi ya Utesaji, CAT ni Costa Rica, Denmark, Kiribati, Misri na Slovenia.../