Miili mingine ya walioaga dunia katika ajali ya EgyptAir yapatikana
Mabaki mengine ya viwiliwili vya watu waliofariki dunia kwenye ajali ya ndege ya abiria ya shirika la ndege la EgyptAir la Misri yamepatikana katika Bahari ya Mediterania.
Kamati ya uchunguzi wa ajali hiyo imesema miili ya abiria wote katika ajali hiyo imeopolewa kufikia sasa na imepelekwa katika bandari ya Alexandria kwa ajili ya kuchunguzwa kabla ya kupelekwa Cairo kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba DNA. Hata hivyo kamati hiyo imesema haiwezi kwa sasa kujua idadi kamili ya miili iliyoopolewa kutokana na kuoza.
Afisa wa kamati ya uchunguzi wa ajali hiyo hivi karibuni alitangaza kuwa mabaki ya viwiliwili vya watu waliofariki kwenye ajali hiyo unaonesha kuwa ulitokea mripuko ndani ya ndege hiyo kabla ya kuanguka katika Bahari ya Mediterania.
Mei 19, Ndege aina ya Airbus A320 ya shirika la ndege la Misri ilianguka katika Bahari ya Mediterania wakati ikitokea Paris, Ufaransa kuelekea Cairo, Misri ikiwa na jumla ya wasafiri 66. Watu wote waliokuwamo ndani yake walifariki dunia.