Tshisekedi ameapishwa leo, makumi ya viongozi wa nchi wamehudhuria
(last modified Sat, 20 Jan 2024 13:48:48 GMT )
Jan 20, 2024 13:48 UTC
  •  Tshisekedi ameapishwa leo, makumi ya viongozi wa nchi wamehudhuria

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, ameapishwa hii leo Jumamosi kwa muhula wa pili wa miaka mitano baada ya Mahakama ya Katiba kuthibitisha ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwezi Desemba mwaka jana.

Sherehe za kuapishwa kwake zimefanyika katika uwanja wa michezo wa Martyrs jijini Kinshasa.

Rais Tshisekedi anatarajiwa kuongoza taifa hilo kwa muhula mwengine  huku baadhi ya maeneo ya nchi hiyohusan mashariki mwa nchi hiyo yakikabiliwa na machafuko, suala ambalo ameahidi kulikomesha.

Viongozi  18 kutoka mataifa mbalimbali mapema waliwasili jijini Kinshasa kwa ajili ya sherehe hiyo.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Congo DR (CENI) ilitangaza kuwa Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 73.47 ya kura, akkifuatiwa na Moïse Katumbi Chapwe, ambaye alipata asilimia 18.08 ya kura. Nafasi ya tatu ilichukuliwa Martin Madidi Fayulu ambaye alipata asilimia 5.33 ya kura. 

Felix Tshisekedi

Kambi ya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia yalitoa wito wa kurudiwa uchaguzi wa rais wa Congo yakidai kwamba uligubikwa na matatizo makubwa ya vifaa ambayo yalitilia shaka uhalali wa matokeo yake.

Tshisekedi aliingia madarakani kwa mara ya kwanza Januari 2019, baada ya kumshinda Joseph Kabila.Tshisekedi ni mtoto wa kiume wa mwanasiasa wa upinzani, Etienne Tshisekedi.

Awali kiongozi huyo alikuwa ameahidi kuboresha hali ya maisha nchini DRC, nchi ambayo inajivunia utajiri wa madini lakini ina wakazi maskini zaidi ya milioni 100. Vilevile aliahidi na kukomesha mapigano ya karibu miaka 25 mashariki mwa nchi hiyo.

Tags