Waziri Mkuu wa UK: Nitapuuza sheria ya kimataifa kuhusu kuwapeleka wahamiaji Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i107408-waziri_mkuu_wa_uk_nitapuuza_sheria_ya_kimataifa_kuhusu_kuwapeleka_wahamiaji_rwanda
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameendelea kung'ang'ania mpango wa serikali ya London wa kuhamishia waomba hifadhi nchini Rwanda, akisisitiza kuwa yuko tayari kupuuza sheria ya kimataifa ambayo imezuia kwa muda utekelezaji wa mpango huo tata.
(last modified 2024-01-20T04:02:33+00:00 )
Jan 20, 2024 04:02 UTC
  • Waziri Mkuu wa UK: Nitapuuza sheria ya kimataifa kuhusu kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameendelea kung'ang'ania mpango wa serikali ya London wa kuhamishia waomba hifadhi nchini Rwanda, akisisitiza kuwa yuko tayari kupuuza sheria ya kimataifa ambayo imezuia kwa muda utekelezaji wa mpango huo tata.

Shirika la habari la Russia Today liliandika habari hiyo jana Ijumaa na kumnukuu Sunak akisema kuwa: Nimeweka bayana kuwa, sitaruhusu mahakama ya kigeni ituzuie kutekeleza mpango huu.

Kauli ya Sunak imekuja baada ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya (ECHR) kupasisha dikrii nambari 39, ambayo imesimamisha kwa dharura na kwa muda mpango wa kuwapeleka Rwanda wahamiaji na waomba hifadhi walioko Uingereza.

London imekuwa ikisisitiza kuwa, itaingia makubaliano mapya na Kigali kwa ajili ya kufufua mpango wake huo wa kuhamishia waomba hifadhi Rwanda, licha ya hukumu ya Mahakama ya Juu ya Uingereza kusema mpango huo ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Wabunge wa Uingereza mwezi uliopita wa Disemba walipiga kura kuunga mkono mpango huo tata wa Rishi Sunak, wa kupeleka wahamiaji walioko nchini humo katika nchi ya Rwanda.

Maandamano ya kupinga mpango wa kuwapeleka Rwanda wahamiaji na waomba hifadhi walioko Uingereza

Sunak amekuwa akipigia debe mpango huo akidai kuwa, watu wa Uingereza ndio wanaopaswa kuamua ni nani atakayeingia nchini humo na si magenge ya uhalifu au mahakama za nchi za kigeni.

Mahakama ya Juu ya Uingereza ilisema mwaka uliopita kwamba, mpango wa serikali ya London wa kuwapeleka nchini Rwanda wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo unakiuka sheria. Ilisema mpango huo unawaweka katika hali hatarishi wakimbizi hao, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao waliikimbia nchi yao ya Rwanda na kuwarejesha huko ni kuwaweka hatarini.

Mpango huo wa serikali ya Uingereza umekuwa ukipingwa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, wanaosema Rwanda haiwezi kuwa nchi salama kwa wakimbizi na wahamiaji hao.