Jan 13, 2024 11:51 UTC
  • Askari 2 wa baharini wa US 'watoweka' pwani ya Somalia

Mabaharia wawili wa Jeshi la Majini la Marekani wameripotiwa kutoweka wakiwa katika operesheni ya kijeshi Pwani ya Somalia; wakati huu ambapo taharuki imeongezeka baina ya vikosi vya Yemen na Marekani katika Bahari Nyekundu.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) iliripoti habari hiyo jana Ijumaa na kufafanua kuwa: Jioni ya Januari 11, mabaharia wawili wa Jeshi la Majini la Marekani waliripotiwa kutoweka baharini wakifanya operesheni katika pwani ya Somalia.

CENTCOM imedai kuwa, eti kwa sababu za kiusalama na kwa ajili ya heshima kwa familia za mabaharia hao, haitatoa taarifa zaidi kuhusu askari hao waliotoweka.

Haijabainika iwapo maharamia au wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamehusika kivyovyote na kutoweka kwa askari hao wa US au la.

Haya yanajiri miezi michache baada ya kiongozi mwandamizi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia kuitishia na kuionya Marekani kufuatia shambulizi la anga la hivi karibuni lililofanywa na ndege za kivita za US kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Mahad Karate alidai kuwa, Marekani ni kizingiti katika kupatikana uthabiti nchini Somalia, na kwamba Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) imekuwa ikiwalenga raia wasio na hatia katika hujuma zake nchini Somalia.

Karate alisisitiza kuwa, wanachama wa al-Shabaab watalipiza kisasi kwa shambulio la anga la Marekani la Septemba 6 mwaka jana katika eneo la el-Laheley karibu na mji bandari wa Kismaayo, mkoa wa Lower Juba. Alidai kuwa shambulio hilo liliua makamanda watatu wa al-Shabaab na raia watano wakiwemo watoto wanne.

Ripoti kadhaa za shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International pia zinaonesha kuwa, jeshi la Marekani linaendelea kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Tags