Maelfu ya wakimbizi wagawiwa chakula Kivu Kusini DRC
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetangaza kuwa, limewagawia chakula maelfu ya wakimbizi katika mkoa wa Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo kuanzia jana kazi ya kuwagawia chakula wakimbizi hao ilianza katika eneo la Kabare huko Kivu Kusini na kwamba, mpango huo unatarajiwa kuwajumuisha wakimbizi elfu 11 na 320.
Mpango huo unatekelezwa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ili kujaribu kukidhi mahitaji ya chakula ya wakimbizi hao ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa chakula, imeeleza taarifa hiyo.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Ukosefu wa usalama katika maeneo hayo umepelekea raia wengi walazimike kuyakimbia makazi yao na hivyo kuwa wakimbizi.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushindwa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa MUNUSCO na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuyatokomeza makundi ya wanamgambo ndiko kulikoshadidisha ukosefu wa amani na uthabiti mashariki mwa nchi hiyo.