Dec 30, 2023 11:16 UTC
  • Waniger washerehekea kufikia tamati uwepo wa askari wa Ufaransa nchini humo+VIDEO

Wananchi wa matabaka mbalimbali nchini Niger wamefanya sherehe maalumu ya kufurahia kufikia tamati uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, wananchi wa Niger jana Ijumaa walikusanyika katika mji mkuu Niamey, kusherehekea kufikia tamati uwepo wa askari wa Ufaransa nchini humo.

Makamanda waandamizi wa jeshi la Niger waliungana na wananchi katika sherehe hizo zilizofanyika katika kambi ya kijeshi ya Kikosi cha 110 cha Jeshi la Niger mjini Niamaye.

Washiriki wa mkusanyiko huo mjini Niamey wamenukuliwa na shirika la habari la Iran Press wakisema kuwa, kuondoka wanajeshi wote vamizi wa Ufaransa nchini humo si ushindi tu kwa Niger, bali ni ushindi mkubwa kwa bara zima la Afrika.

Kuondoka kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa kulifanyika Ijumaa iliyopita katika hafla iliyohudhuriwa na makamanda wakuu wa jeshi la Niger katika Kituo cha Anga cha 110 mjini Niamey. 

Kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Niger kumefanyika wakati vikosi vya nchi hiyo ya Magharibi vimekuwepo moja kwa moja au njia isiyo ya moja kwa moja na kwa miongo kadhaa katika nchi mbalimbali za Afrika, hasa za eneo la Sahel.

Kufuatia mashinikizo makubwa yaliyotolewa na serikali mpya za Mali, Burkina Faso na sasa Niger, serikali ya Ufaransa hatimaye imelazimika kuwaondoa askari wake wote katika nchi za eneo la Sahel.

 

Tags