Hali tete DRC; Matokeo ya uchaguzi wa rais kutangazwa leo
(last modified Sun, 31 Dec 2023 03:06:27 GMT )
Dec 31, 2023 03:06 UTC
  • Hali tete DRC; Matokeo ya uchaguzi wa rais kutangazwa leo

Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) inatazamiwa kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo leo Jumapili, na hali ya taharuki imetanda huku jamii ya kimataifa ikiwa na wasi wasi wa kuibuka machafuko ya baada ya uchaguzi nchini humo.

Mwenyekiti wa CENI, Denis Kadima amethibitisha kuwa matokeo rasmi na ya mwisho ya uchaguzi huo yatatangazwa leo Jumapili, huku Rais aliyeko madarakani Félix Tshisekedi akitazamiwa kupata ushindi mkubwa.

Matokeo hayo yanatazamiwa kutangazwa katika hali ambayo,  serikali ya DRC imetupilia mbali wito wa upinzani wa kutaka kurejewa uchaguzi huo wenye utata, baada ya ujumbe wa waangalizi wa Kanisa Katoliki kudai kuwa kulikuwa na ''kasoro na udanganyifu'' katika zoezi hilo la kidemokrasia.

Jumatano iliyopita, askari polisi wa Kongo DR walirusha mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wafuasi wa upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa, wanaotaka kurudiwa uchaguzi wa rais na wabunge uliokumbwa na machafuko na mvutano mkubwa.

Viongozi wa upinzani nchini humo wanasisitiza kuwa, matokeo lazima yabatilishwe huku serikali ikishikilia msimamo wake kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.

Kati ya kura zaidi ya milioni 16 zilizohesabiwa hadi sasa na CENI, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, ambaye anatafuta muhula wa pili wa miaka mitano, anaongoza kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura zote.

Ghasia za Jumatano iliyopita jijini Kinshasa

Mgombea wa upinzani, Moïse Katumbi, ambaye ni gavana wa zamani wa eneo lenye utajiri wa madini la Katanga, anatazamiwa kushika nafasi ya pili, kwa asilimia 14 ya kura, akifuatiwa na Martin Fayulu, (4%).

Wapiga kura milioni 44 walijiandikisha kupiga kura kuwachagua viongozi wao, ambapo wagombea wa nafasi ya urais ni 20 akiwemo Rais Tshisekedi anayesaka awamu ya pili. Wakongomani pia walipiga kura kuwachagua wabunge wa kitaifa na wa mikoa, na madiwani wa serikali za mitaa.

Ikumbukwe kuwa, uchaguzi wa Tshisekedi kama rais mwaka 2018 ulikumbwa na shutuma za wizi wa kura na udanganyifu. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 34 waliuawa na wengine 59 kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Tags