Ethiopia yatia saini makubaliano ya bandari ya kihistoria na Somaliland
(last modified Tue, 02 Jan 2024 03:27:16 GMT )
Jan 02, 2024 03:27 UTC
  • Ethiopia yatia saini makubaliano ya bandari ya kihistoria na Somaliland

Ethiopia imefikia makubaliano ya kihistoria ya kutumia bandari kuu katika eneo lililojitenga la Somalia, la Somaliland wakati nchi hiyo isiyo na eneo lililoungana na bahari ikitafuta ufikiaji zaidi wa njia za baharini kwa meli. Haya yalibanishwa jana na maafisa wa pande mbili.

Makubaliano kuhusu kutumia bandari ya Berbera ya Somaliland yamefikiwa miezi kadhaa baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kusema nchi yake, ambayo ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika, itatetea haki yake ya kufikia Bahari Nyekundu, na hivyo kuzua wasiwasi miongoni mwa nchi jirani.

Makubaliano ya kihistoria kati ya Ethiopia na Somaliland

Katika pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden, bandari ya Berbera inahesabiwa kuwa lango kuu la Kiafrika katika Bahari ya Sham na kaskazini kuelekea upande wa  mfereji wa Suez.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imeeleza kuwa hati ya makubaliano (MOU) kati ya Ethiopia na Hargeisa, makao makuu ya serikali ya Somaliland, ilitiwa saini na Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia. Imeongeza kuwa, makubaliano hayo yatafungua njia  Ethiopia ili kutimiza azma yake ya kufikia baharini na kutumia pakubwa huduma za bandari na wakati huo kuimarisha ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa kati ya Ethiopia na Somaliland.